Header Ads

FAILI KESI YA MANJI,MENGI LAITWA KORTI KUU

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeitisha jalada la kesi ya madai ya kashfa ya shilingi moja iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na mfanyabiashara Yusuf Manji dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi na ITV kwaajili ya kulipitia upya.


Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana wakili wa Manji, Dk.Ringo Tenga alisema kesi hiyo ambayo ilipangwa kuendelea kusikilizwa juzi na jana ilishindikana kusikilizwa na Mahakama ya Kisutu kwasababu wao wamepata taarifa kuwa jalada la kesi ya msingi limeitishwa Mahakama Kuu kwaajili ya kulikagua jarada hilo.


“Kama mlivyoona juzi na jana sisi mawakili wa mlalamikaji na nyie waandishi wa habari tulikaa sana pale mahakama ya Kisutu kusubiri mteja wetu (Manji)aendelee kutoa ushahidi wake lakini baadaye tukaja kupata taarifa kuwa jalada la kesi hiyo limeitishwa Mahakama Kuu na hatujui limeitwa kwaajili ya nini ila kwa mujibu wa sheria za nchi Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuitisha jalada la kesi inayoendeshwa katika mahakama za chini….hivyo tunasubiri taarifa zaidi”alisema Dk.Tenga.

Alipotafutwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Semistocles Kaijage ili aweze kulizungumzia hilo alisema yupo safarini hivyo hayupo kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo.


Februali 15 mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Alocye Katemana alitupilia mbali ombi la Mengi lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyoutoa Februali 11 mwaka huu,wa kuzikataa nyaraka 14 zikiwemo zinazoihusu kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ambazo mdaiwa zinauhusiano na Manji, ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio.


“Nataka ieleweke kwamba mahakama inaongozwa na kutenda kazi zake kwa mujibu wa sheria na hivyo basi mahakama hii inatupilia mbali ombi la mdaiwa (Mengi) lililotaka apatiwe nakala ya uamuzi wangu ili aweze kuomba upitiwe na Mahakama Kuu kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ambazo zimeandikwa Na. 25 ya mwaka 2002, inakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na mahakama ya chini hadi kesi ya msingi itakapomalizika na kutolewa hukumu.


“Sababu hiyo ya kimsingi na kisheria niliyoitoa hapo juu ndiyo imenisukuma kulitupilia mbali ombi hilo la mdaiwa (Mengi) la kutaka kwenda kuiomba Mahakama Kuu iupitie uamuzi wangu niliokwisha utoa kwa maana hiyo kesi hii itaendelea kusikilizwa katika mahakama hii ya Kisutu na hata sasa niko tayari kwa ajili ya kuanza kuisikiliza na imeamriwa hivyo na mahakama hii,” alisema Hakimu Mkazi Katemana kwa kujiamini.


Mapema mwaka juzi, Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 16 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.