TANZANIA IJITAZAME UPYA
Na Happiness Katabazi
Salaam! wasomaji wote wa safu hii.Leo nitaanza makala yangu kwa nukuu ya Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere. Nukuu hiyo inapatikana katika hotuba zake maarufu, katika kitabu cha ‘Moyo kabla ya silaha’, aliyoitoa mwanzoni mwa miaka ya 1960. Na nitaichambua nukuu hiyo.
Jifunze wakati ni huu: “Afadhali tuwe na taifa ambalo halina silaha za kisasa, lakini tuna moyo wa ushujaa, kuliko kuwa na taifa lenye silaha, lakini vijana wake ni waoga. Tuwe taifa la binadamu, tujue wapi tunatoka na wapi tunakwenda.
“Kuwa na moyo safi ni jambo jema sana kwani tukiwa na moyo safi silaha zitafuata baadaye. Afadhali kuwa maskini, lakini tunajitegemea, kuliko kuwa matajiri kwa kuomba na kutegemea taifa jingine. “Tujiamini kwa nguvu zetu zote na tunajitegemea. Taifa linaloshiba makombo siyo taifa.
“Tuwe na tabia ya ushujaa, tusiwe waoga. Tuwe na tabia ya kujitegemea na kusaidiana. Ni afadhali kuwa na chakula kidogo, lakini tukagawana kidogo kidogo kuliko kuwa na chakula kingi na tukaanza kukigombea. Tanzania iwe na tabia mpya. Inawezekana, timiza wajibu wako.”
Aya ya kwanza ya nukuu hiyo Mwalimu Nyerere, alikuwa anaona kwamba vijana wengi walikuwa wanadai wapewe silaha, watakomboa taifa na kukomboa Bara la Afrika kutokana na ukoloni na ubeberu wa watu weupe. Wakati huo vita ya kupigania uhuru ilikuwa inarindima katika nchi za Msumbiji , Angola , Zimbambwe na kwingineko.
Nchi hizo zilikuwa chini ya ukoloni na ubeberu na Tanzania ilikuwa makao makuu ya kamati ya ukombozi ya Afrika ya Umoja wa Nchi Uhuru za Afrika. Na wakati huo ndege za Wareno zilikuwa zikivuka mpaka na kudondosha mabomu nchini mwetu.
Mwalimu Nyerere aliona upungufu katika mtazamo wa vijana wale ambao waliona silaha ndiyo njia sahihi ya kukomboa ukoloni na ubeberu.
Yeye aliona ni tofauti, kwani alichokuwa anakihitaji yeye ni ‘commitment’, uwe unaliamini hilo jambo kwa moyo wako wote na akili zako zote na ujitoe mhanga kulitetea Bara la Afrika. Hiyo ndiyo nadharia ya upambanaji na huo ndio msingi wa upambanaji wa kweli.
Mwalimu alizungumzia katika mazingira hayo. Je, leo hii kauli hiyo inatugusa vipi Watanzania, umma ambao idadi kubwa ya ni sisi vijana? Na je, tuna amini kwa moyo wote kuhusu vita dhidi ya ubeberu? Ukweli ni kwamba hatuamini.
Walio wengi hawaamini kama kuna ubeberu, wanaamini kwamba kuna utandawazi kwa maana kwamba mtaji wa kibeberu unaweza ukatumika kulikomboa taifa na kufuta umaskini.
Kwa Watanzania wengi wa leo wanatofautiana sana na Mwalimu Nyerere, hawana moyo wala ushupavu wa kupambana na udhalimu wa kila aina. Na kwa hakika kwa kiasi fulani tunashawishika kuamini sera nzima ya uwekezaji ni tamko la kukumbatia ubeberu.
Kwa msingi huo vijana hatuna budi kupambana na hata kuhitaji kuwa na moyo wa ushujaa. Tumeishakubali kwamba wageni wana haki kubwa hata kuliko wananchi kuwekeza na kuvuna rasilimali zetu.
Wajibu wetu na nafasi tuliyonayo tujiendeleze kielimu na kuomba ajira. Na katika hilo hakuna cha ushupavu wala cha woga, cha msingi ni kumpigia magoti na kumlamba miguu tajiri ili upate mradi wako.
Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba ili tuwe na taifa la binadamu linalostahili heshima lazima tujue wapi tunatoka na wapi tunakwenda: Kwa hilo Watanzania wa leo hatumo kwa sababu hatuna sera thabiti.
Tunachokiabudu leo hii ni kupewa misaada na wafadhili ambao sasa ndio wanatupangia mipango yetu na uchumi wa maendeleo. Miongoni mwa kazi kubwa ya baadhi ya watendaji wa serikali ni kuandika michanganuo (proposals) ili kupewa fedha, na kweli kazi hiyo inafanikiwa kwa kuandaa makongamano mbalimbali na kisha inafuatiwa na kazi kubwa ya kuandika ripoti na kuwapelekea wale mabwana zetu waliotoa fedha zao kwa nchi yetu.
Mwalimu Nyerere alisema, afadhali kuwa maskini, lakini tunajitegemea kuliko kuwa matajiri kwa kuomba kutegemea taifa jingine; kwa maana hiyo taifa linalostahili heshima ni lile linalojiamini, linalotegemea nguvu zake kwa maendeleo yake badala ya taifa linaloshiba ‘makombo,lawalawa’ linayopewa kwa jina la misaada.
Hebu tujiulize, Tanzania tunajitegemea kwa kitu gani? Vijana wetu hawajui tena kilimo wala hawapendi ufugaji, kwa hiyo chakula kilichopo sokoni na kwenye ‘supermarket’ kinaagizwa kutoka nje ya nchi.Na hatupendi kwa sababu hakuna mazingira mazuri yatayotushawishi kujikita kwenye sekta hiyo ya kilimo.
Serikali ya Tanzania haina tena viwanda vya nguo, japo inazalisha zao la pamba. Tanzania haisindiki kahawa wala matunda japo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao hayo. Tanzania haizalishi mafuta ya kula, inanunua mafuta hayo kutoka kwenye viwanda vya watu binafsi au nje ya nchi ambazo nyingine ni jangwa japo Tanzania inazalisha zao la alizeti, karanga na mbegu nyingine za mafuta ya kula.
Viwanda vyetu tumevibinafsisha tena kwa wingi, vingine vinafungwa na vilivyopo ni vya jua kali vinavyozalisha bidhaa duni zisizo na tija wala thamani kwenye masoko ya kitaifa na kimataifa.Kwa mantiki hiyo, Tanzania sasa ni jalala la kila kitu, kuanzia mitumba na kila uchafu unaotoka nje hasa nchi za Asia .
Je, kwa staili hii ni jeuri gani tunaweza kuwa nayo wakati tumeshindwa kujitegemea karibu kwa kila kitu ? Cha msingi nikuona jinsi taifa letu lilivyo taifa la waoga kiuchumi, kwani badala ya kuanzisha miradi ya kuzalisha mali , tunaanzisha miradi ya uchuuzi ya kuuza karanga na takataka kutoka nje.
Kwetu maendeleo ya uchumi ni kuligeuza taifa kuwa la wachuuzi wa aina ya wamachinga. Sasa ujasiri gani tutakuwa nao wakati karibu sote tumezama kwenye umaskini wa mali , akili,kauli, maadili na elimu na matatizo ya kiafya?.Kwani hakuna ubishi sasa kwamba taifa hili lina wagonjwa wengi sana kuliko tulivyokuwa tukifikiri hapo awali.Na ukweli huo unaendelea kujidhiirisha kule kwa Babu Loliondo(Ambilikile Mwaisapile)jinsi viongozi wetu na wananchi wanavyomiminika kwa wingi huko kupata kikombe cha dawa kinachodaiwa kutibu magonjwa sugu.Hatari sana .
Taifa la aina hii ni taifa duni ambalo litatugeuza kuwa taifa la watumwa wa mataifa mengine.Sasa hivi baadhi ya Watanzania hususani vijana wamechoka hata kufikiri, wanaogopa kufikiri na wako tayari kufuta Utanzania wao ili angalau watawaliwe na taifa lolote linalopenda kututawala.
Wengi wa Watanzania wa leo ni watu wanaopenda kutumia njia za mkato zisizo sahihi kujipatia kipato, hawapendi kufanya kazi wakatoka jasho wanapenda sana starehe na matokeo ya taifa kuwa na watu wa aina hiyo ni kuwa na taifa la matapeli, wasanii, vizabizabina,wala rushwa, wapika majungu,mafedhuli , maafiliti,mabazazi, wazandiki na watu wasioaminika kabisa na hii sasa imeanza kuwa sifa kuu ya Watanzania kimataifa.
Kwa hiyo hivi sasa ukikutana na Mtanzania awe kiongozi, mbunge,majaji,mahakimu,mawakili,maaskari,wanahabari, wapenzi,wafanyabiashara, matajiri, walemavu na wananchi wa kawaida unaanza kuwa na wasiwasi kwamba huyo si mmoja mwenye sifa kama hizo nilizozitaja hapo juu?.
Si siri tena, zile zama za Mtanzania ni kioo cha uadilifu duniani zimeanza kutoweka.Kila mmoja wetu mwenye tabia kama hizo ajirekebishe.
Mungu ibariki Tanzania , Mungu Ibariki Afrika.
0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 29 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment