HEKO OFISI YA DPP,POLE WAFUASI WA SHEIKH PONDA
Na Happiness Katabazi
MACHI 21 mwaka huu, Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Sundi Fimbo
aliwahukumu wafuasi 53 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Sheikh Ponda
Issa Ponda kwenda jela mwaka mmoja baada ya kuwatia hatiani kwa makosa matatu
likiwemo kosa la kufanya maandamano haramu ya kutaka kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi kumshinikiza ampatie dhamana
Ponda.
Hakimu Fimbo alisema
alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa
na makosa manne ambapo mshitakiwa Salum Bakari
Makame na wenzake 52 wanaotetewa na wakili wa kujitegemea Mohamed
Tibanyendera.
Kosa la kwanza ni la kula njama
kutenda kosa kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka
2002, kosa la pili ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifungu cha 74 na
75 cha sheria hiyo ambavyo vinasomwa pamoja na kifungu cha
43(2)(4) na 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002 , kuwa Februali 15
mwaka huu, walitenda kosa hilo la kutaka kuandama kwenda katika ofisi ya
Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka ,Dk.Eliezer Feleshi kumshinikiza ampatie dhamana
Sheikh Ponda,kwani Feleshi amemfungia dhamana Ponda tangu Oktoba 18 mwaka jana
hadi leo hii.
Kosa la tatu ni la
kukaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka watawanyike ambalo ni kinyume na
kifungu 79 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kinachosomwa pamoja na kifungu cha
44 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002 na kosa la
nne ni la uchochezi ambalo lilikuwa likiwakabili washitakiwa
watatu tu ambao ni Makame, Said Idd, Ally Nurdin Nandumbi ambao
wote hawa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), aliwafungia dhamana tangu walipofikishwa
kwa mara ya kwanza mahakama ni hapo Februali 18 mwaka huu.
Hakimu Fimbo alisema
ili kuthibitisha kesi yao upande wa jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na
mawakili waandamizi wa serikali Bernad Kongora,Peter
Ndjike,na Joseph Mahugo na walileta jumla ya mashahidi 10 na
upande wa utetezi walileta jumla ya mashahidi 54.
“Baada ya kujiuliza
maswali hayo mahakama hii imefikia uamuzi wa kuwaona washitakiwa 52 walitenda
kosa la kula njama isipokuwa mshitakiwa wa 48 (Waziri Omar Toli) hakutenda kosa
hilo kwa sababu alikutwa akitoka kununua mabeseni, mahakama hii imewatia hatiani
kwa kosa hilo kwani kwa mujibu wa vielelezo vilivyoletwa mahakamani yaani barua
iliyoandikwa na Taasisi ya Jumuiya ya Maimamu kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar
es Salaam kuomba kibari cha maandamano na polisi wakawakataza ila wakaandamana,
washitakiwa wengine walikamatwa na vipeperushi, mabango,vipaza sauti vinavyosema
‘Dpp ukristo utakuponza’:
“Kwa
vielelezo hivyo mahakama hii imeridhika kwamba walitenda kosa la kwanza,
la pili na la tatu na kosa la nne ambalo ni la
uchochezi mahakama hii imeona upande wa jamhuri umeshindwa kulithibitisha na
kwasababu hiyo mahakama hii imewatia hatiani kwa washitakiwa wote
kwa makosa matatu isipokuwa mshitakiwa 48 ametiwa hatiani kwa kosa la tatu tu”
alisema Hakimu Fimbo.
Akilichambua kosa la
pili ambalo ni la kufanya mkusanyiko haramu, hakimu huyo alisema pia mahakama
inamuachilia huru mshitakiwa wa 48 katika kosa hilo,isipokuwa
washitakiwa wengine wote wametiwa hatiani kwa kosa hilo kwasababu walikutwa
katika maeneo tofauti wakitenda kosa hilo na katika utetezi wake walitoa walitoa
ushahidi unaopishana ambao wengine walidai kuwa wa walikuwa wameenda kununua
bidhaa,na walikuwa na fedha mfukoni lakini hata hivyo kiwango cha fedha
walichokitaja polisi,na mahakamani ni tofauti ‘alisema hakimu Fimbo.
Hakimu huyo alisema kila kosa
alilowatia nalo hatiani watalitumikia kifungo ha gerezani kwa mwaka mmoja,hivyo
washitakiwa hao watatumikia adhabu ya mwaka mmoja jela.
Baada ya kumuliza kutoa hukumu hiyo,
ndugu na jamaa wa washitakiwa hao waliigeuza mahakama na viunga vyake
ni sehemu ya msiba kwani walianza kuangua vilio kwa sauti ya juu na
kusababisha wanausalama kuwatoa nje.
