ZOMBE AISHIKA PABAYA SERIKALI
HATIMAYE aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Mohamed Zombe(57),amemfungulia kesi ya madai ya fidia ya Sh bilioni tano serikali kwasababu ilimnyanyasa, kumdhalilisha,kumbakizia kesi na ilikiuka sheria na Katiba ya nchi wakati ilipomkamata na kumfungulia kesi ya mauji ya watu wa nne.
Zombe kupitia wakili wake Richard Rweyongeza aliifungua kesi hiyo juzi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, na tayari imeishapewa namba 35 ya mwaka 2011.Ambapo mdaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa hati ya madai yenye kurasa tisa ambayo Tanzania Daima imefanikiwa kupata nakala yake, Zombe ametoa sababu 21 za kufungua kesi hiyo ya madai ya fidia ya kutaka alipwe sh bilioni tano na riba ya Sh milioni 200.
Zombe anadai Jeshi la Polisi lilikiuka sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inayotaka kabla ya mtu kukamatwa ni lazima aelezwe anakamatwa kwa sababu gani na akifikishwa kituo cha polisi ni lazima ahojiwe na kuchukuliwa maelezo yake ambayo baadaye hutumika mahakamani kama kielelezo.
“Jeshi la polisi lilikwenda kinyume na sheria hiyo kwani ilinikamata, na kunifungulia kesi hiyo ya mauji bila ya hata ya kunihoji na kunichukua maelezo …kwahiyo utaona kitendo hicho cha polisi walichonifanyia kilininyang’anya haki yangu ya msingi iliyoainishwa kwenye Katiba ya nchi inayosema kila mtu ana haki ya kusikilizwa;
“Mimi licha nilikuwa ni mshtakiwa lakini nilikuwa ninafahamu vyema sheria za nchi hivyo kitendo hicho cha ukiukwaji wa sheria nilichofanyiwa na polisi ambapo nilifikishwa mahakamani bila ya kuchukuliwa maelezo na polisi kiliniathiri kisaikolojia”alidai Zombe.
Aidha Zombe kwa sasa anafanya shughuli zake zinazomuingizia kipato huko mkoani Morogoro na Rukwa,anadai kuwa sababu nyingine ilisababisha afungue kesi hiyo ni Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi(IGP)-Said Mwema kushindwa kulijibu kusudio lake la kuishtaki serikali ambapo kusudio hilo lilikuwa linatakiwa lijibiwe na Mwema ndani ya siku 90.
Anaeleza kuwa Septemba 27 mwaka huu, ndiyo alikabidhi barua hiyo ya kusudio kwa IGP-Mwema na ilionyesha kupokelewa na kiongozi huyo na kwamba siku hizo 90 zilikuwa zikimalizika Desemba 25 mwaka jana.Katika barua yake ya kusudio mlalamikaji huyo alimweleza Mwema kuwa atakwenda mahakamani iwapo masharti hayo ya kuombwa radhi na kulipwa fidia hayatatekelezwa.
Agosti 17, mwaka 2009,Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa hukumu ya kushtusha baada ya kumwachilia huru Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.
Serikali ilikata rufaa Oktoba 7 mwaka 2009 katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachilia Zombe na wenzake.
Akisoma hukumu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, alibaini kuwa serikali ilishindwa kuthibitisha mashitaka na kuwa kamwe mahakama haiwezi kumtiha hatiani mshitakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo, kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria.Kwamba washitakiwa hao si wauaji na aliliagiza Jeshi la Polisi liwatafute wauaji halisi wa marehemu wale.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 9 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment