Header Ads

KUBADILI SHERIA,KUNUNUA MITAMBO YA DOWANS NI KUTOHESHIMU UTAWALA WA SHERIA

Na Happiness Katabazi

KUBADILISHA Sheria ya Manunuzi Umma ya mwaka 2004 ili serikali iweze kuinunua mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, ndiyo ufisadi wenyewe na kutoheshimu utawala na dhima nzima ya utawala wa sheria(Rule of Law).

Wahenga walisema ni bora kuchakaza nguo kuliko kuchakazi akili.Sasa ni wazi kuwa baadhi ya viongozi wetu na wataalamu wetu waliopo serikalini wamechaka akili zao.

Na hilo linadhibitisha jinsi miongoni mwao wanavyong’ang’ania ufisadi na kujaribu kwa kila namna kuupa rangi au kuubatiza jina jipya kila siku,.

Kila mtu mwenye akili timamu za kung’amua mambo na akashuhudia kashfa ya Richmond , hanajua kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliunda Kamati maalum ya kuchunguza jambo hilo iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk.Harrison Mwakyembe na kamati hiyo hatimaye iliwasilisha ripoti yake na bungeni.

Na ilipojadiliwa kwa mapana na ikadhihirika wazi kwamba Richmond ni kikundi feki ambacho wala hakikuwa kampuni yenye hisa Marekani wala Tanzania na kwamba tenda ya serikali ya kufua umeme wa dharula ilitolewa kwa kikundi kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.
Mara baada ya bunge kumaliza kuijadili ripoti ya Kamati ya Dk.Mwakyembe, maamuzio yake yalipelekea aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo Edward Lowassa, waliokuwa mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, Nazir Karamagi na Dk.Ibrahim Msabaha walijiudhuru nafasi ya uwazi.

Lakini wajanja walio nyuma ya kampuni hizo wanadaiwa kuwa walijitahdi kuilazimisha Tanesco ama iridhie mrithi wa mkataba wa Richmond na Tanesco ajulikanae kwa jina la Dowans apewe uhalali.

Juhudi hizo zilishindikana kwa kipindi fulani mbunge wa Kigoma Kaskazini. (Chadema),Zitto Kabwe alijitokeza adharani na kutoa maoni yake kwamba mitambo ya Dowans inunuliwe kwa maslahi ya umma.Zitto hakulieleza taifa lina maslahi gani katika kununua mitambo hiyo ambayo inadaiwa kuwa ilishakwishatumika(used).

Cha msingi ni kwamba mitambo ya kufua umeme wa dharula inaundwa mipya viwandani na mnunuzi kuchagua kununua mitambo chakavu na uchagauzi wake ambao labda unasababishwa na ufukara wa kutokuwa na fedha za kununulia mitambo mipya.

Kumbe ikiwa mitambo mipya inauzwa sokoni na hakuna sababu ya taifa letu kununua mitambo iliyokwishatumika.Hivyo maslahi ya umma aliyokuwa anayazungumzia Zitto hatuyajui ni yapi.

Leo hii imezuka hoja kuhusu mitambo ya Dowans.Wanasema iwashe wanaangalia hali ya sasa ya kutokuwepo umeme wa kutosha.Hao hawajali kuwa hali ya mgao wa umeme imekuwa ikitokea kila mwaka hata kabla ya mitambo ya kufua umeme ya Dowans kuingizwa hapa nchini.

Hivi megawati 100 za Dowans zinaweza kusaidia nini kuondoa tatizo hili la katizo la umeme hapa nchini?Tukubali kwamba sekta ya nishati imeendeshwa vibaya na baadhi ya watu wasiyo na upeo ambao hawatangulizi maslahi ya taifa mbele.
Hivi kweli tangu mwaka 2006 serikali imeshindwa kununua hata mitambo mipya kumi tu, hadi inasubiri hicho kibiriti cha Dowans?

Sasa tujadili ambalo limezuka sasa ambalo linadaiwa kuwa serikali ipo mbioni kupeleka mswaada bungeni ili sheria ya Manunuzi ya Umma ibadilishwe ili iweze kuinunua mitambo hiyo.Sheria hiyo ya sasa inaizuia serikali kununua mitambo au bidhaa zilizokwishakutumika.Na hiyo ni kuakikisha inaziba mianya ya rushwa.

Binafsi nachelea kusema serikali iununue mtambo huo kwasababu zifuatazo;
Utawala wa Sheria hauruhusu sheria itungwe inayomlenga mtu mmoja au kikundi cha watu.Sheria ya namna hiyo ni mbaya(Bad Law).Mabadiliko hayo yakifanywa yatakuwa yanalenga mitambo ya kufua umeme iliyopo Ubungo ambayo ni mali ya Dowans.

Je! baada ya kuitunga sheria hiyo, tutatunga sasa sheria ya kuifuta hiyo sheria mpya ili turejee kwenye sheria yetu nzuri ambayo inakataza kununua vitu ambavyo vimekwishatumika?

Na ikiwa ni hivyo hao baadhi ya maofisa wa serikali akili zao ni nzuri?Kimsingi wana jamii wanasema watu wengine si lazima wafanyekazi serikali kama akili zao haziwatoshi .Waache kazi serikali wasitualibie nchini.

Ikiwa watang’ang’ania hayo tutaendelea kuwanyoshea vidole kwa haki na kwamwe wasidhani wanajamii wa taifa hili hatujui utawala bora nini.

Mungu Ibariki Tanzania , Mungu Ibariki Afrika.
0716 774494


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 22 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.