Kesi hii ya kihistoria
ilifunguliwa rasmi Februali 18 mwaka huu,saa nane mchana na siku
hiyo hiyo upande wa jamhuri uliwasomea mashitaka na siku hiyo hiyo
ukasema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Februali
19 mwaka huu,upande wa jamhuri uliwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao na
shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum
ya Dar es Salaam, Hemed Msangi na mashahidi wengine walianza kutoa ushahidi
wao.
Februali
26 upande wa jamhuri ulifunga ushahidi wake.
Februali 28 washitakiwa walianza kujitetea na Machi
19 upande wa utetezi ulifunga utetezi.
Februali 20 mawakili
wa pande zote mbili waliwasilisha mahakamani kwa maandishi
majumuisho ya mwisho ambapo mawakili wa upande wa Jamhuri waliomba mahakama
iwatie hatiani washitakiwa wakati wakili wa utetezi
aliomba mahakama iwaachilie huru kwa sababu hawana hatia.
Machi 21 mwaka huu
mahakama hiyo ilitoa hukumu yake ambapo iliwahukumu washitakiwa wote kwenda jela
mwaka mmoja.
Kwanza kabisa napenda kuipongeza timu
ya mawakili wa serikali waandamizi iliyokuwa ikiongozwa na
Bernad
Kongora,Peter Ndjike,na Joseph Mahugo kwa kuweza kuleta ushahidi thabiti ambao
umeweza kuishawishi mahakama hadi ikawatia hatiani washitakiwa.
Pili,nalipongeza jeshi la polisi
ambao ndiyo walikuwa wakipeleleza kesi hiyo kwani waliweza
kufanyakazi yao ya kipelelezi kwa kasi ya ajabu ukilinganisha na
upelelezi wanaoufanya katika baadhi ya kesi nyingine ambao
uwachukua muda mrefu kukamilisha upelelezi huku wakiacha watuhumiwa wa kesi
mbalimbali kuendelea kusota gerezani.
Tatu, naupongeza uongozi wa Mahakama
nchini kwa kutoa agizo maalum la kutaka kesi hiyo na ile kesi ya inayomkabili
Ponda ambayo itatolewa hukumu Aprili 18 mwaka huu na hakimu Mkazi Victoria
Nongwa, kusikilizwa mfululizo kila siku wakati kesi nyingine ambazo
zimefunguliwa miaka mitano nyuma hazipata bahati hii ya mtende ya kusikilizwa
mfululizo.
Lakini pia nawapongeza mawakili wa
upande wa jamhuri na wakili wa utetezi Mohamed Tibanyendera kwa kuwaweza
kutimiza wajibu wao wa kitaaluma wa kuisaidia mahakama kutoa haki
bila kuingiza mbinu chafu za kuchelewesha kesi ambazo zimekuwa zikitumiwa na
baadhi ya mawakili wahuni na wababaishaji(Delay Ethnics).
Lakini pia binafsi napenda
kujipongeza mimi na waandishi wenzangu wa habari za mahakamani
kwani tumeweza kuiripoti kesi hii mwanzo hadi mwisho.
Pia
kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama yaani askari wa
Jeshi la Magereza na Polisi kwa kuimarisha ulinzi wa hali ya juu
mahakamani hapo siku zote wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa tena katika
mazingira magumu kwani ukumbi uliokuwa ukiendeshewa kesi hiyo ulikuwa hauna viti
vya kutosha, hakuna feni.Na ninaomba nisisitize ushirikiano wa waandishi wa
habari za mahakamani,mawakili ,wanausalama uzidi kuimarika.
Aidha napenda kutoa pole kwa
washitakiwa 53 waliohukumiwa kwenda jela mwaka mmoja, pamoja familia zao, kwani
ni wazi jela siyo sehemu nzuri ya kwenda kuishi ila kwasababu nchi yetu
inaongozwa kwa utawala wa sheria basi yule yoyote anayetiwa hatiani kwa makosa
mbalimbali mahakama inaweza kumpatia adhabu ya kwenda jela ambapo unapokuwa
gerezani ni wazi uhuru wako unakuwa umezuiwa.
Kwanza kimsingi napenda mkubaliane na
hesabu zangu kuwa kesi hiyo ya jinai Na.125/2013
ilidumu mahakamani hapo kwa siku 32 tu tangu ilipofunguliwa rasmi
Februali 18 na kutolewa hukumu Machi 21 mwaka huu.
Kwa hiyo binafsi umalizikaji wa kesi
hiyo haraka kiasi hicho binafsi umenifundisha mambo kadhaa ya msingi kuwa, kumbe
mahakama, ofisi ya DPP na jeshi la polisi vikiamua kufanyakazi yao kikamilifu
vinaweza sana, ila wakati mwingine uwa vyombo hivi ni kama vinaamuaga kujitoaga
fahamu kwa kushindwa kutoa vipaumbele katika kesi za mbalimbali ili nazo
zisikilizwe mfululizo kama hii ili watuhumiwa wajue hatia yao hali
inayosababisha msongamano magerezani.
Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka
jana hadi Mwanzoni mwa mwaka huu, Tanzania iliingia katika historia chafu ya
baadhi ya wananchi wake kujihusiasha na malumbano ya na vurugu za kidini hali
iliyosababisha hata makanisa kuchomwa mto,na viongozi wa dini kuuwawa na
kujeruhiwa lakini serikali iliweza kuwakamata wahusika na kuwafikisha mahakamani
watuhumiwa na moja ya kesi inayooendana na madai ya udini ni hii
ambapo imetolewa hukumu.
Najua makala hii itawakera baadhi ya
watu ila napenda ieleweke wazi kuwa hukumu ya kesi hii ni funzo kwa wale wote
wanaofikiri Tanzania ni chini ya kiuni na ambayo haiongozwi kwa utawala wa
sheria,pia ni funzo kwa wale wote wanaofikiri dini ya kiislamu au kikristo ndiyo
zinazoliongoza dola la Tanzania.
Lakini pia hukumu hii ni funzo kwa
wale wote wanaoleta chokochoko za kidini pia kwa wale wafuasi wa vyama wa baadhi
ya vyama vya upinzania hapa nchini ambao wamejiwekea kasumba ya kufanya
maandamano haramu kwa kisingizio kuwa mahakama haiwezi kuwafunga jela
washitakiwa wanaokabiliwa na kesi za maandamano haramu kwani magereza yamezidiwa
na idadi kubwa ya watu na kwamba serikali haina uwezo wa kuwatunza wafungwa
wengine wa kesi za maandamano haramu.
Nalisema hili kwasababu kuna wafuasi
wa chama kimoja cha upinzani huko mitaani wamekuwa wakijifariji
kuwa mahakama haiwezi kuwafunga jela washitakiwa wengi wanaokabiliwa kwa makosa
ya maandamano na mkusanyiko haramu.
Leo hii wenzetu hao 53 waliofungwa
jela, wale waliowatuma watenda makosa hayo wala hatukuwaona kuja mahakamani
kuwasaidia zaidi ya ndugu na wake wa washitakiwa ndio kila siku walikuwa
wakifika mahakamani kufuatilia kesi .
Watu hao 53 wanafamilia
zao,wameziacha familia yao kwa mambo ya kijinga tu ya kukaidi sheria za nchi,
leo hii nani atazihudumia familia zenu wakati nyie mpo gerezani?
Hukumu hii iwafumbue macho wafuasi wa
vyama vya siasa ambao ni wao na familia zao ni malofa wa kutupa kama mimi
wasikubali kushiriki maandamano haramu yanayoandaliwa na vyama vyao, kwani siku
zote viongozi wa kubwa wa vyama visiasa ni kama mashetani ambao wamekuwa
wakipenda kuwaamasisha watoto wawenzao washiriki kwenye vurugu ,maandamano
haramu mwisho wa siku mtajikuta mnaangukia kwenye mikoni ya dola.Na muwajibu
viongozi hao waende kuwachukua watoto wao wa kuwazaa na wake zao ndiyo washiriki
maandamano hayo haramu ili wakutane na mkono wa dola.
Maana imekuwa ni desturi kwa
wanasiasa hasa wa upinzani kuwakataza watoto na wake zao kushiriki kwenye
maandamano haramu ila siku wanasiasa hao wakienda kuapishwa,au kwenye vikao vya
bunge ndiyo uwachukua wake na watoto zao kwenda kustarehe ila kwenye maandamano
haramu ambapo kule kuna virungu vya polisi na mabomu ya machozi hawazipeleki
familia zao.
Ikumbukwe kuwa Watanzania wengine
tunajifanya tunapenda wakati tukiwa na afya njema, tuna madaraka au uwezo
fulani,hatuna matatizo na hatujafunguliwa kesi mahakamani ila ukiishaondoka
madarakani, mali na fedha hauna,una ugua na umefunguliwa kesi mahakamani wale
wote waliokuwa wanajifanya wapo karibu yao wanakukimbia na kuanza kukusema
vibaya.Mifano ya haya ninayasema ninayo kwani nimeishuhudia na imenifundisha
sana tu.
Mwisho, kasi hii ya kutisha ya
kuimaliza kesi hii pia ipelekwe kwenye kesi za maandamano na mkusanyiko haramu
zilizofunguliwa katika Mahakama za Arusha,Dar es Salaam na kwingineko ambazo
zinawakabili viongozi wa siasa na wafuasi wao ili nazo kesi hizo ziweze
kumalizika kwa haraka na hatimaye watuhumiwa wapatiwe haki yao na mahakama.
Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com ; Aprili 3 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment