ALIYEGUSHI SAINI YA MIZENGO PINDA KIZIMBANI
Na Happiness
Katabazi
MFANYABIASHARA Amadi Ally Popi(35), jana alifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikakabiliwa na makosa mawili
likiwemo la kughushi barua inayoonyesha imeandikwa na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda.
Inspekta wa
Polisi Hamis Said mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alilitaja kosa la
kwanza linalomkabili Popi ni la kughushi
kinyume na kifungu cha 333,335(a) na 337
cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Inspekta Said alidai kuwa tarehe na siku isiyofahamika ndani ya
jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya
kudanganya Popi alighushi barua
yenye kumbukumbu Na,DA21/3078/01A/142 ya Desemba 3 mwaka 2012 akijaribu
kuonyesha kuwa barua hiyo ni halali na
ilikuwa imeandikwa na kusainiwa na
Waziri Mkuu Pinda.
Said
alilitaja kosa la pili kuwa ni la
kutengeneza nyaraka ya serikali bila ya
kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo kosa ambalo ni kinyume cha kifungu cha 346(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka
2002, ambapo tarehe na siku isiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam, Popi bila ya kuwa na mamlaka yoyote alitengeneza barua hiyo na kuisani na kisha alimpatia
barua hiyo Islamu Mohammed Mtila akijaribu kuonyesha barua hiyo imetoka katika ofisi ya waziri Mkuu na
imesainiwa na waziri Mkuu Pinda.
Hata hivyo
mshitakiwa huyo alikanusha mashitaka yote na Hakimu Lema alisema ili mshitakiwa
apate dhamana ni lazima awe na wadhamini
wawili wanaofanyakazi serikali au kwenye taasisi zinazofahamika ambapo watasaini bondi ya Sh.milioni 10 na
mmoja katika wadhamini hapo atawasilisha mahakamani hati ya mali
isiyoamishika yenye thamani hiyo,
masharti ambayo yalishindwa kutekelezwa na mshitakiwa huyo na hivyo hakimu Lema
aliamuru mshitakiwa apelekwe rumande hadi Septemba 5 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja
kwaajili ya kutajwa na upepelezi wa shauri hiyo haujakamilika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi Agosti 24 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment