NTAGAZWA ALIPONDA JESHI LA POLISI
Na Happiness Katabazi
WAZIRI wa zamani Arcado
Ntagazwa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, analishangaa
Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini kujitwishwa jukumu
lisilolao la kuamua kumfungulia kesi ya jinai inayomkabili wakati kisheria kesi hiyo ilipaswa iwe ni ya madai.
Ntagazwa ambaye hivi sasa ni
Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ni msomi wa taaluma ya
sheria alieleza hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Gene Dudu wakati akitoa utetezi
wake katika kesi ya kujipaia kofia ,fulana zenye jumla ya thamani ya Sh.milioni
74.9 kwa njia ya udanganyifu.
Ntagazwa ambaye anatetewa na
wakili wa kujitegemea Alex Mshumbusi alitoa maelezo hayo wakati akipangua
maswali aliyokuwa akihojiwa na wakili wa serikali Charles Anindo ambapo alidai kuwa kesi hiyo ilipaswa iwe nay
a madai na aliyekuwa na haki ya
kuifungua ni mkwe wa Edward Lowassa, Noel Severe ambaye ni mkurugenzi wa
kampuni ya Visual Storm na siyo Polisi ,DPP kwani Polisi ,DPP wanajukumu la
kufungua kesi ya jinai tu na siyo kesi za madai.
Akiongozwa na wakili
Mshumbushi kutoa utetezi wake, Ntagazwa alieleza kuwa yeye ni miongozi wa wadhamini wa Asasi isiyo
ya kiserikali ya FORD na kwamba mwaka
2010 taasisi hiyo ilikuwa inataka kumuenzi Baba wa Taifa Julias Nyerere ambaye
Oktoba 14 mwaka 2010 alikuwa anatimiza miaka 10 tangu afariki dunia na kwamba
FORD ilikuwa imeandaa mradi ukiwemo wa kutengeneza fulana, kofia zilizokuwa
zinapinga vitendo vya kifisadi kwaajili ya kumuenzi Nyerere na kwamba FORD
kwakuwa haikuwa haina fedha, iliamua kuandika mradi na kuupeleka kwa wafadhili
mbalimbali ili ziweze kuwapatia fedha za kuweza kufanikisha mradi huo uliokuwa umebeba dhima ya kumuenzi Nyerere
kwa kupinga ufisadi.
“Baada ya kupeleka maombi
yetu hayo kwa wafadhili, wafadhili walikubali ombi letu na wakatuambia
tuendelee na taratibu nyingine na kwamba watatupatia fedha…na sisi FORD kwa
kuanzia tulienda kuona na kampuni ya Visual Storm ambayo mmoja wa wakurugenzi
wake ni Mkwe wa Lowassa , Severe na kumwomba atutengenezee fulana na kofia zenye thamani ya Sh.milioni 74.9 na tulimweleza mapema kuwa wafadhili
wakitupatia fedha tutamlipa na Severe alitukubalia akatutengenezea hizo fulana
na FORD na Visual Storm haikuwa imeandikishia mkataba wa maandishi kwaajili ya
kazi hiyo;
“Lakini ilipofika Januari 23 mwaka 2010 gazeti la Mtanzania
lilichapisha habari iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Vigogo
walioisaliti CCM wahanikwa’. Na ndani ya habari hiyo zilipigwa picha fulana
zetu ambazo zilitengenezwa na Visual Storm na hiyo habari kumbe ilisomwa vizuri
na wale wafadhili waliokuwa wametuahidi kutupatia fedha, wale wafadhili
wakashtushwa na habari ile wakatuita viongozi wa FORD na kueleza kuwa
hawatawafadhili tena fedha kama walivyowaadi kwasababu kutokana na habari hiyo
wameona kumbe FORD siyo asasi ya kirai ni chama cha siasa cha upinzani” alidai
Ntagazwa.
Ntagazwa ambaye alikuwa
akitumia lugha ya Kiingereza na kisheria
kujitetea alieleza kuwa baada ya wafadhili wale kujitoa, FORD wakaamua kwenda
polisi kutoa taarifa kuhusu habari hiyo iliyochapishwa na gazeti la Mtanzania
lakini baada ya muda mfupi baadaye alishangaa polisi wanakuja kumkamata
nyumbani kwake akiwa bafuni na hadi leo polisi hawajawai kumchukua maelezo ya
onyo na jeshi la polisi na akashtukia
anafunguliwa kesi hiyo ambayo alilisitiza ni kesi ya madai siyo ya jinai na
polisi imekuwa ni jadi yao sasa kudandia mambo hata yasiyowahusu mke na mume
wanadaiana polisi wanaingilia kati.
“Kwanza nikuulize wewe wakili
wa serikali Charles hivi hata kama kweli kesi hii ilikuwa inatakiwa iwe ya
jinai ,minikifungwa jela ndiyo huyo Severe atazipata hizo fedha?,Umesikia wewe
kijana nenda kamwambie huyo Severe kuwa
polisi wamemdanga sana kwa kumshauri anifungulie kesi ya jinai….narudia
tena hata nikifungwa ndiyo hizo hela atalipwa na polisi? Hizo fulana hadi leo
zipo nyumbani kwa mjumbe wa wadhamini wa FORD ,Wakili Steven Thonya ambaye naye ni wakili na atakuja kutoa
ushahidi wake na hata leo hii mahakama ikitaka kuthibitisha hilo iamie nyumbani
kwa Thonya na itazikuta hizo fulana” alidai Ntagazwa na kusababisha watu
kuangua vicheko.
Baada ya Ntagazwa kumaliza
kutoa utetezi wake hakimu Dudu aliarisha kesi hiyo hadi Septemba 17 mwaka huu, itakapokuja kwaajili mshitakiwa
wa tatu ambaye ni mtoto wa Ntagazwa, Dk. Webhale Ntagazwa na mshitakiwa wa
kwanza Senetor Mirelya (60) alishamaliza kutoa utetezi wake.
Aprili 23 mwaka 2012,
ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Ladslaus Komanya kuwa Oktoba 22 mwaka 2009 huko Msasani
Mikoroshini washtakiwa hao kwania ovu walijipatia fulana 5000 na kofia 5000
zenye jumla ya thamani ya Shilingi milioni 74.9 toka kwa Noel Sevele kwa
makubaliano kuwa wangemlipa Sevele kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha
mwezi mmoja tangu walipochukua vifaa hivyo lakini hata hivyo walishindwa
kumlipa na washtakiwa walikana shtaka na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika.
Ntagazwa ambaye kwa sasa ni
Kada wa Chadema , kabla ya kujiunga na chama hicho miaka minne iliyopita,
akitokea chama cha Mapinduzi (CCM).Akiwa mwanachama wa CCM, aliwahi kuteuliwa
na rais wa Serikali ya awamu ya pili na ya tatu, Ally Hassan Mwinyi na Benjamin
Mkapa kushika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali hadi ilipofika
mwanzoni mwa mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete alipounda baraza lake jipya la
mawaziri na kuamuacha nje ya baraza hilo.
Ntagazwa ambaye aliwahi kuwa
mbunge wa muda mrefu wa Jimbo la Mhambwe kwa tiketi ya CCM, hadi sasa
nakumbukwa kwa msemo wake mmoja maarufu aliowahi kuutoa bungeni akiwa Waziri
Nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira alisema ‘Ipo siku
wajukuu zetu watafukua makaburi yetu wachunguze ubongo wetu kama tulikuwa na
akili timamu’. Ntagazwa alitoa msemo huo kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya
maamuzi yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji waliopewa dhamana.
Chanzo:Gazeti la
Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 28 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment