Header Ads

RUFAA YA DDP V ZOMBE KUANZA LEO




Na Happiness Katabazi
 
MAHAKAMA ya Rufaa nchini leo inatarajia kuketi Dar es Salaam na kuaza kusikiliza  rufaa iliyokatwa na   Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake na kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu  katika kesi ya mauji Na.26/2006 ambayo iliwaachiria huru Zombe na wenzake.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama ya rufaa  ambayo gazeti hili imeona nakala ya ratiba hiyo, inaonyesha rufaa hiyo inayosubiriwa kwa shauku kubwa na umma itasikilizwa kwa siku mbili mfululizo yaani leo na kesho.

Rufaa hiyo itasikilizwa mbele ya majaji wa tatu wanaongozwa na Jaji Natharia Kimaro,Catherine Oriyo na Semistocles Kaijage.

Upande wa mwomba rufaa(DPP), unawakilishwa na jopo la mawakili waandamizi wa serikali saba ambao ni Mgaya Mtaki, Timon Vitalis,Edward Kakolaki, Angaza Mwipopo, Prudence  Rwenyongeza ,Alexanda Mzikila na Peter Njike .

Wakati upande wa wajibu rufaa unawakilishwa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na washtakiwa wengine wanatetewa na mawakili Majura Magafu, Denis Msafiri, Deodoras Ishengoma

Itakumbukwa kuwa Desemba 12 mwaka jana,rufaa ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa lakini ilishindikana kuanza kusikilizwa kwasababu Jaji Kaijage alikuwa mgonjwa.

Agosti 17  mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kihistoria ya kesi ya mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake ambapo jaji Salum Massati ambaye hivi sasa ni jaji wa mahakama ya rufani aliwaachilia huru Zombe na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi hiyo kwa maelezo kuwa upande wa jamhuri ulishindwa kuleta ushahidi mzuri ambao ungewea kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.


Baada ya hukumu hiyo ya mahakama kuu, DPP hakulidhishwa na hukumu hiyo Oktoba 7 mwaka 2009 akakata rufaa Mahakama ya Rufaa ,  kupinga hukumu hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama ya rufaa,rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa jana lakini ikashindikana.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi na jana washtakiwa wote walifika mahakamani hapo.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Aprili 22 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.