TRAFIKI 'FEKI' ATINGA KORTINI
Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Trafiki ‘feki’ James Hassan
(45) Mkazi wa Kimara jana alifikishwa
katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa mawili likiweko kosa la kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Wakili wa Serikali Nassor Katuga
mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,Joyce Minde,alidai kuwa Agosti 14, mwaka huu,
eneo la Kinyerezi katika eneo la mnara
wa Voda, mshitakiwa kwa njia ya udanganyifu alijitambulisha kwa Inspekta wa
Polisi, Gabriel Chiguma, kuwa ni askari wa kikosi cha usalama barabarani.
Wakili Katuga alidai siku hiyo kwa
njia ya udanganyifu mshitakiwa huyo alikutwa akiwa na sare za Jeshi la polisi ambazo
ni kofia, jaketi na mkanda wa kiunoni.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana
mashitaka, ambapo Katuga alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe
nyingine ya kutajwa.
Mshitakiwa huyo aliomba apewe
dhamana, ambapo Hakimu Joyce alitaja masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na
wadhamini wawili wenye makazi ya kudumu watakaotia saini dhamana y ash. Milioni
saba.
Hata hivyo mshitakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana
na hakimu Minde akaamuru apelekwe
gerezani hadi Septemba 5 mwaka huu, kesi
hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 23 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment