Header Ads

RUFAA YA WAFUASI WA PONDA YAANZA KUUNGURUMA


Na Happiness Katabazi
WAFUASI 53 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ,Sheikh Issa Ponda Issa, ambapo Machi 21  mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, iliwahukumu adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela, wameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, itengue hukumu hiyo na iwaachirie huru .
 
Maombi hayo yaliwasilishwa jana na mawakili wao Ibrahim Tibanyendera na Yahya Njama mbele ya Jaji Salvatory  Bongole, wakati akiwasilisha sababu za rufaa yao iliyokatwa na waomba rufaa Salum Bakari Makame na wenzie 52 ambao wapo magerezani wakitumikia adhabu hiyo  ambapo wakili Tibanyendera alidai kuwa wanasababu tisa za kupinga hukumu ya mahakama ya chini na jana wakili huyo aliweza kuwasilisisha jumla ya sababu mbili.
 
Wakili Tibanyendera aliomba Mahakama Kuu itengue hukumu ya mahakama ya Kisutu, kwasababu Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambaye ndiye alitoa hukumu ile yenye dosari nyingi za kisheria na akasema amewatia hatiani kwa makosa matatu ya kula njama,kufanya mkusanyiko haramu na kukidi amri ya jeshi la polisi liliwataka wasiaandamane kwenda ofisini kwa Mkyurugenzi wa Mashitaka(DPP), dk.Eliezer Feleshi kushinikiza ampatie dhamana Ponda ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 ambaye alihukumu kifungo cha mwaka mmoja jela.
 
Tibanyendela alidai kuhusu kosa la kwanza la kula njama kwa mujibu wa rekodi ya hukumu, ile hakuna ushahidi unaonyesha washitakiwa walikutana mahali kokote kupanga njama ya kutenda kosa hilo lakini wanashangazwa na Hakimu Fimbo kuwatia hatiani kwa kosa hilo kwa shahidi kwanza hadi wa 10 ambao ni maofisa wa polisi walieleza mahakama kuwa waliwakamata washitakiwa hao katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam Februali 15 mwaka huu.
 
Wakili Tibanyendera alikilichambua kosa la kula njama kutenda kosa kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kosa la pili ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifungu cha 74 na 75 cha sheria hiyo  ambavyo vinasomwa pamoja na kifungu cha 43(2)(4) na 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002.
 
‘Kwa masikitiko makubwa tu   nasema kosa la kula njama halikuthibitika, na hakimu Fimbo alikosea kuwatia hatiani kwa kosa la kula njama kwa kutumia kifungu hicho cha 384 cha sheria ya Kanuni ya adhabu. Na kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002,inasema wazi kabisa mtu anayekutwa a hatia ya kutenda kosa la mkusanyiko haramu atapaswa alipe faini ya Sh.50,000 au kwenda jela miezi mitatu au vyote pamoja:
 
‘Lakini tunashangaa huyu hakimu Fimbo ameto adhabu ya juu kabisa ya mwaka mmoja jela..sijui hiyo sheria ameipata wapi?Tunaomba mahakama hii itengue hukumu hiyo kwani inadosari nyingi za kisheria na hakukuwa na ushahidi wowote wakuweza kuishawishi mahakama hiyo iwatie hatiani waomba rufaa”alidai wakili Tibanyendera.
 
Baada ya kumaliza kuwasilisha sababu hizo mbili za kukata rufaa, jaji Bongole aliarisha usikilizwaji wa rufaa hiyo hadi kesho ambapo wakili  wa waomba rufaa ataendelea kuwasilisha sabababu zake za kukata rufaa.
 
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumanne, Agosti 13 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.