MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana imempatia
dhamana mfanyabiashara Razah Hussein Razah na wenzake 10,
wanaokabiliwa na makosa 24 ya kuua bila kukusudia watu walioangukiwa
na ghorofa katika mtaa wa Indira/ Gandi hivi karibuni.
Mbali na Razah washtakiwa wengine ni Godluck Mbaga, Wilbroad
Mugabisyo, Ibrahim Kisoki, Mohamed Abubakar, Charles Salu, Zonazea
Anage, Vedasto Ferand, Michael Hemed, Albert Jones na Joseph Ringo
wanaotetewa na wakili Adronicus Byamungu.
Mawakili waandamizi wa serikali, Bernad Kongora , Tumaini Kweka,
Lasdiraus Komanya na Mahugo waliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo
jana ilikuja kwa ajili ya mahakama hiyo kutolea uamuzi wa ama ina
mmlaka ya kutoa dhamana kwa kesi hiyo ya kuua bila kukusudia au la.
Hakimu Devota Kisoka alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili
ambapo mawakili wa utetezi siku ya kwanza ilipofunguliwa kesi hiyo
Aprili 3, mwaka huu, waliomba washtakiwa hao wapewe dhamana.
Aliongeza kuwa mawakili hao wa utetezi walidai kuwa katika kesi ya
jinai No.34/2008, Jaji Thomas Mihayo katika uamuzi wake alizitaka
mahakama za chini zinazoendesha kesi zinazotakiwa kusikilizwa na
mahakama kuu, zinapokuwa katika hatua za awali, zinatakiwa ziwapatie
dhamana washtakiwa hao.
Alisema kuwa mawakili wa serikali, siku hiyo walipinga wakidai kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya kuua bila
kukusudia na kwamba ni mahakama kuu pekee yenye mamlaka ya kusikiliza
na kuitolea uamuzi.
“Nilizisikiliza hoja za pande zote mbili na mahakama hii imefikia
uamuzi wa kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kwamba mahakama
hii inao uwezo wa kutoa dhamana katika kesi hiyo, kwani mahakama kuu ni
mahakama ya rekodi na inapotoa mwongozo wake katika mahakama za chini,
basi ni lazima mahakama za chini ziufuate,” alisema Kisoka.
Alifafanua kuwa ameisoma vizuri kesi hiyo Na 34/2008 ambayo Jaji
Mihayo alitoa mwongozo huo kwa mahakama za chini akisema kuwa mahakama
hiyo ni miongoni mwa zile za chini, hivyo imefikia uamuzi wa kuwapatia
dhamana washtakiwa wote kwa masharti.
Kisoka alifafanua kuwa ili washtakiwa wapate dhamana ni lazima kila
mmoja awe na mdhamini atakayesaini bondi ya sh milioni 20, kusalimisha
hati ya kusafiria itakayohifadhiwa polisi, kutotoka nje ya mkoa au nchi
bila kibali cha mahakama.
Hata hivyo wakili wa serikali Kongora aliomba mahakama kuwa wakati
ikitoa dhamana izingatie masharti ya kifungu cha 148(6),(7) cha Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai mwaka 2002 na kwamba upande wa jamhuri
unaomba barua zinazowatambulisha wadhamini wapatiwe ili waweze kwenda
kuzikagua.
Ombi hilo lilikubaliwa na hakimu Kisoka ambapo alipokea barua za
wadhamini na maelezo hayo kisha akaiahirisha kesi hiyo hadi leo kwa
ajili ya kutoa nafasi kwa upande wa jamhuri kwenda kujiridhisha.
Itakumbukwa kuwa Machi 29, mwaka huu, jengo la ghorofa 16 lililokuwa
linajengwa katika mtaa wa Indira Ghandi lilianguka na kusababisha vifo
vya watu 34 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Aprili 17 mwaka 2013.
|
|
No comments:
Post a Comment