Header Ads

KESI YA WIZI WA GARI LA DPP:SITA WAFUTIWA SHITAKA LA UNYANG'ANYI

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewafutia shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha washtakiwa sita katika kesi unyanganyi wa kutumia silaha, kupokea mali za wizi na wizi wa gari na kompyuta mali ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DDP) vyenye jumla ya thamani ya shilingi sh 111,500,000.


Sambamba na hilo Hakimu Mkazi Jenevitus Dudu ambaye ndiye anasikiliza kesi hiyo ambayo ina jumla ya washtakiwa 12, pia amewaachilia huru washtakiwa watatu ambao walikuwa wakikabiliwa na kosa la kupokea mali za wizi baada ya kuwaona hawana kesi ya kujibu.

Hakimu Mkazi Dudu alisema baada ya kuuchambua ushahidi wa uliwasilishwa na wakili mwandamizi wa serikali Timon Vitals amebaini kuwa ushahidi huo umeshindwa kuthibitisha kuwa washtakiwa sita , Ally Mustapha,Haji Mwanga,Bakari Makala,Deogratius Chuwa, Philipo Jose na Abubakar Kamugisha ambao ndiyo walikuwa wakikabiliwa na shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha ambalo kwa mujibu wa sheria halina dhamana kuwa hawakutenda kosa na hivyo akawafutia kosa hilo na kufanya washtakiwa hao wakibaki wakikabiliwa na makosa mawili ya wizi na kupokea mali za wizi.

Hakimu Dudu alisema baada ya kupitia ushahidi wa Jamhuri pia amefikia uamuzi wa kuwaona washtakiwa wanne, Antony Mengi, Wilfred Maleko,Alex Kimaro na Hajat Kileo waliokuwa wakikabiliwa na kosa la wizi wa mali hizo kuwa hawana kesi ya kujibu chini ya kifungu cha 291 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.Na hivyo kuwaona washtakiwa wawili, Mary Lyimo na Jacob Mosha kuwa wana kesi ya kujibu katika kosa wizi wa mali hizo hivyo wanapaswa wajitete.

“Mahakama hii imefikia uamuzi huo kama nilivyouanisha hapo juu kwenye kesi hii iliyokuwa ikiwakabili jumla ya washtakiwa 12 kwasababu jamhuri imeshindwa kuthibitisha shtaka la unyang’anyi kwa washtakiwa sita, bila limeshindwa kuthibitisha shtaka la kukutwa na mali za wizi kwasababu mahakama hii imeona washtakiwa hao wanne ambao walikuwa wakikabiliwa na kosa hilo la kukutwa na mali za wizi hawakuwa wakifahamu mali hizo ni za wazi na pia mahakama hii imewaona washtakiwa nane wana kesi ya kujibu katika shtaka la wizi na kukutwa na mali za wizi.

Baada ya Hakimu Dudu kutoa uamuzi huo , Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Eliezer Feleshi aliwasilisha mahakamani hapo hati ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa sita walifutiwa shtaka la unyang’anyi kwa kutumia silaha ambalo kwa mujibu wa sheria za mwenendo wa makosa ya Jinai ya mwaka 2002, shitaka hilo halina dhamana na Wakili wa Serikali Zuberi Mkakati naye akawasilisha mahakamani hapo hati ya kusudio ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi wa hakimu huyo.

Aidha kwa upande wake Hakimu Dudu baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha hati hizo mbili, alisema leo kesi hiyo ilikuja kwaajili washtakiwa sita kutimiza masharti ya dhamana lakini kwakuwa DPP amewasilisha hati ya kufunga dhamana kwa washtakiwa hao akasema anaiarisha kesi hiyo hadi Aprili nne mwaka, ili kuipa nafasi ya hati hiyo ya DPP ambayo inazuia washtakiwa hao wasipewe dhamana na na akaamuru washtakiwa hao kurejeshwa rumande.

Hata hivyo baadhi ya ndugu na jamaa wa washtakiwa ambao wamesota rumande tangu mapema mwaka 2009 hadi sasa,waliokuwa wamefika mahakamani hapo kwaajili ya kukamilisha taratibu za kuwadhamini washtakiwa, walijikuta wakiangua vilio baada ya kusikia jamhuri imewasilisha hati ya kukataa rufaa na DPP kuwasilisha hati mahakamani ya kuzuia washtakiwa hao wasipewe dhamana.

Mapema mwaka 2009 mahakamani hapo Inspekta Emma Mkonyi alidai kuwa Machi 5 mwaka huo, huko Tabata Liwiti CCM, Kamugisha aliiba gari STK 5002 Toyota Hiace modeli mpya lenye thamani ya sh 56,972,000, komyuta sita zenye thamani ya sh 4,250,000, printa zenye thamani ya sh 7,435,000, seti ya UPS, laptop na vitabu vya sheria mali ya ofisi ya DPP na vitu vyote hivyo vikiwa na jumla ya thamani ya sh 111,500,000.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 19 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.