Header Ads

JAJI MWANGESI AJITOA KESI YA MAHALU

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE jaji Sivangilwa Mwangesi ambaye alikuwa akisiliza kesi ya uhujumu uchumi wa Euro zaidi ya milioni mbili inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Meneja Utawala na Fedha, Grace Martin ametangaza kujiondoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo.


Jaji Mwangesi alitangaza umuzi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ambapo kesi hiyo ilikuja kwaajili ya jaji huyo kutoa uamuzi wa ama kuendelea au kujiondoa katika kesi hiyo kufuatia sababu sita zilizowasilishwa Ijumaa iliyopita na washtakiwa ambayo yalimtaka ajitoe kwasababu hawana imani nae kwasababu amekuwa akiendesha shauri hilo kwa malengo yake badala ya sheria.

“Naheshimu maoni ya washtakiwa ya kunitaka minijiondoe…ila nasema zile sababu zao sita hazina msingi msingi wowote wa kisheria kwani sababu zote za kunikataa mimi zilikwisha tolewa uamuzi na Mahakama Kuu katika ombi namba 2/2009 ililowasilishwa katika mahakama hiyo ya juu na washtakiwa hao ambapo ulilitupilia mbali ombi hilo lililotaka wafutiwe kesi ya msingi kwasababu mahakama ya Kisutu iliendesha kesi hiyo kimakosa; “Ila kwakufuata haki, washtakiwa wanahaki ya kumkataa hakimu au jaji pindi wanapokosa imani na hakimu huyo…na mimi sitaki kung’ang’ania kusikiliza kesi hii kwa misingi ya haki natangaza kujitoa kuendelea na shauri hili kuanzia leo”alisema Jaji Mwangesi na kuondoka ndani ya chumba cha mahakama ya wazi.

Lakini muda mchache baadaye Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Elvin Mugeta aliingia mahakamani na jalada la kesi hiyo ya Mahalu huku tayari wakiwa washaondoka katika eneo hilo la mahakama na kusema kuwa anaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 28 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itakuja kwaajili ya kutajwa na kujua ni hakimu gani amepangwa.

Machi 25 mwaka huu,wakili wa washtakiwa hao, Mabere Marando, Alex Mgongolwa, Alex Mushumbusi,Beatus Malima waliwasilisha sababu sita za kumwomba jaji Mwangesi ajitoe kwenye shauri hilo sababu ya kwanza ni ni kwamba upande wa utetezi ulishatoa mahakamani hapo Ansard ya bunge ya mwaka 2004 iliyomnukuu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya awamu ya tatu ambaye kwasasa ni rais Jakaya Kikwete akieleza bunge kuwa manunuzi ya jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ulikidhi matakwa ya Sheria ya manunuzi ya umma na kwamba hakukuwa na wizi katika ununuzi huo lakini jaji huyo akuzingatia ansard hiyo.

“Sababu ya pili ni wewe Jaji Mwangesi ulipindisha makusudi sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002 ukachukua ushahidi wa shahidi wa jamhuri aliyekuwa nchini Italia kwa njia ya video wakati sheria ya nchi hii inakataza na ndiyo maana hivi sasa serikali inapeleka muswaada bungeni wa kuifanyia marekebisho sheria iliyopo hivi sasa, sheria hiyo mpya ikitungwa ndiyo itakuwa ikiruhusu mahakama kuchukua ushahidi kwa njia ya video”alidai Marando.

Sababu ya tatu; tangu mapema upande wa washtakiwa waliuomba upande wa Jamhuri uwatajie mlalamikaji wa kesi hiyo na upande wa Jamhuri ulishawahi kuieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo haina mlalamikaji lakini jaji huyo alishtushwa na kauli hiyo ya Jamhuri na akaiarisha kesi na kuwautaka upande wa jamhuri ukamlete mlalamikaji na mwisho wa siku jamhuri ilienda kuleta nakala ya nusu kurasa ya maelezo ya mlalamikaji ambaye ni Afisa wa TAKUKURU,na mbaya zaidi jamhuri hadi inafunga kesi yao hakuweza kumleta mlalamikaji huyo kutoa ushahidi wake mahakamani.

“Kwa hiyo sisi upande wa utetezi tunasema kwa kitendo cha wewe Jaji Mwangesi kuung’ang’ania upande wa Jamhuri walete mlalamikaji wa kesi hiyo huku upande wa Jamhuri ulishawahi kumleleza kuwa kesi hiyo haina mlalamikaji kimetunyima fursa sisi kuwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo ifutwe kwasababu ilikuwa haina mlalamikaji”alidai Marando.

Sababu ya nne ni kwamba jaji huyo aliunyima haki upande utetezi wa kuwasilisha majumuisho ya kuwaona hawana kesi ya kujibu pale jaji huyo kwa malengo yake anayoyajua yeye siku Jamhuri ilipofunga kesi yake na ndipo siku hiyo hiyo akatoa uamuzi wa kuwaona washtakiwa wanakesi ya kujibu.

“Sababu ya tano ya kukataa jaji wewe ni kwamba wewe unasikiliza kesi hii kama hakimu wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwasababu mahakama zote zina mipaka ya ardhi ya kufanyakazi zake isipokuwa Jaji Mkuu anaweza kutoa kibali maalum kwa mahakama husika kusikiliza kesi iliyo nje ya mamlaka yake … lakini wewe mheshimiwa jaji hukupata kibali cha Jaji Mkuu na ukadiriki kupokea ushahidi wa shahidi wa Jamhuri aliyekuwa nchini Italia kwa njia ya video jambo ambalo tunaliona ulikiuka makusudi sheria za nchi kwa malengo yako binafsi.”alidai Marando.

Alitaja sababu ya sita ni kwamba alikiuka kwa makusudi sheria za Tanzania kwakukubali kwake kupokea nakala kivuli ya mkataba wa mauzo ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Italia kama kielelezo toka kwa shahidi wa Jamhuri ambaye ni wakili wa nchini italia ambaye alikuja hapa nchini kutoa ushahidi ambapo shahidi huyo aliambia mahakama kuwa kwa mujibu wa sheria za Italia hazimruhusu yeye kuutoa mkataba halisi na jaji huyo akakubaliana na hoja ya shahidi huyo wakati sheria za Tanzania zinakataza hilo na kwamba alikubali kupokea kielelezo hicho ambacho kiliandaliwa na shahidi huyo mwenyewe ambaye ni wakili huyo wa Italia wakati sheria za Tanzania zinakataza mkataba unaondaliwa na mwanasheria husika zisibitishwe na mwanasheria huyo huyo bali zikathibitishwe na mwanasheria mwingine.

Mapema mwaka 2006 ,Jamhuri alimfikisha Mahalu na Martin katika mahakama hiyo wakidai manunuzi ya jengo hilo hayakufuata sheria za manunuzi, na kwamba waliibia serikali kiasi hicho cha fedha kwaajili ya ununuzi wa jengo hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 29 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.