Header Ads

MENGI AKWAA KISIKI KORTI KUU


Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa ametoa amri ya kurudishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jalada ya kesi ya madai ya kashfa ya shilingi moja iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mfanyabiashara Yusuf Manji dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi na ITV.


Jalada la kesi hiyo ambayo lilitua katika Mahakama Kuu Machi 23 mwaka huu, likitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na barua ya februali 23 mwaka huu, iliyoandikwa na wakili wa mdaiwa(Mengi) , Michael Ngaro kwa Jaji Mfawidhi Semistocles Kaijage ambapo ndani ya barua hiyo Ngaro alimuomba Jaji Kaijage apitie mwenendo mzima wa kesi hiyo kwani hakimu mkazi anayeisikiliza kesi hiyo Alocye Katemana ametoa maamuzi kadhaa yanaoonyesha anaupendelea upande wa mlalamikaji(Manji).

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu, vililiakikishia Tanzania Daima tayari Jaji Kaijage alishatimiza wajibu wake wa kulipitia jalada hilo na kwamba jalada la kesi na amebaini hakuna sheria zozote zilizokiukwa na Hakimu Mkazi Katemana shauri hivyo ameamuru jalada hilo lirudishwe katika mahakama ya Kisutu na liendelee kusikilizwa kwa hakimu yule yule Katemana.
“Tunakuakikishia kwamba Jaji Mfawidhi Kaijage alishatimiza wajibu wake wa kulipitia jalada hilo na amebaini kuwa Hakimu Mkazi Katemana hakupindisha sheria yoyote hivyo ameliamuru jarada hilo lirejeshwe katika katika mahakama ya Kisutu na hakimu yule yule Katemana ndiye aendelee kulisikiliza;

“Na jalada la kesi hiyo ya Manji na Mengi limeishatoka hapa mahakama kuu tangu jana (Juzi) na kupelekwa Mahakama ya Kisutu kwa hakimu Katemana…hivyo ukienda mahakama ya Kisutu utaweza kujua kesi hiyo imepangwa tarehe ipi kwaajili ya kutajwa ama upande wa mlalamikaji (Manji)kuendelea kujitetea”vilisema vyanzo vyetu.
Hata hivyo alipotafutwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,Kaijage ili aweze kuthibitisha taarifa hizo jana saa tisa mchana hakuweza kupatikana kwasababu simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.

Februali 15 mwaka huu, Hakimu Mkazi Katemana alitupilia mbali ombi la Mengi lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyotolewa na hakimu huyo Februali 11 mwaka huu,ambapo hakimu huyu alikazikataa nyaraka vivuli 14 zikiwemo nyaraka ambazo zinaonyesha ni mali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU),Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mkataba wa kukopeshana fedha baina ya kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd na Kampuni ya Quality Finance Corporation Ltd , ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kanuni ambazo zimeandikwa Na. 25 ya mwaka 2002, zinakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na mahakama ya chini hadi kesi ya msingi itakapomalizika na kutolewa hukumu.

Hakimu Katemana alisema siyo tu sheria hiyo ina kataza maamuzi madogo kama hayo aliyoyatoa kuyakatia rufaa pia nyaraka hizo 14 haziusiani na kesi iliyopo mbele yake, ni nyaraka vivuli ambazo hazijathibitishwa kisheria na pia hazionyeshi kama ofisi hizo za serikali zimetoa kibali kwa mdaiwa kutumia nyaraka hizo katika kesi hiyo na kuongeza kuwa nyaraka hizo zimewasilishwa nje ya muda mwafaka kwani kisheria zilipaswa kuwasilishwa kabla ya mlalamikaji kupanda kizimbani kuanza kutoa ushahidi wake.

Mapema mwaka 2009, Manji anatetewa na mawakili maarufu nchini, Mabere Marando, Richard Rweyongeza, Dk.Ringo Tenga na Beatus Malima alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 31 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.