Header Ads

KESI YA MANJI Vs MENGI: JALADA LATUA KORTI KUU

Na Happiness Katabazi
JALADA la kesi ya madai ya kashfa ya shilingi moja iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mfanyabiashara Yusuf Manji dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi na ITV, limetua rasmi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu vililithibitishia gazeti hili kuwa jalada hilo limefika mahakamani hapo jana asubuhi likitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Vyanzo hivyo vilibainisha kuwa chanzo cha jalada hilo kuitwa katika mahakama hiyo ya juu ni kutokana na barua ya Februali 23 mwaka huu, iliyoandikwa na wakili wa mdaiwa(Mengi),Michael Ngaro kwa Jaji Mfawidhi Semistocles Kaijage ambapo ndani ya barua hiyo Ngaro anamuomba Jaji Kaijage alipitie mwenendo mzima wa kesi hiyo kwani hakimu mkazi anayeisikiliza kesi hiyo na akatolea maamuzi mbalimbali Alocye Katemana alionesha kuupendelea upande wa mlalamikaji(Manji).

“Nakukuakishia kuwa ni wakili wa Mengi ndiye aliyemuandikia Jaji Mfawidhi Kaijage barua ya malalamiko kwamba Hakimu Mkazi Katemana ameonekana kupendelea upande na jalada hilo limefika leo hapa Mahakama Kuu na hivi lipo mbioni kupelekwa kwa Jaji Kaijage ili aweze kuyafanyia kazi maombi ya wakili wa Mengi”kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo alipotafutwa wakili Ngaro ili athibitishe taarifa hizo hakuweza kupatikana kwani simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.Na gazeti hili lilipomtafuta wakili wa Manji, Mabere Marando alithibitisha kuwepo kwa taarifa hizo za wakili Ngaro kuwasilisha malalamiko hayo Mahakama Kuu lakini hata hivyo kwa upande wao wanachosubiri ni kuitwa na mahakama.

Februali 15 mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Katemana alitupilia mbali ombi la Mengi lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyoutoa Februali 11 mwaka huu,wa kuzikataa nyaraka 14 zikiwemo zinazoihusu kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ambazo mdaiwa zinauhusiano na Manji, ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ambazo zimeandikwa Na. 25 ya mwaka 2002, inakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na mahakama ya chini hadi kesi ya msingi itakapomalizika na kutolewa hukumu.
Mapema mwaka 2009, Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 24 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.