Header Ads

KESI YA MBATIA Vs MDEE:MBATIA ONGEZA MSHTAKIWA MWINGINE

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali ombi la aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Kawe kwa tiketi ya (NCCR-Mageuzi) James Mbatia lilokuwa likitaka mahakama hiyo imruhusu kuondoa mahakamani hati yake ya madai ili aende kuifanyia marekebisho na kisha kuirejesha upya mahakamani hapo.

Mbatia katika kesi hii ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya jimbo la Kawe,ambayo imepewa Na.111/2010.Mbatia anamlalamikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa jimbo hilo Halima Mdee (CHADEMA) ambaye hata hiyo Mdee hakuwepo mahakamani jana ila Mbatia alikuwepo.

Amri hiyo ya kukubali ombi la Mbatia ilitolewa jana na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,Amir Msumi ambapo alisema anakubaliana na ombi kuibadilisha hati ya madai lilowasilishwa na mawakili wa Mbatia, Mohamed Tibanyendera na Alocye Komba na akawataka wawasilishe hati mpya Machi 8 na kesi hiyo itakuja kutajwa Machi 10 mwaka huu.

Awali mapema jana asubuhi wakili Tibanyendera na Komba waliambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutajwa ila mlalamikaji (Mbatia) anawasilisha ombi la kuomba kuiondoa hati ya madai ili aende kuifanyia marekebisho kwani kwa mujibu mabadiliko ya Kanuni za kesi uchaguzi yaliyofanyika mwaka 2010,yanalazimisha Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo husika naye afunguliwe kesi jambo ambao katika hati yao ya madai hawakuwa wamemshtaki.

Tibanyendera alieleza kuwa kwa mujibu wa kanuni za zamani za sheria ya uchaguzi ya mwaka 2002 kabla hazijafanyiwa mabadiliko mwaka jana mlalamikaji alikuwa akiruhusiwa kumshtaki mbunge aliyeshinda katika jimbo husika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mbapo huyo mwanasheria mkuu wa serikali ndiyo aliyekuwa akishtakiwa kwaniaba ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.

“Kwa maelezo hayo ya kisheria mteja wetu(Mbatia) anaomba abadilishe hati yake ya madai ya awali ili aweze kumuongeza Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kawe kwahiyo katika hati hiyo mpya tutakayoiwasilisha Jumatatu ijayo wadaiwa watakuwa ni watatu na si wawili tena;

“Na sababu ya pili ya mteja wetu kuiondoa hati hiyo akaifanyie marekebisho ni kuna wapiga kura wawili wa jimbo hilo wamejitokeza na wametaka kuungana na Mbatia katika kesi hiyo kuwashtakiwa wadaiwa hao.Na wapiga kura hao ni Hemed Manoni na Solomoni Mfunda na hivyo wataifanya hati mpya kuwa na walalamika watatu ambao ni Mbatia,Manoni na Mafundi dhidi ya AG,Mdee na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kawe”alidai Wakili Tibanyendera.

Novemba 25 mwaka 2010 Mbatia alifungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza Halima Mdee(CHADEMA) kuwa ndiye aliyeshinda na ataliongoza jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 5 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.