KIBANDA ANA KESI YA KUJIBU
Na Happiness
Katabazi
MAHAKAMA ya
Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemuona aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa
Gazeti la Tanzania Daima,Absalom Kibanda na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya
kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi wana kesi ya kujibu.
Uamuzi huo
ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema jana muda mfupi baada ya wakili
wa serikali Beatha Kitau kuambia mahakama kuwa upande wa jamhuri umeifunga kesi
yake na kwamba mashahidi watatu waliowaleta kujenga kesi hiyo wanatosha.
Hakimu Lema
alisema alisikiliza ushahidi mashahidi wa upande wa jamhuri amefikia uamuzi wa
kuwaona washitakiwa wote wanakesi ya kujibu na hivyo haoni haja ya kutoa nafasi
kwa mawakili wa jamhuri na utetezi kupewa mwenendo wa kesi hiyo ili waeende
kuandaa majumuisho ya kuwaona washitakiwa hao wanakesi ya kujibu au la.
Hata hivyo
wakili wa Kibanda, Isaya Matambo aliomba mahakama impatie mwenendo wa kesi hiyo
ili aweze kuupitia na kwenda kujiandaa na kisha awasilishe maombi ya kuiomba
mahakama imuone Kibanda hana kesi ya kujibu, lakini hakimu huyo alitupilia
mbali ombi hilo na kusema kuwa yeye ndiye ameisikiliza kesi hiyo mwanzo hadi
hapo ilipofikia jana na ameona washitakiwa wana kesi ya kujibu na haoni sababu
ya kutoa nafasi ya mawakili kwenda kuandaa maombi ya kuwaona wateja wao wana
kesi ya kujibu na akaiarisha kesi hiyo hadi Septemba 3 mwaka huu, itakapokuja
kwaajili ya washitakiwa kuanza kujitetea.
Mbali na Kibanda washitakiwa wegine ni Mhariri Mtendaji wa
Gazeti la Tanzania Daima, Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi
Communication Ltd, Theophil Makunga, na mchangiaji wa makala kwenye gazeti la
Tanzania Daima, Samson Mwigamba.
Shtaka la pili ni kuchapisha waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1) ( c) na 31 (1)(a) vya Sheria ya Magazeti namba 229 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 linalomkabili Makunga.
Novemba 30 mwaka 2011 gazeti la Tanzania Daima toleo namba 2552 lilichapisha makala inayodaiwa kuwa ya uchochezi yenye kichwa cha habari ‘Waraka Maalum kwa Askari Wote’.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 15 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment