Header Ads

KOMENI KUJADILI MWENENDO WA KESI YA LWAKATARE NJE YA MAHAKAMA 
 
Na Happiness Katabazi

BAADHI ya wabunge,wanahabari na wananchi wengine wote wanaoijadili kesi ya jinai PI,6/2013 ya Jamhuri Vs Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph iliyopo mbele ya Hakimu
MKazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,Alocye Katemana,ama wana matatizo ya akili  au ni mambumbumbu wa sheria.

Ndiyo maana wameamua kwa makusudi kuingiza uhayawani wao kwa kuijadili kesi hiii nje ya mahakama wakati tayari mawakili wa upande wa Jamhuri walishaieleza mahakama Machi 22 mwaka huu, siku kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa kuwa upelelezi bado haujakamilika na kesi hiyo ikaarishwa hadi Aprili 17 mwaka huu, kwaajili ya kuja kutajwa.

Na kesho (Aprili 15 mwaka huu), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lawrence Kaduri atasikiliza ombi lilowasilishwa na Lwakatare mahakamani hapo linaloomba mahakama hiyo iyaite majalada ya kesi ya msingi iliyopo Kisutu na iyapitie.
Ninashangaa sana si mahakama, bunge wala hiyo wizara ya habari haipigi marufuku vyombo vya habari kuchapisha au kutangaza maoni ya watu wanaoijadili mwenendo wa kesi hiyo nje ya mahakama kwani mjadala huo unaonyesha wazi watu wanaijadili kesi hiyo nje ya mahakama kwasababu za kijinga wanazozijua wao.

Lakini hao hao wanaoijadili kesi hiyo ya Lwakatare nje ya mahakama na wengine eti wanajifanya wanamuonea huruma sana Lwakatare wakati ni wanafki ,hatujawaona wala kuwasikia hata siku moja wakibeba hata dumu moja la maji ya uhai wakampelekea maji katika gereza la Segerea Lwakatare.

Tunachokiona wanajitafutia umaarufu wa kipuuzi kwa kuijadili kesi ya Lwakatare ambapo kwa ujinga wao huo wanaoufanya hawajui ama wataendelea kumkandamiza Lwakatare bila sababu za msingi.

Tuwaulize hawa wabunge wanaojifanya wanaijadili sana hii kesi hiyo, wao si ni wabunge wa wananchi?, mbona huko majimboni mwao kuna wanachi wao tena waliowapigia kura nao wamefunguliwa kesi za zinazotaka kufanana na hizo kama za mauji, utakatishaji fedha haramu ambazo nazo ni kama kesi ya ugaidi inayomkabili Lwakatare ambazo hazinaga dhamana, mbona wabunge hawa wapayuki kama hivi kuwatetea wananchi hao na kusema kuwa wamebambikiwa kesi?

Kwa nini baadhi ya waandishi wahabari,baadhi ya wanasiasa uchwara ambao ni maamuma wa sheria kutwa kuijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama kuwa kesi hiyo ni ya kubambikiwa?

Mbona tumemshuhudia aliyekuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba, Daniel Yona, Rajabu Maranda, David Mattaka,Idd Simba na watu wengine wenye nyadhifa kubwa walipofunguliwa kesi pale Mahakama ya Kisutu, mbona wanasiasa nyie hamkujitokeza kupayuka adharani kuwa nao wamebambikiwa kesi?

Sana sana ninachokumbuka hawa hawa wanasiasa wa upinzani ambao kipindi hicho cha mwaka 2008 ndiyo walikuwa wakishinikiza serikali iwafikishe mahakamani vigogo wa CCM ambao wanatuhumiwa kwa ufisadi na kweli baadhi ya vigogo waliokuwa wakituhumiwa walifikishwa na wengine walipatikana na hatia wakafungwa kama aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, Kada wa CCM, Rajabu Maranda na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin wakashinda kesi yao uhujumu uchumi.

Wakiwemo wanasiasa na wanahabari walianza kusema kesi hizo ni danganya toto na hakuna atakayekutwa na hatia lakini mwisho wa siku baadhi ya washitakiwa walikutwa na hatia.
Na hiyo ndiyo aina ya wananchi wa nchi yetu wa Tanzania, kwanza wengi wetu tumejenga kasumba ya kudandia gari kwa mbele yaani ‘kujadili hoja fulani bila kujua undani na uhalisia wake’.

Pili, tunapenda sana kushinikiza hatua fulani zichukuliwe dhidi ya watu fulani bila hata ya kufahamu kuwa suala la kumfikisha mtu mahakamani linahusisha wanataaluma ambao ni wapelelezi na wanasheria.
Hawa ndiyo tumewapa jukumu la kupeleleza na kuwafungulia kesi watuhumiwa mahakamani pindi wanapoona kuna ushahidi wa kuweza kuwafungulia kesi.

Lakini mbaya zaidi vyombo hivyo vinapoanza kufanyakazi kwa watu ambao sisi tunamapenzi na maslahi binafsi na washitakiwa ambao wamefunguliwa kesi mahakamani ,basi ni sisi tunageuka na kuanza kuvishutumu vyombo hivyo kuwa vinaonea watu na kuwabambikizia kesi watu.

Sisi wasomi wa sheria tunasema kwamba jukumu la kusema mshitakiwa ametenda kosa au hajatenda kosa ni la mahakama siyo la wanasiasa ‘uchwara ’ ambao wanataka kuparamia majukumu ya mahakama ya kutoa haki na kutafsiri sheria wakati jukumu la mhiri wa bunge na wabunge ni kutunga sheria.

Ni wabunge hawa hawa ambao leo hii wanaijadili kesi ya Lwakatare ilipo mahakamani, ndiyo bunge lao limetunga sheria hiyo ya ugaidi, lakini leo hii sheria hiyo imetumika kumshitaki Kaka yangu Lwakatare ambaye sijui ni mwanasiasa mwenzao wanaiona mbaya.Tuwahoji siyo wao ndiyo waliyoipitisha sheria hii au sheria hii ilipitishwa na mashetani?

Hivi sini hawa wabunge ndiyo kutwa tunawasikia wakilalamika kuwa mhimili wa serikali unauhubuza mhimili wa bunge na kwamba hawapendi hiyo tabia?

Sasa sisi wadau wa mahakama tunatoa rai kwa mhimili wa mahakama utoe amri ya kuitaka jamii,wabunge, vyombo vya habari kuacha mara moja kuijadili kesi ya LWakatare nje ya mahakama.Na hili linawezekana kwani nakumbuka mwaka 2007 Jaji Salum Massati wakati akiwa jaji wa Mahakama Kuu, alitoa amri ya kuzuia mtu yoyote kulijadili suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi hadi shauri lilokuwa mbele yake ambalo lilifunguliwa mahakamani hapo na Mchungaji Christopher Mtikila ,atakapolitolea uamuzi.

Madhara ya kuacha jambo hili lijadiliwe nje ya mahakama ni wazi linapandikiza chuki baina ya ndugu na familia ya Lwakatare na serikali.Maana Serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), DK.Eliezer Feleshi ndiyo aliyeifungua kesi hii kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 9 cha Sheria ya Usimamizi wa Mashitaka ya mwaka 2008.

Na nyie wanahabari mnaojifanya kuijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama, kama siyo unafki na kutumika vibaya na upande mmoja wa vyama vya siasa ni kitu gani.? 

Ina maana nyie wanahabari mpo karibu sana na Lwakatare kuliko wanahabari wenzenu ambao ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari ,Absalom Kibanda na Samson Mwigamba na Theophil Makunga ambao nao wanakabiliwa na kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi katika gazeti la Tanzania Daima mwaka 2011 na kesi hiyo ipo mbele ya hakimu mkazi Waliarwande Lema katika mahakama hiyo ya Kisutu?

Mbona wanasiasa,na nyie wanahabari mnaoijadili kesi ya Lwakatare kuwa amebambikiwa kesi, mbona amuonyeshi kuandika makala za aina hiyo za kusema nao wanahabari hao kutwa mnafanyanao kazi miaka nenda rudi kuwa nao walibambikiwa kesi?

Kuna nini hapa katika kesi ya Kaka yangu Lwakatare?Au kwasababu Lwakatare ni kiongozi wa kisiasa?

Napenda kuwashauri wale wote wanaoijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama, hamsaidii Lwakatare zaidi hayo maneno yenu mnayopayuka huko nje yatazidi kumgandamiza kwa njia moja au nyingine kwasababu sisi wasomi wa sheria tunasema hizo blabla zenu hazina mashiko (Merit).

Si mnadai Lwakatare amebambikwa kesi ina maana mnaushahidi na hilo, basi ili mmsaidie Lwakatare aepukane na balaa hilo nyie wanahabari ambao hata mlango wa mahakama ya Kisutu wala hata ya mashitaka ya kesi hiyo hamjaisoma wala kuiona, ni vyema mkaenda pale jengo la Sukari House, muombe kuonana na DPP-Dk.Feleshi na kisha mumueleze kwa vielelezo kuwa kesi hiyo ya PI 6/2013 R v Lwakatare,Ludovick ni ya kupikwa na ushahidi wa kuthibitisha hayo mmpatie.

Wanasiasa hasa nyie wabunge ,mjirekebishe na mtambue kuwa porojo zenu mlizozoea kuzitoa majukwaani na kutoa ahadi za uongo kwa wananchi kupitia majukwaa ya siasa,hazikubaliki mahakamani hata chembe na wala mwisho wa siku haziwezi kuishawishi mahakama imuone mshitakiwa ana hatia au la.

