Header Ads

KWA HILI,JESHI LA POLISI LINASTAHILI SIFA

Na Happiness Katabazi

SALAAM! Wasomaji na wapenzi wote wa safu yangu ya FUKUTO LA JAMII ambayo awali ilikuwa ikitoka kila siku ya Jumapili katika gazeti hili ila kwasababu zisizoweza kudhuhirika na zilizokuwa nje ya uwezo wangu,nimelazimika kuamishia safu hii kwenye gazeti letu litokalo kila kila siku ya jumanne hivyo.


Februali 23 mwaka huu, Serikali ilifikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, watu wanne wakiwemo raia wawili wa Pakstan wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama na kusafirisha kilo 179 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.2. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Biswalo Mganga, mbele ya Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Freddy Chonde na Kambi Zubery ambao ni Watanzania na Abdul Ghan Peer Bux na Shahbaz Malik ambao ni raia wa Pakstan, Februari 21, mwaka huu, maeneo ya Mtaa wa Jogoo, Mbezi Beach kwa pamoja washitak
iwa wote waliingiza nchini dawa za kulevya zenye uzito na thamani hiyo ya fedha.

Machi 7 mwaka huu, Jamhuri ilifikisha raia wengine wa nne wa kigeni katika mahakama hiyo wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama na kuingiza dawa za kulevya zenye uzito wa aina gramu 81 zenye thamani ya Sh bilioni 2.8.

Mustapher Siyani wakili mwandamizi wa serikali Biswalo Mganga aliyekuwa akisaidiwa Prosper Mwangamila na Theophili Mtakyawa aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Dinnis Chukwudi Okechukwu,Paul Ikechukwu Obi ambao ni raia wa Naigeria, Stani Hycenth raia wa Afrika ya Kusini na Shoaib Mohammed Ayazi ambaye ni raia wa Pakstani.

Machi 9 mwaka huu, tena Jamhuri ilimfikisha kwa hakimu huyo , raia mwingine wa Nigeria , Luvinus Ajina Chime akikabiliwa na kosa la kuingia dawa za kulevya hapa nchini aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 810 na zina thamani ya Sh milioni 28.3.Mahakimu wote wanaosikiliza kesi hizo kwa nyakati tofauti waliwaeleza washtakiwa hawapaswi kujibu chochote kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.

Kesi hizo tatu za dawa za kulevya ni miongoni mwa kesi kadhaa zilizokwishafunguliwa katika mahakama mbalimbali hapa nchini.

Hakuna ubishi kwamba uzito wa dawa huo ni mkubwa na kama watuhumiwa wangefanikiwa kuziingiza dawa hizo sokoni hapa nchini bila kukamatwa na askari wa Jeshi la Polisi wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya kinachoongozwa na Kamanda mzalendo, Godfrey Nzowa ni wazi washtakiwa hao wangepata fedha nyingi na baadhi ya vijana wetu wangezidi kualibiwa na dawa hizo.

Na hapa naomba ieleweke kwamba mada ya leo haitaingilia mwenendo wa kesi hizo tatu kwani mwandishi wa habari hizi si maamuma kihivyo wa sheria kwani ana fahamu vyema kesi ikishafikishwa mahakamani hakuna mtu yoyote anayepaswa kuizungumzia na kwamba mtuhumiwa atabaki kuwa mtuhumiwa hadi pale mahakama ikapotoa hukumu dhidi yake.

Hivyo kilichonisukuma kuandika mada hii ni kutaka kukipongeza Kitengo hicho kinachoongozwa na Kamanda Nzowa pamoja na askari wa kitengo hicho nchi nzima, kwani hivi sasa tunashuhudia kasi ya watu wanaotuhumiwa kuingiza dawa za kulevya nchini wakikamatwa na kufikishwa mahakamani ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Licha watu hao ambao ukamatwa na askari wa kikosi hicho hawana majina makubwa wala wafanyabishara wakubwa nchini,kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na wengi kwamba baadhi ya matajiri na wafanyabiashra wa kubwa ndiyo wanaongoza kuuza dawa hizo lakini sisi tusiopenda ‘longolongo’ , tunaziamini taarifa zinazotolewa na Kitengo hicho ambazo utolewa muda mchache baada ya kuwakamata watuhumiwa hao na dawa na si uvumi unaozagaa mitaani.

