Header Ads

VIONGOZI ACHENI KUMSINGIZIA MUNGU

Na Happiness Katabazi

LEO Machi 8 ni Siku ya Wanawake Duniani. Hivyo wanawake tunasherehekea siku hii kwa njia mbalimbali.


Binafsi naisherehekea siku hiyo kwa kutumia kalamu yangu kuandika makala hii.

Heko wanawake duniani, kwani naamini katika dhana hii isemayo: “Katika mafanikio ya mwanamume, basi mwanamke yuko nyuma yake.”

Wanawake tunaweza sana, licha ya kuwepo baadhi ya wanaume wasiopenda mabadiliko na wenye chuki binafsi sehemu za maofisini, majumbani na mitaani ambao wamekuwa wakiwagandamiza wanawake makusudi.

Leo wakati tukisherehekea siku yetu, wanawake tutiane moyo katika kuvitokomeza kwa nguvu zote vikwazo hivyo tunavyowekewa na baadhi ya wanaume ambao ama wana madaraka mahali pa kazi, biashara, vyama vya siasa na kwenye ngazi ya familia.

Lakini nitakuwa sijatenda haki kama wanawake Watanzania leo tunavyoungana na wenzetu duniani hatuna budi kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwani katika serikali ya awamu ya nne ni wazi ameweza kuwateua wanawake wengi kuwa majaji, wakurugenzi, mawaziri na manaibu waziri.

Nimeshuhudia wanawake wengi wakiwemo katika vyombo vyetu vya dola kama ulinzi na usalama.Heko Kikwete katika hilo. Nirejee kwenye mada yangu ya leo.

Taifa linalochakachua elimu, taifa linalochakachua mfumo wake wa elimu, taifa hilo ama halipo au limo njiani kuangamia.
Kwa sababu ufahamu ni mfumo wa akili za binadamu kutambua mambo, ukweli na vitu vinavyomzunguka. Ufahamu ndiyo elimu yenyewe na ndiyo moyo wa elimu. Kwa maana kwamba hakuna kitu binadamu anakijua bila ufahamu. Ukiondoa ufahamu binadamu tutakuwa hakuna kitu tutakachokuwa tunakijua.

Kwa hiyo mambo tunayoyajua na tunathibitisha kuwa ni kweli ndiyo ambayo tunayafundisha kuwa ni ya kweli. Kwa hiyo elimu msingi wa kwanza ni ukweli.

Sasa ukishajua ukweli, binadamu anaweza kuanza kujitambua.
Sasa hatuwezi kujitambua kama viumbe hai wenye ufahamu ikiwa kile tunachotambua ni ukweli kimechakachuliwa.

Katika kipindi hiki mambo yameharibika kutokana na baadhi kujitambulisha kuwa ni wahandisi kumbe vyeti wameghushi; na watu huo wanapewa kazi ya kujenga daraja ambalo usiku linabomoka kwa kusombwa na maji kisha wananchi wanashindwa kupita, fedha za walipa kodi zilizotolewa kujenga zimeteketea kwa sababu si mtaalamu wa fani ya uhandisi; hakika yote yanatokana na watu kutokuwa wakweli.

Baba au mama anahonga fedha ili walimu wamuuzie mitihani aweze kumpatia mwanae kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani ili aweze kufaulu.

Na mtoto huyo anajikuta anafaulu na kupata daraja la kwanza. Je, kweli elimu aliyoipata mtoto huyo ni sawa ya kufaulu daraja la kwanza?

Na mtoto huyo atazuia watoto wenzake waliopata daraja la pili kwa akili zao. Mtoto huyo aliyepata daraja la kwanza ataenda chuo kikuu na huko nako atapata shahada ya mtindo wa kununuliwa mitihani na wazazi wake na mwisho wa siku anahitimu na kuwa daktari wa binadamu; je, wewe mwananchi au wewe mzazi utaridhika kutibiwa na daktari wa aina hiyo?

Kumbe basi, viongozi wetu wanaokimbilia nje ya nchi kutibiwa mara kwa mara, wanajua ni kitu gani walikifanya kwenye mfumo wetu wa elimu.

