Header Ads

PONDA AFUTIWA KESI DAR,AFUNGULIWA KESI MOROGORO




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imemfungulia mashitaka matatu na kisha kumnyima dhamana Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, kutokana na kukiuka agizo la mahakama.

Hatua hiyo ilikuja ikiwa ni muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana kumfutia kesi ya uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofunguliwa hivi karibuni.

Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, baada ya kuwasili kwa helikopta ya Jeshi la Polisi katika uwanja wa gofu mjini Morogoro.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bernard Kongola, alisema kuwa Agosti 10, mwaka huu, katika eneo la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu wasikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwa madai kuwa zimeundwa na BAKWATA, ambao ni vibaraka wa CCM na serikali.

Alidai kuwa Sheikh Ponda aliwaagiza waumini hao kuwa endapo watu hao watajitokeza kwao na kujitabulisha kwamba ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha wawapige.
Ilielezwa kuwa kauli hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyotolewa na Hakimu V. Nongwa Mei 9, mwaka huu, ambayo ilimtaka Ponda ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani.
Katika shitaka la pili, Kongola alidai kuwa Agosti 10, mwaka huu, katika eneo la Uwanja wa Ndege, Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu kuwa serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi ili kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi hao ni Waislamu.

Kwamba, Ponda aliwaambia wafuasi wake kuwa serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa huko ni Wakristu.

Shitaka la tatu ambalo linafafana na lile la pili, ambalo nalo linadaiwa kutendwa Agosti 10, mwaka huu, ambapo kauli ya Ponda inadaiwa kuumiza imani za watu wengine kinyume cha kifungu cha sheria namba 390 na kanuni ya adhabu namba 35 cha mwaka 2002.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo na kuyakana, mwanasheria wa serikali aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kupanga kuanza kusikilizwa Agosti 28, mwaka huu.
Mapema baada ya Sheikh Ponda kuwasili mjini hapa kwa helikopta, aliingizwa kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na magari mengine matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la mahakama.

Alipofikishwa eneo la mahakama saa 5:00 asubuhi, magari yalisimama kwa takriban dakika 30, kisha akashuka akiongozana na askari kadhaa kuingizwa mahakamani.

Mawakili wake, Ignas Punge na Bartlomelo Tarimo, walisema sababu za kuomba kesi isikilizwe tarehe hiyo ni kutokana na mteja wao kuwa bado mgonjwa, anayehitaji kupatiwa matibabu.
Baada ya kesi kuahirishwa, Ponda alipandishwa tena katika helikopta mchana kurejeshwa jijini Dar es Salaam.

Mapema jana saa tatu asubuhi Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana saa tatu asubuhi imemfutia kesi  mpya ya  uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Sheikh Ponda Issa Ponda.

Hakimu Mkazi Hellen Liwa alisema amefikia uamuzi huo wa kumfitia kesi Ponda kwasababu wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kuwasilisha mahakamani hapo hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi  chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 , kwasababu DPP hana haja ya kuendelea kumshitaki Ponda katika kesi hiyo ya jinai na. 144/2013 na hivyo namwachiria huru.

Hata hivyo baada ya hakimu Riwa kumwachilia huru,Ponda ambaye aliletwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi na wanausalama wa polisi na magereza chini ya ulinzi mkali, alikamatwa tena na kupakizwa kwenye magari ya wanausalama hao ambapo baadhi ya wanausalama hao waliliambia gazeti hili kuwa wanampeleka Ponda mkoani Morogoro kwaajili ya kufunguliwa makosa matatu ya uchochezi, kufanya mkusanyiko haramu na kisha akarejeshwa gereza la Segerea Dar es Salaam.

Agosti 15 mwaka huu, wanausalama walimwondoa Ponda katika wodi ya MOI na kuwamishia katika gereza  la Segerea ili kusubiria kesi yake hiyo ambayo ilipangwa kuja kutajwa Agosti 28 mwaka huu.

Agosti 14 mwaka huu, saa kumi jioni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamia katika wodi ya MOI  na wakili Kweka alimsomea shitaka Ponda ambaye anakabiliwa na kesi hiyo ya Jinai Na.144 ya mwaka huu.

Wakili Kweka alidai mshitakiwa huyo anakabiliwa na kosa moja aambalo ni uchochezi kuwa Juni 2  hadi Agosti 11 mwaka huu, katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  akijifanya yeye ni Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania,  aliwashawishi waumini wake katika maeneo hayo kutenda makosa ya jinai, ikiwemo kosa la  kutoa lugha  ya kudhalilisha  dhidi ya viongozi wa serikali . kutoa maneno  ambayo yalikuwa na lengo ya kuamsha hisia na mawazo mabaya ya kidini  na aliwashawishi  wafuasi wake kufanya  mikusanyiko,maandamano haramu mkinyume na kifungu cha  390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Baada ya wakili Kweka kumaliza kumsomea shitaka hilo,hakimu Riwa alitoa amri iliyotaka Ponda aendelee kukaa chini ya ulinzi wa vyombo vya ulinzi.

Mei 9 mwaka huu, aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Victoria Nongwa alimfunga Ponda kifungo cha mwaka  mmoja jela baada ya kumkuta na hatia katika kosa moja kati ya matano yaliyokuwa yakimkabilia mbapo kosa alilomtia nalo hatiani ni kosa la kuingia kwa jinai kinyume na kifungu cha 85 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, katika kiwanja cha Ch’angombe Marks.

Katika hukumu yake Hakimu Nongwa alisema anamfunga kifungo cha nje kwa mwaka mmoja, ila wakati Ponda akitumikia adhabu hiyo anatakiwa asitende makosa.

Oktoba 18 mwaka jana, Ponda na wenzie 49 walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa matano, kosa la kwanza ni la kula njama, kujimilikisha mali, kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chan’ombe Markas,wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh. Milioni 59 na kosa la uchochezi ambapo katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na serikali Tumaini Kweka na hakimu Nongwa akitoa hukumu yake alisema anawaachiria huru washitakiwa 49  kwasababu jamhuri wameshindwa kuthibitisha kesi dhidi yao na kwamba anamtia hatiani Ponda kwa kosa moja tu  la kuingia kwa jinai na kwamba na anamuachiria huru katika makosa manne yaliyosalia kwasababu pia jamhuri ilishindwa kuthibitisha mashitaka hayo dhidi ya Ponda.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 20 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.