Header Ads

JERRY MURRO ANA KESI YA KUJIBU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemuona aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC1, Jerry Murro na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kula njama, kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10, kuwa wana kesi ya kujibu.


Uamuzi huo wa kushtua ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe ikiwa ni muda mfupi baada ya shahidi wa sita wa upande wa Jamhuri, D/C Koplo Lugano Mwampeta kumaliza kutoa ushahidi wake na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface kueleza kuwa wamefunga ushahidi.

Baada ya Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Boniface kueleza hayo, Hakimu Mirumbe alisema anaahirisha kesi hiyo kwa dakika kumi, ili aweze kupitia jalada la kesi hiyo na ushahidi wote uliokwishatolewa na mashahidi sita wa upande wa jamhuri kisha atarudi kutoa uamuzi wa ama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Ilipofika saa 6:47 mchana Hakimu Mirumbe aliingia kwenye chumba cha mahakama hiyo na kutoa uamuzi wake ambapo alisema baada ya kulipitia jalada la kesi hiyo mahakama imeona upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake na hivyo mahakama hiyo imewaona washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.

“Baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri katika kesi hii mahakama imewaona washtakiwa wote mna kesi ya kujibu na ninaaharisha kesi hadi Machi 29 ambapo washtakiwa mtaanza kukjitetea,” alisema Hakimu Mirumbe.

Awali, shahidi wa sita, D/C Koplo Lugano Mwampeta akiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Boniface, kutoa ushahidi wake, alidai Januari 31, 2010 alikuwa ofisini katika ofisi za Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ambapo mkuu wake wa kazi ambaye ndiye mkuu wa upelelezi wa mkoa huo(RCO)-Duwani Nyanda alimpatia kazi.

Mwampeta alieleza kuwa RCO-Nyanda alimpatia kazi ya kumsaidia kulikagua gari la Murro ambapo kiongozi wake huyo ndiye aliyekuwa mkaguzi mkuu, ambapo katika ukaguzi kwenye gari hilo walipata miwani na pingu na wakati wakifanya upekuzi huo Murro alikuwa akishuhudia.

Mbali na Murro, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Edmund Kapama na Deogratius Mugasa ambao wanadaiwa Februari 15 mwaka jana walikula njama kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage. Kati ya mashtaka matatu yaliyofunguliwa dhidi yao, Murro anakabiliwa na mashtaka mawili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 9 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.