Mambo yanayohusu kesi mahakamani kwa taarifa yenu yanazingatia, sheria, kanuni na ushahidi, hizo porojo zenu wala mahakama haizitaki.

Lakini porojo hizi za wanasiasa hawa uchwara wanazozitoa katika kesi ya ugaidi ya Lwakatare, hazinishangazi kwani hata mwanasiasa mkongwe na msomi nchi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Sheikh Ponda alipofikishwa katika Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza na wenzake 49, Oktoba 18 mwaka jana, Lipumba alijitokeza adharani katika mikutano yake na waandishi wa habari tena bila haya akasema kuwa kesi hiyo inayomkabili Sheikh Ponda ambayo ni ya makosa ya uchochezi wizi wa malighafi wa Sh.milioni 59 ambayo inatarajiwa kutolewa hukumu na hakimu Victoria Nongwa, Aprili 18 mwaka huu.

Bila haya Profesa Lipumba alisema kesi hiyo ni ya madai lakini anashangazwa na DPP kuifungua kesi hiyo kuwa ni ya jinai.Sisi wasomi wa sheria tulimpuuza na ninakumbuka niliandika makala ya kumpinga Lipumba iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho (PROFESA LIPUMBA NI MBUMBUMBU WA SHERIA).

Na Machi 4 mwaka huu, hakimu Nongwa alitoa uamuzi wake ambao alimuona Ponda na wenzake wanakesi ya kujibu na akatupilia mbali hoja ya wakili wa Ponda, Juma Nassor iliyokuwa ikidai kuwa kesi hiyo ni ya madai, ambapo hakimu alisema kesi hiyo siyo ya madai na kwamba kesi hiyo ni ya jinai.

Kwa hiyo niitimishe kwa kuwaasa wabunge wetu ambao mmeshupaza shingo kuijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama na nyie baadhi ya wanahabari wetu, kuwa sheria haina urafiki, na sheria ni msumeno na kwamba make mkijua kufunguliwa kesi ni hatua nyingine, kukutwa na hatia au kuachiliwa ni hatua nyingine.Kwahiyo Lwakatare yeye yupo kwenye hatua ya kufunguliwa kesi hiyo ambayo haina dhamana bado hajatiwa hatiani.

Hivyo ni vyema basi tuiachie mahakama, na mawakili wa pande zote mbili katika kesi hiyo ya mawakili wa utetezi na upande wa jamhuri wafanyekazi yao ya kisheria ya kuisaidia mahakama mwisho wa siku ifikie uamuzi wa kutoa maamuzi ya haki na si vinginevyo.

Wengi wanaojifanya leo hii wanaisemea hiyo kesi ya Lwakatare ukiwauliza walishatoa hata mchango wa nauli kwa mke wake Lwakatare wa kumuwezesha kila siku kumpelekea mume chakula Gerezani, hawajawahi kufanya hivyo.

Nina uzoefu mkubwa wa kuripoti kesi mbalimbali mahakamani kwa zaidi ya miaka 13 sasa.Nimejifunza kuwa ukiwa unashitakiwa ukae ukijua ndiyo umaskini umeukajilibisha ndani ya nyumba, utakimbiwa na marafiki na ndugu zako na familia yako ndiyo watakaoangaika na wawe kwa karibu,na wale uliokuwa nao wakati wa raha watakukumbia.

Sasa ndugu wa kaka yangu Lwakatare walitambue hilo,Lwakatare alipokuwa hajakumbwa na matatizo ya kesi hii alikuwa anaheshimiwa na kuthaminiwa sana na muda wote watu walikuwa wakitaka kuwanae karibu kwaajili ya shughuli za kikazi lakini.

Leo hii amepatwa na kesi hii ni wazi ndugu na jamaa wa kaka yangu Lwakatare nawataka mtegee kuona watu hao wakiwa mbali kabisa na familia ya Lwakatare na wengine itafikia mahala mkiwapigia simu watakuwa hawapokei, na hao leo hii wanaojifanya wanaisemea kesi yake nje ya mahakama ,mwisho wa siku watanyamaza kimya, na nyie ndugu wa familia ndiyo msalaba wa majukumu ya kumpelekea chakula gerezani Kaka Lwakatare litakuwa kwenu.

Hivyo nashauri ni vyema mkawakataza wale wote wanaotaka kuigeuza kesi ya ndugu yenu kuwa ni mtaji wao kisiasa wakijipatia umaarufu wa chee.Tumieni muda mzuri wakuwa karibu na mawakili wa Lwakatare,puuzeni porojo za wanasiasa.

Mwisho, nyie baadhi ya wanasiasa na wanahabari tuheshimu taaluma za watu wengine yaani wanasheria ,wapelelezi na mahakama.Na hiyo ndiyo zana nzima ya mgawanyo wa madaraka yaani (Separetion of Power).

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika

0716 -774494

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com ; Aprili 14 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.