Header Ads

HAKIMU PAMELA KALALA ASHINDA KESI YA RUSHWA





Na Happiness Katabazi

HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam,imemwachia huru Hakimu  wa Mahakama ya Wilaya ya  Ilala ,Pamela Kalala, aliyekuwa akikabiliwa na  makosa mawili  ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 900,000 baada ya kuomba hana kesi ya kujibu.

Uamuzi huo ulitolewa jana asubuhi na Hakimu Mkazi Alocye Katemana ambaye alisema kwa mujibu wa vielelezo na ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa  jamhuri katika kesi hiyo, mahakama yake yake imeona upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yake.

Hakimu Katemana alisema kwa mujibu wa hati ya mashitaka inaonesha Taasisi ya Kuzuia ya Kupambana na Rushwa, walidai kuwa Kalala aliomba na kupokea rushwa kutoka kwa  Josephine Wage ambaye ni mke wa mshitakiwa Abubakar Mzirai  ambaye Kalala alikuwa akiisikiliza kesi ya jinai inayomkabili Mzirai ili amsaidie.

‘Lakini mimi nimeyasoma malalamiko yaliyoandikwa na Joseph kuhusu Kalala na nimebaini katika malalamiko yake Josephine alikuwa akilalalamika kuwa Hakimu Kalala alimpomfutia dhamana mumewe(Mzirai),hakutaja sababu za kumfutia dhamana na akalalamikia mwenendo wa kesi, lakini hakuna mahala popote alipolalamika kuwa Kalala alimuomba au kumpatia rushwa;

Ila nilichobaini ni kweli hakimu Kalala alishindwa kuandika sababu za kumfutia dhamana mshitakiwa licha sababu hiyo haiwezi kuishawishi mahakama hii imuone mshitakiwa huyo ana kesi ya kujibu….na kwasababu hiyo mahakama hii inamuachiria huru kwasababu upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo ya rushwa dhidi ya hakimu Kalala”alisema Hakimu Katemana.

Awali ilidaiwa na wakili wa serikali  Kasamala alidai Pamela akiwa mwajiriwa wa Mahakama, kama Hakimu Mkazi na wakala wa Sheria ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), kifungu namba 11 ya mwaka 2007, aliomba rushwa kutoka kwa Josephine Wage, mke wa mshtakiwa katika kesi ya jinai namba 703 ya mwaka 2008, jamhuri dhidi ya Abubakar Mziray na wenzake.
Kasamala alidai Pamela alitenda kosa hilo, ili kumshawishi kutoa uamuzi wa kumpendelea mumewe.

Alidai kuwa katika shtaka la pili, Hakimu Mkazi Pamela anadaiwa tarehe mbalimbali Februari mwaka huu, eneo la Manispaa ya Ilala, akiwa na wadhifa huo, alipokea sh 800,000 kutoka kwa Josephine.

Pia anadaiwa Februari 6 mwaka huu, katika eneo hilo, alipokea tena sh 100,000 kutoka kwa Josephine.

Hiyo si mara ya kwanza kwa mahakimu kufikishwa mahakamani hapo kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.

Aliyekuwa hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Jamila Nzota, alifikishwa katika mahakama hiyo na mwaka 2010 alitiwa hatiani kwa makosa hayo na kufungwa jela miaka mitatu.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 30 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.