Header Ads

MPENDAZOE ALIPA KORTINI SH MIL 15/-

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE aliyekuwa Mgombe Ubunge wa Jimbo la Segerea (Chadema),Fred Mpendazoe amelipa sh milioni 15 katika Idara ya Fedha ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam ikiwa ni dhamana ya kesi yake ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa jimbo uliofanyika mwaka jana ambayo yalimtangaza Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Dk.Makongoro Mahanga (CCM) kuwa ndiye mbunge wa jimbo hilo.

Mbali na Dk.Mahanga wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo na katika madai yake mlalamikaji ambaye ni Mpendazoe anataka mahakama kuu itengue ushindi wa Dk.Mahanga kwakuwa taratibu za sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010 hazikufuatwa.

Wakili wa Mpendazoe, Peter Kibatala jana ndiye aliyekwenda idara ya hiyo ya fedha iliyopo ndani ya jengo la Mahakama ya Rufani nchini kulipa kiasi hicho cha fedha na kuwaonyesha waandishi wa habari risiti ya malipo hayo.

“Hii ndiyo risiti ya kiasi hicho cha fedha nilicholipa mahakamani kama dhamana ya kesi iliyofunguliwa na mteja wangu ….na kwakuwa tayari tumeishalipa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya kuupata udhibitisho wa malipo haya ndiyo atapanga tarehe ya kesi ya mteja wangu kuanza kusikilizwa rasmi kwani taratibu zote za kisheria tumeishazikamilisha”alisema wakili Peter Kibatala.

Machi nane mwaka huu, Jaji Profesa Ibrahimu Juma alitupilia mbali pingamizi la wakili Jerome Msemwa anayewatetea wadaiwa liloiomba mahakama hiyo imzuie Mpendazoe asiruhusiwe kuweka kiasi hicho cha fedha mahakamani kwasababu muda wa kuwasilisha fedha hizo ulikuwa umeishapita kwakuwa halikuwa limekidhi matakwa ya kisheria na badala yake akalikubali ombi la Mpendazoe kuweka mahakama kiaisi hicho cha fedha kama dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 12 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.