Pili, natoa pongezi kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)-Elizer Feleshi kwa kufanyakazi kama timu na kitengo hicho cha polisi kwa kuwafungulia mashtaka washtakiwa wanaokabiliwa na kesi za aina hiyo.Kwa kuwa sote tunafahamu kuwa hivi sasa polisi kazi yake ni kuchunguza na kukamata na ofisi ya DDP ni kuwafungulia mashtaka washtakiwa, tofauti na zamani kwani polisi ndiyo waliokuwa wanapeleleza,wanakamata na wanaendesha kesi mahakamani .

Ni kweli hayo ni majukumu yanapaswa kufanywa na kitengo hicho na ofisi ya DDP.Lakini safu hii inasema kwamba licha hayo ni miongoni mwa majukumu yao inapenda kuwapongeza kwani kama askari wa kitengo hicho kinachoongozwa na Kamanda Nzowa wangekuwa ni wachumia tumbo na wanatamaa ni wazi wangechukua rushwa kwa washtakiwa na wangewaruhusu washtakiwa hao kuondoka na dawa hizo na mwisho wa siku huyo Nzowa,Feleshi na sisi wananchi tusingejua kilichokuwa kikiendelea.

Dawa za kulevya ni miongoni mwa jinamizi kubwa linaloangamiza taratibu kizazi na nguvu kazi ya taifa hili.Kwakuwa sote ni mashahidi tunapopita mitaa ya Kinondoni, Buguruni, Manzese-Shidele, Mananyamala, Shekilango, Temeke,Ubungo Standi na huko mikoani utawakuta vijana wetu ambao ni watumiaji wa dawa hizo haramu wakiwa wamelewa hata asubuhi hawajitambui, sura zao zimegeuka kuwa kama mababu wanaoishi Mwituni.Inasikitisha sana na kukera pia.
Lakini taifa wakati nguvu kazi yake hiyo ikizidi kuangamia kwa dawa hizo, watu wazima ambao ndiyo wafanyabiashara wa dawa hizo ndiyo vipato vyao vinazidi kukukua kutokana na vijana hao kununua dawa hizo kwa wingi.Inasikitisha sana.

Ndiyo maana nilivyoona kasi ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya na kuburuzwa mahakamani inaongezeka,nikalazimika kuandika makala ya kupongeza kitengo hicho na ofisi ya DPP .Naamini kasi ya ukamataji ikiongezeka naye DPP akaaongeza kasi ya kuwafungulia kesi na sisi wanahabari wa habari za mahakama nchini tukaongeza nguvu ya kuripoti kesi hizo, ni wazi watuhumiwa wengine wanaofanyabiashara hiyo wataogopa kama sikuiacha kabisa.

Ikumbukwe kwamba wahalifu nao kila kukicha wana buni mbinu mbadala za kukabiliana na mkono wa dola wakati wa kuingiza na dawa hizo nchini.Na biashara hiyo haramu wameigeuza kuwa ndiyo ajira yao rasmi ambayo inawaingizia kipato cha kuishi na kuwaliopia ada watoto.Hivyo ni vyema serikali sasa iamke na ikatae nchi yake kugeuzwa shamba la bibi na baadhi ya wageni ambao wakuwa wakiingiza dawa za kulevya ambazo zinakuja kuteketeza kizazi cha taifa hili.Kwa kukiongezea fedha , mafunzo kwa askari wa kikosi cha kuzuia dawa za kulevya.
Kwakuwa inauma kuwaona vijana wadogo wakikatisha masomo yao kwaajili ya kuharibiwa na dawa hizo.Siku zote minaamini taifa ambalo wananchi wake hawana elimu ni wazi taifa hilo litakuwa ni taifa tegemezi.

Baada ya kuyasema hayo napenda kutoa angalizo kwa Kitengo hicho kwamba wasiishie kuwakamata waingizaji wa dawa za kulevya tu , bali pia wawageukie wauzaji wadogo ‘wazungu wa unga,mapusha’ , hao uishi mitaani kwetu na hao ‘mateja’ uenda kwa hao kununua kete hizo za dawa na kisha kubwia au kujidunga.Na kama hamjui wanapatikana mitaa gani ni vyema mkaunda urafiki na mateja waliozagaa kwenye vituo vya basi watawaonyesha ni wakinanani wanawauziaga dawa hizo.Tunachokishuhudia sasa mmeelekeza nguvu nyingi katika kuwakamata wanaoingiza dawa hizo nchini.

Kingine ambacho ningependa kifanywe na kitengo hicho nikuwakamata mateja wote wanaorandaranda mitaani hasa kwenye vituo vya mabasi na baadhi ya wanamuziki hawa muwapeleke hospitali wakachukuliwe vipimo ili kuona kama kweli ulevi wao una tokana na matumuzi ya dawa hizo za kulevya na kama hakuna sheria ya kuwashughulikia walaji wa dawa hizo basi sote tuone haja ya bunge letu kutunga sheria ya kuwabana walaji wa dawa hizo maarufu kama kwa majina ya ‘mateja,wala unga’.

Kama ripoti za madaktari zitathibitsha ulevi wao unatokana na dawa za kulevya, hivi hatuoni haja sasa ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya ya mwaka 2002; inaongezewa makali ya kuwabana vilivyo hata walaji dawa hizo kwa siri lakini adharani wanaonekana wamelewa?Kwani hivi sasa tunachokishuhudia wanaokamatwa ni waingizaji na wasafirishaji, walaji wa dawa hizo hawakamatwi na wengine wanafahamika kabisa kwamba ni walaji wazuri wa dawa hizo.

Nasema hivyo kwasababu wala unga kwa kificho halafu wanalewa adharani hatuwaoni, ulevi wao huo mwisho wa siku vijana ambao ni wepesi kurubunika wanatajikuta wanarubunika kwa kutamani kutumia ulevi huo?.

Angalizo jingine nalitoa kwa mawakili wetu wa serikali mtakapowea jukumu la kuendesha kesi hizi za dawa za kulevya, nanyi tunaomba mziendeshe kesi hizi kwa kutanguliza haki na siyo tamaa za kupenda kuhongwa fedha na ndugu wa washtakiwa ili muweze kuzivuruga hizo kesi mwisho wa siku washtakiwa waokoke kwenye mkono wa dola.

Kwani tayari kuna malalamiko ya chini chini toka kwa baadhi ya askari polisi kwamba wao wamekuwa wakijitahidi kufanyakazi yao ya upelelezi vizuri tu lakini baadhi ya mawakili wa serikali wenye hulka za kifisadi wamekuwa wakiziaribu kesi hiyo kwaajili kupokea rushwa.Narudia tena sitaki kuingilia kazi ya mahakama lakini napenda kuona haki inatendeka na kila mmoja wetu anatimiza majukumu yake ipasavyo katika kuakikisha taifa hili linapambana na biashara hii haramu ya dawa za kulevya.

Hapa Dar es Salaam, sasa hivi imeanza kuwa sifa moja wapo ajira ya kupiga debe lazima uwe ‘teja’ na yote hayo tunayaona hakuna mamlaka inayochukua hatua.Kama ilivyoongezwa makali makosa ya utakatishaji fedha haramu ndivyo tunavyotaka sheria ya kuzuia dawa za kulevya iongezewe makali.Kwani adhabu nyepesi kama kifungo au faini za wanazopewa watuhumiwa wa kesi hizo pindi wanapitiwa na mahakama ndiko kunako wapa jeuri ya kutoogopa ya kuendelea kufanya biashara hiyo haramu ambayo inatuharibia nguvu kazi ya taifa.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 15 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.