Header Ads

KORTI YAKUBALI OMBI LA MPENDAZOE,LISSU KIDEDEA

Na Hapiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali ombi la aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Segerea(Chadema), Fred Mpendazoe la kutaka mahakama hiyo imruhusu aweke sh milioni 15 mahakamani kama dhamana.

Dhamana hiyo ni sh milioni tano kwa kila mdaiwa ambapo wadaiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Dk. Makongoro Mahanga (CCM), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi anazotakiwa kuzitoa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

Katika kesi ya msingi Mpendazoe anapinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 jimbo la Segerea yaliyomtangaza Dk. Mahanga kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Uamuzi huo ulitolewa jana asubuhi na Jaji Profesa Ibrahimu Juma ambapo alisema anakubaliana na ombi lilowasilishwa na wakili wa Mpendazoe, Peter Kibatala liloiomba mahakama hiyo iwaruhusu kuweka kiasi hicho cha fedha kwa sabababu ombi hilo limekidhi matakwa ya kifungu cha 111(2) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

Kwani kifungu hicho ndicho kinachomruusu mlalamikaji wa kesi za uchaguzi kuwasilisha fedha mahakamani na kwamba mlalamikaji katika ombi hilo hakutaka apunguziwe kiasi cha kulipa bali alikuwa anaomba ridhaa ya kulipa kiasi chote cha fedha anachotakiwa alipe kwa mujibu wa sheria.

“Kwa maana hiyo mahakama hii inakubaliana na ombi la mlalamikaji(Mpendazoe) na linalitupilia mbali pingamizi la mdaiwa(Dk.Mahanga) na wenzake kwasababu kifungu cha sheria walichokitumia kuwasilisha pingamizi hilo si sahihi na hakiendani na ombi la mlalamikaji…na kwa maana hiyo mahakama hii imemruhusu mlalamikaji kuwasilisha kiasi hicho cha fedha ndiyo kesi ipangwe tarehe ya kuanza kusikilizwa”alisema Jaji Profesa Juma.

Februali 28 mwaka huu, wakili wa Mpendazoe, Peter Kibatala aliwasilisha ombi jipya la kuomba mteja wake aruhusiwe kuweka kiasi hicho cha fedha kwani tayari mteja amepata kiasi hicho cha fedha.Hata hivyo wakili wa wadaiwa hao Jerome Msemwa alilipinga ombi hilo na kuiomba Mahakama isimruhusu hadi pale mlalamikaji atakapopeleka ombi rasmi mahakamani la kuiomba impangie kiwango cha kuweka mahakamani hapo.

Wakili Msemwa aliongeza kuwa kifungu cha 111(3) cha Sheria ya Uchaguzi, kinamtaka mwombaji anayeiomba mahakama imsamehe kulipa dhamana hiyo au kumpunguzia kiwango cha kulipa, anatakiwa awasilishe ombi hilo ndani ya siku 14 tangu alipofungua kesi ya msingi ya kupinga matokeo ya Ubunge.

Akipangua hoja hiyo wakili wa Mpendazoe, Kibatala aliambia kuwa kifungu hicho kilichotumiwa na Msemwa hakiendani na ombi lao waliloliwasilisha kwa kuwa ombi lao ni Mahakama imruhusu mlalamikaji aweke kiasi hicho cha fedha na si vinginevyo.Februali 15 mwaka huu, Jaji Juma alitupilia mbali ombi la Mpendazoe la kuitaka Mahakama hiyo imsamehe kulipa fedha hizo kwa sababu hana uwezo wa kupata fedha hizo na kwamba amebaini hati ya kiapo cha maombi hayo kina dosari za kisheria.

Katika katua nyingine; Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imetupilia mbali maombi ya kuondoa ama kusamehewa dhamana za gharama za uendeshaji kesi za uchaguzi, yaliyofunguliwa na wanachama wawili wa CCM dhidi ya mbunge wa Singida Mashariki, Tindu Lissu (Chadema).
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Silivangira Mwangesi na kuongeza kuwa Lissu ameshinda kesi hiyo kutokana na kutofuatwa kwa utaratibu wakati wa kufungua kesi hiyo.

Hata hivyo, hukumu hiyo ilitolewa wakati Lissu hakuwepo mahakamani. Mlalamikiwa huyo aliwakilishwa na ndugu yake aliyejitambulisha kwa jina la Samson Mkotya ambaye alidai alifanya hivyo kwa kuwa Lissu aliharibikiwa na gari mkoani Morogoro.

Maombi hayo yaliwasilishwa na wanachama wawili wa CCM, Shaban Itambu na Pascal Hallu ambao wamewafungulia kesi ya kupinga matokeo ya ubunge jimbo la Singida Mashariki, Tindu Lissu, Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria wa Serikali.

Hata hivyo, Lissu alipinga maombi hayo kwa sababu waombaji hawakuwasilisha maombi ya kutaka kupangiwa dhamana ya gharama za uendeshaji kesi za uchaguzi.

Lissu aliwasilisha hukumu za kesi tatu ambazo mahakama kuu iliwahi kuzitupa baada ya walalamikaji kutowasilisha kwanza maombi ya kupangiwa dhamana hiyo.

Hukumu zilizowasiliswa na Lissu ni ya John Mnyika na Charles Keenja, Joyce Chitende na Zainabu Gama, John Jomba Koyo na Christopher Ole Sendeka. Akipinga pingamizi hilo, wakili wa walalamikiwa hao ni Abdallah Possi, alisema si lazima Jaji akubaliane na hukumu hizo ambazo zimetolewa na majaji wenzake wa mahakama hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 9 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.