Mambo yote mabaya yanayotokea serikalini raia wanalalamika, chimbuko lake ni mfumo wa elimu. Kuna mawaziri hawajui a,b,c za hizo wizara walizopewa kuziongoza.

Hiyo mikataba mibaya inayopingwa sasa, ni matokeo mabaya ya mfumo wa elimu. Hao wanasheria wanaoiandika hiyo mikataba si ni wanasheria wetu? Baadhi ya mawakili wetu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wamekuwa wakiandaa hati za mashitaka zenye dosari za kisheria, hali inayosababisha mahakama kuwafutia mashitaka washitakiwa.

Baadhi ya mahakimu na majaji nao wamekuwa wakiandika hukumu zenye makosa ambazo mwisho wa siku hutenguliwa na mahakama za juu.

Tangu mwaka 2006 mgawo wa umeme ulikuwepo, sasa huo umeme wa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 utatusaidia nini?

Siku chache baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), kutoa hukumu katika kesi ya Dowans na Shirika la Umeme nchini (TANESCO); iliamuru Tanesco iilipe fidia Dowans ya sh bilioni 94 pamoja na riba.

Tulimsikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, akisema hatuna budi kuilipa Dowans,Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akasema tusiilipe. Halafu wote hao ni wanasheria kitaaluma.

Hivi karibuni Brigedia Jenerali mstaafu, Yahya Ali Adawi, alikuja hapa nchini na kujitangaza kuwa yeye ndiye mmiliki mwenye hisa nyingi wa Kampuni ya Dowans, halafu inaibuka Kamati ya Bunge ya Nishati inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba inasema isipowashwa mitambo hiyo mgawo wa umeme hautakoma.

Watanzania tunataka umeme wa zaidi ya megawati 5,000. Serikali ya awamu ya nne tangu mwaka 2006 inagombania umeme wa megawati 100 wa Dowans!
Hivi tuwaulize viongozi wetu, elimu yao waliipata wapi?
Aliyewaambia kuna uhusiano kati ya ukame na uzalishaji umeme ni nani? Hiyo elimu mliipata wapi? Hivi mbona baadhi ya viongozi wetu mnasingizia Mungu?

Hivi nchi zenye ukame kama Saudi Arabia, Somalia na nyingine zilizo kwenye majangwa mbona hawana mgawo wa umeme? Hoja hiyo ya ukame ni dhaifu, ni ya taifa lisilo na elimu.

Taifa la Tanzania lina upepo, makaa ya mawe na gesi kwa miaka mingi tu, nishati zote hizo hazitegemei mvua. Na zipo hapa nchini miaka nenda rudi.

Kwa hiyo dhiki hii ya maisha tunayoipata inayotokana na mgawo wa umeme haina maelezo katika maelezo ya kudra za Mwenyezi Mungu?

Tunamlaumu Mungu bure kumbe sisi wenyewe ni wazembe na wataalumu wetu wa masuala ya nishati ambao wana moyo wa kizalendo hatuwapi nafasi ya kututatulia tatizo hili la umeme ambalo ni wazi litayumbisha pato la taifa.

Sasa hakuna mtu aliyewajibika matokeo mabaya ya wahitimu wa kidato cha nne yalivyotoka hivi karibuni, hakuna mtu anayewajibika tunavyosema mitahala imekosewa. Tumefika mahala hakuna watu wa kuwajibika.

Lakini ni Mungu huyo ndiyo anatuambia tuchukue fedha za walipa kodi tuilipe Dowans? Hizi ndimi mbili zinazotolewa na viongozi wetu wanazipata wapi?

Nchi hii kwa kuwa imeondokana kwenye misingi ya kusema ukweli na hata baadhi ya viongozi wetu wengi hivi sasa wamejifanya mahiri sana wa kutotoa taarifa za ukweli katika baadhi ya mambo. Kwa hiyo lazima taifa letu siku moja litaangamia.

Sipendi tufike huko. Nyie viongozi wetu na sisi wananchi kwa ujumla tujirekebishe na tuwe na hofu ya Mungu.

Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki Afrika.

0716- 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 8 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.