Header Ads

DOWANS YAWAWEKEA PINGAMIZI WANAOIPINGA MAHAKAMA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Kampuni ya Dowans Holding SA na Dowans Tanzania Ltd,imeiwekea pingamizi Shirika Umeme (TANESCO),Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) na Mwandishi wa Habari Mwandamizi, Timoth Kahoho katika kesi yake ya kuomba tuzo waliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC) isajiliwe na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo ambayo jana ilikuja mbele ya Jaji Emilian Mushi katika Mahakama Kuu kwaajili ya kutajwa, wakili wa mlalamikaji(Dowans), Keneddy Fungamtama aliiambia mahakama tayari ameishawasilisha mapingamizi matatu kwa pande tatu katika kesi ambazo ni Tanesco anayetetewa na , LHRC na Kahoho ambaye anajiwakilisha binafsi

Kesi hiyo ilifunguliwa mapema mwaka huu na mshinda tuzo hiyo ambayo ni Kampuni ya Dowans ambayo inatetewa na wakili Kennedy Fungamtama dhidi ya TANESCO ambayo nayo inatetewa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju , Jamhuri Johnson, Dk.Angelo Mapunda na Florence Luoga. Na wapinga maombi ya Dowans ambao hawaja orodheshwa kwenye kesi hiyo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) kinachotetewa na Dk.Sengondo Mvungi, Harold Sungusia na Francis Kiwanga na Mwanahabari mkongwe ambaye hana wakili.

Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Emilian Mushi wakati kesi hiyo ya madai namba 8 ya mwaka huu,ilipokuja kwa mara ya kwanza kwaajili ya kutajwa alisema amefika uamuzi wa kutoa amri hiyo baada ya wapinga maombi (LHRC na Timoth Kahoho) kueleza kuwa hawakuwa wamepatiwa nakala tuzo hiyo na wao hawajawaipatia Dowans na Tanesco nakala za mapingamizi yao.

Jaji Mushi pia alikubaliana na maombi ya mawakili wa pande zote yaliyotaka pande zote katika kesi hiyo(Dowans na Tanesco) kuacha kufanya jambo lolote linalohusiana na maslahi ya pande hizo mbili hadi pale kesi hiyo itakapomalizika.

“Ila kama mlivyoomba nyie mawakili wa pande zote mbili kwamba endapo serikali kupitia Tanesco wakitaka kulimaliza jambo hili nje ya mahakama,mahakama hii inaziamuru pande hizo kabla ya kufikia uamuzi huo wa kumalizana nje ya mahakama au kuwasha mitambo,walete kwanza ombi mahakamani la kuomba kufanya hivyo;

“Na sioni haja ya kutoa amri ya kuwazuia wale wote wanaopiga kelele za Dowans,Dowans huko mitaani na kwenye vyombo vya habari kwasababu sheria na utaratibu unaeleweka wazi kwamba kesi ikiwepo mahakamani ni marufuku kwa mtu au vyombo vya habari kuizungumzia …lakini minanasema waache watu waendelee kupiga kelele zao huko mitaani kuhusu tuzo ya Dowans kwani napenda wajue kwamba mahakama hii aiyumbishwi na hizo kelele zao kwani siku zote inafanyakazi zake kwa kuzingatia sheria”alisema Jaji Mushi.

“Kwa sababu upungufu huo umejitokeza natoa siku 21 kwa pande mbili katika kesi hii na nyie wapingaji wawili , wenyewe kwa wenyewe muakikishe mnapeana nyaraka mlizonazo na ninaiarisha kesi hii hadi Machi 30 mwaka huu, ambapo kesi hii itakuja kwaajili ya kutajwa na kuangalia kama tayari mmeishapeana nyaraka hizo”alisema Jaji Mushi.

Awali wakili wa Tanesco, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Masaju aliomba mahakama impatie siku 21 kujibu hoja za kutaka tuzo ya Dowans isisajiliwe.Naye wakili wa Dowans, Fungamtama pia aliomba mahakama impatie siku 21 kujibu pingamizi hilo litakalowasilishwa na Tanesco.

Kwa upande wakili wa (LHRC), Dk.Mvungi aliomba apatiwe siku saba kujibu hoja kama kutakuwa na chakujibu.Na Kahoho yeye ambaye hana wakili akaeleza kuwa kama maombi yake ya kupinga Dowans isisajiliwe yatawekewa pingamizi anaomba apewe siku 14 kujibu na kuongeza kwa kuiomba mahakama itoe amri ya kuzuia watu au vyombo vya habari kuchapisha habari ambazo zinaingilia mwenendo wa kesi hiyo.

Kesi hiyo ambayo inafuatiliwa kwa karibu na umma wa Tanzania iliendeshwa chemba hali iliyobabisha mawakili na waandishi baadhi waliofika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo ambayo jana kwa mara ya kwanza ndiyo ilitajwa kushindwa kuingia ndani ya chumba hicho na kuishia kukaa kwenye kordo za mahakama hiyo na ambapo waliushauri uongozi wa mahakama hiyo utambue kuwa kesi hiyo inagusa maslahi na hisia za watanzania wengi hivyo ni vyema siku nyingine jaji Mushi aendekusikiliza kesi hiyo kwenye mahakama ya wazi.
Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake lakutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC na siku chache baadaye Tanesco, LHCR,Kahoho wakawasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe.

Mahakama ya ICC, ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco, Novemba 15 mwaka jana, ambapo mahakama ilitia hatiani Tanesco kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaimuru iilipe fidia ya shilingi bilioni 94.Hukumu ambayo imezua mjadala mkali hapa nchini kuanzia kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa,na makundi mengine ambapo wengine wanataka Dowans ilipwe huku wengine wakitaka kampuni hiyo isilipwe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 31 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.