TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), jana
ilimfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya
Makazi, Simon Lazaro, kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na wizi
sh milioni 100 mali ya serikali.
Mbali na Lazaro wakili wa TAKUKURU, Leonard Swai, mbele ya Hakimu
Mkazi, Aloyce Katamana, aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Mkurugenzi
Mkuu wa Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi, Gerald Mango, na Kaimu Mhasibu
Mkuu wa tume hiyo, Charles Kijumbe.
Wakili Swai alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Lazaro peke yake
anashtakiwa kwa kosa la kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mwajiri wake
na kwamba kosa hilo alilitenda Mei 18 mwaka jana, katika wizara hiyo.
Alidai kuwa akiwa mwajiriwa wa wizara hiyo kwa cheo cha Kaimu
Mkurugenzi wa Sera na Mipango, kwa makusudi aliwasilisha nyaraka hizo
za uongo kwa mwajiri wake zinazoonyesha amepokea sh milioni 100 kutoka
Tume ya Taifa ya Matumizi bora ya Ardhi kwa ajili ya kufanyia kazi ya
upimaji wa ardhi katika wilaya za Babati, Kilolo na Bariadi wakati
akifahamu nyaraka hizo ni za uongo.
Kosa la pili ni la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha
31 cha Sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007, kwamba washtakiwa wote watatu
kati ya Julai 4 na Agosti 5 mwaka 2011, wakiwa ni waajiriwa wa wizara
hiyo walitumia madaraka yao vibaya kinyume cha kanuni ya 87(1) na
86(1) ya kanuni ya fedha za umma ya mwaka 2004.
Wakili Swai alidai shtaka la tatu linalomkabili Lazaro peke yake ni
ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma ambalo ni kinyume na kifungu cha
28(1) cha Sheria ya TAKUKURU mwaka 2007, ambalo alilitenda kati ya
Julai 4 na Agosti 5 mwaka 2011.
Aliongeza kuwa alitumia fedha za umma sh milioni 100 alizozipokea
toka Tume ya Taifa ya Matumizi bora ya Ardhi kwa manufaa yake binafsi
wakati fedha hizo zilitolewa na wizara kwa ajili ya kupimia ardhi
katika maeneo ya Arusha, Muleba, Ngorongoro, Songea, Kilosa na Mpanda.
Alilitaja shtaka la nne kuwa ni mbadala wa kosa la tatu linalomkabili
Lazaro, kuwa ni la wizi kinyume cha kifungu cha 258 cha Sheria ya
Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Swai alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Julai 4 na Agosti 5
mwaka 2011 akiwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo
ambapo aliiba sh milioni 100 zilitolewa na tume kwa wizara kwa ajili ya
upimaji ardhi katika maeneo tajwa.
Washtakiwa hao walikana mashtaka hayo na wakili Swai alidai upelelezi
wa kesi hiyo umekamilika na kwamba anaiomba mahakama ipange tarehe ya
kuja kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa.
Hakimu Katemana alisema kuwa makosa yanayowakabili washtakiwa yana
dhamana na kwamba Lazaro peke yake anatakiwa awe na wadhamini wawili wa
kuaminika ambao watasaini bondi ya sh milioni 50 na barua za
utambulisho wa ofisi zinazotambulika.
Mshtakiwa wa pili na wa tatu walitakiwa wawe na wadhamini wa
kuaminika ambao watasaini bondi ya sh milioni 25. Na washtakiwa wote
walitimiza masharti na wakapewa dhamana huku kesi hiyo ikiahirishwa
hadi Aprili 30.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Aprili 17 mwaka 2013.
|
No comments:
Post a Comment