Header Ads

DPP AMFUTIA KESI ALIYEDAIWA KUMTEKA DK.ULIMBOKA, AMFUNGULIA KESI MPYA

 
Na Happiness Katabazi
 
MKURUGENZI wa Mashitaka nchini(DPP), Dk.Eliezer Feleshi jana alimfutia kesi ya kujaribu kumuua na kuteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Steven Ulimboka, raia wa Kenya Joshua Mulundi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, baada ya kuona hana haja kuendelea kumshitaki kwa makosa hayo ambayo yalikuwa hayana dhamana.
 
Hati hiyo ya DPP iliyowasilishwa chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwaniaba yake na Wakili Mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka jana mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema ambapo wakili Kweka aliambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutajwa lakini upande wa jamhuri hauna nia tena ya kuendelea kumshitaki Mulundi kwa kesi hiyo.
 
Kwa upande wake Hakimu Waliarwande alikubaliana na hoja hiyo ya wakili Kweka na akamfutia kesi hiyo Mulundi ambaye yupo gerezani tangu Julai 13 mwaka jana hadi sasa kwasababu makosa ya kujaribu kuua na kumteka nyara Dk.Ulimboka hayana dhamana na ni Mahakama Kuu ndiyo ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ambayo imefutwa jana
 
Hata hivyo muda mfupi baada ya Hakimu Lema kumfutia kesi hiyo Mulundi, askari kanzu walimkamata tena Mulundi na kisha kumfikisha kwa hakimu mkazi mwingine mahakamani hapo Alocye Katemana na kisha wakili Kweka akaiambia mahakama kuwa upande wa jamhuri umemfungulia kesi mpya mshitakiwa huyo ambayo itakuwa na shitaka moja tu.
 
Wakili Kweka mbele ya Hakimu Katema alimsomea shitaka hilo mshitakiwa ambapo Julai 3 mwaka jana, katika Kituo cha Polisi Oystebay mshitakiwa huyo alitoa taarifa za uongo kwa ofisa wa polisi ambapo alimweleza ofisa huyo wa polisi yeye na wenzake ambao waliokodiwa kwenda kumteka na kumjeruhi Dk.Ulimboka jana ambalo si kweli kosa ambali ni kinyume na kifungu cha 122 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo mpya umekamilika.
 
Wakili Kweka alidai licha kosa hilo lina dhamana kwa mujibu wa sheria lakini upande wa jamhuri unaomba asipewe dhamana kwaajili ya usalama wake,kesi hiyo ina maslahi kwa taifa hoja ambayo ilimlazimu hakimu Katemana aairishe kesi hiyo kwa muda na kisha kuutaka upande wa jamhuri uende ukalete kwa maandishi hati ya kumfungia dhamana mshitakiwa huo.
Hata hivyo mshitakiwa huyo alikanusha shitaka hilo na akaomba apewe dhamana kwani ana wadhamini na kisha aliza kusema maneno yafuatayo;
“Nimesota muda mrefu gerezani wakati hata sijatenda makosa haya, na ninajua wanataka kunifungia dhamana makusudi ili waweze kunyamazisha bunge na umma usiendelee kupiga kelele kuhusu tukio la kupigwa na kuteswa kwa Dk.Ulimboka na kwa taarifa yenu mkinipeleka tena gerezani naenda kuanza mgomo …nimechoka kuonewa’alidai Mulundi.
 
Hata hivyo kesi hiyo ilivyorudi tena mchana wakili Kweka hakuweza kuja na hati ya kuzuia dhamana ya Mulundi hali iliyosababisha hakimu Katemana kutoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo ambapo alisema ili mshitakiwa huyo apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambapo mmoja awe ni mtumishi wa serikali ,yeye mwenyewe kusaini bondi ya Sh.milioni tano na mdhamini wake asaini bondi ya Sh.milioni tano, kusalimisha hati zake za kusafiria ,atatakiwa awe ana ripoti katika vyombo vya dola.
 
Hata hivyo mshitakiwa huyo jana alishindwa kutimiza masharti hayo  na Hakimu Katemana aliarisha kesi hiyo Agosti 20 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa, na Septemba 4 kwaajili ya kuja kusomewa maelezo ya awali, na akaamuru arejeshwe rumande kwasababu ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana.
 
Julai 13 mwaka 2012, Mulundi (21), alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akikabiliwa na makosa mawili, kosa la kwanza ni la kutaka kuua Dk.ulimboka na kosa la pili ni la kumteka,ambapo makosa hay ohayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana na yanasikilizwa na Mahakama Kuu peke yake na kwamba mahakama ya Kisutu ilikuwa haina mamkala ya kusikiliza kesi hiyo hiyo na hivyo kusababisha kukaa gerezani tangu siku hiyo.
 
Wakili wa serikali, Ladslaus Komanya, mbele ya Hakimu Agnes Mchome, alidai kuwa Mulundi ambaye mkazi yake ni Murang’a nchini Kenya, anadaiwa kuwa  Juni 26 mwaka jana, akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk. Ulimboka.
Katika shtaka la pili, Komanya alidai kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa Mwabepande Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha sheria, mshtakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.
 
Hakimu Mchome alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwani Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
 
Juni 27 mwaka 2012, Dk. Ulimboka aliokotwa na msamalia mwema katika msitu huo wa Mwabepande akiwa amejeruhiwa vibaya na kisha akafikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa na maumivu makali na kuanza kutibiwa na kisha kupelekwa afrika Kusini kwaajili ya matibabu zaidi na kisha kurejeshwa nchini akiwa amepona.
  
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 7 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.