Header Ads

JAJI AJITOA KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE jaji Razia Sheikh anayesikiliza kesi ya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi ukanda wa Tanzania inayowakabili ryaia 34 wa kigeni maarufu kama ‘kesi ya samaki wa Magufuli’ amejitoa kuendelea kusikiliza kesi hiyo.

Jaji Sheikh alitoa uamuzi huo jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufuatia ombi la washtakiwa hao walioliwasilisha mbele yake Ijumaa iliyopita ambapo washtakiwa walimwomba ajitoe kwasababu hawana imani naye.

Jaji Sheikh alisema anajitoa kusikiliza shauri hilo si kwasababu ya hoja zilizowasilishwa na wakili wa washtakiwa John Mapinduzi na Ibrahim Bendera bali anajitoa ili haki ionekane inatendeka na kwamba jalada la kesi hiyo atalipeleka kwa Jaji Mfawidhi Semistocles Kaijage ili aweze kumpanga jaji mwingine.

Alisema mawakili wa washtakiwa waliwasilisha maombi ya kutaka yeye ajitoe kusikiliza kesi hiyo hayana msingi mantiki ya kisheria na kwamba waliyatoa kwa nia mbaya dhidi yake kufuatia uamuzi wake alioutoa Ijumaa iliyopita ambao uliwanyima dhamana washtakiwa.

Jaji Sheikh alisema sababu za kumtaka ajitoe alizozitoa wakili Mapinduzi hazikidhi matakwa ya sheria yaliyowekwa na Mahakama ya Rufani na ya kumlazimu jaji au haki aweze kujitoa katika kesi na kwamba sababu zilizowasilishwa na wakili Mapinduzi wiki iliyopita zilikuwa anatakiwa akazitumie siku atakapoukatia rufaa uamuzi wake katika Mahakama ya Rufani na siyo pale Mahakama Kuu.

“Miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya jaji au hakimu ajitoe kusikiliza kesi ni pamoja na kuonesha upendeleo kwa upande mmoja…hivyo naamua kujitoa kwenye kesi hii siyo kwasababu ya hoja za mawakili wa utetezi ila najitoa ili haki ionekane inatendeka”alisema Jaji Sheikh.

Aidha alisema tuhuma zilizotolewa na wa washtakiwa (Mapinduzi) dhidi yake hazina ushahidi kwani hata mawakili wa washtakiwa walishindwa kuzithibitisha tuhuma hizo ikiwemo tuhuma ya yeye kuichelewesha kesi hiyo kwa makusudi hali iliyosababisha mshtakiwa mmoja kufia jela.

Jaji huyo akiipangua tuhuma kwamba washtakiwa hao hawana imani naye ,alisema tuhuma hiyo haina msingi kwani kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo unaonyesha kuwa ucheleweshwaji wa kesi hiyo umekuwa ukichangiwa na mawakili hao wa utetezi hasa wakili John Mapinduzi.

“Wakili Mapinduzi kwa mujibu wa kumbukumbu ya jalada ya kesi hii ndiyo anaonekana amekuwa mara nyingi haudhulii kesi hii tena hata bila kutoa taarifa”alisema Jaji huyo Aidha Jaji Sheikh aliwashambulia vikali mawakili wa utetezi katika kesi hiyo kwa kusema kuwa licha mawakili hao ni maofisa wa mahakama nchini ambao wanajukumu la kuisaidia kufikia maamuzi ya haki na sahihi lakini cha kushangaza mwenendo wao umekuwa siyo mzuri kwa mahakama hususani wakili Mapinduzi.

Februali 25 mwaka huu, washtakiwa ho kupitia kwa wakili wao Mapinduzi walimtaka jaji huyo ajitoe ikiwa ni saachache tu baada ya jaji huyo kutoa uamuzi wa kuwanyima dhamana licha makosa yanayowakabili yanadhamana kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ila akasema kwa mazingira ya kesi hiyo mahakama hiyo imetumia mamlaka yake kuwanyima dhamana.

Uamuzi huo uliwafanya baadhi ya washtakiwa hao kumwaga machozi baada ya wakalimani wao kuwatafisiriwa uamuzi wa jaji huyo na ndipo kupitia kwa mawakili wao wakamtaka ajiondoe katika kesi yao. Katika sababu zao za kumkataa jaji huyo mmoja wa mawakili wao John Mapinduzi walidai kuwa hawana imani naye kwa kuwa kesi yao imechukua muda mrefu kiasi kwamba hata mwenzao mmoja amefariki akiwa mahabusu.

Pia walidai kuwa hakuna ushahidi kuwa wakipewa dhamana watatoroka kama ambavyo jaji alisema huku wakipinga kuwa wao si wahamia haramu kwa kuwa hawakuwa na mpango wa kuja Tanzania bali walikuja baada ya kutiwa mbaroni na kikosi cha doria cha maafisa wa uvuvi. Walikamatwa Machi 9 mwaka 2009 na kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Makazi Kisutu Machi 12 mwaka huo kabla ya kesi yao kuhamishi Mahakama Kuu mbele ya Jaji Sheikh.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 4 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.