ARCADO NTAGAZWA ANA KESI YA KUJIBU
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemuona aliyekuwa waziri
wa zamani ambaye kwa sasa ni Kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Arcado Ntagazwa kwa kosa moja tu la kujipatia kofia,fulana zenye
jumla ya thamani ya shilingi milioni 74.9 kwa njia ya udanganyifu ana kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa jana Hakimu Mkazi Geni Dudu ,ambaye alisema kesi
hiyo ilikuja jana kwaajili ya kutoa uamuzi wa kumuona Ntagazwa na wenzake wana
kesi ya kujibu au la na kwamba upande wa jamhuri katika kesi hiyo ili
kuthibitisha kesi yao waliweza kuleta jumla ya mashahidi wa tano.
Hakimu Dudu alisema baada ya kupitia vielelezo na ushahidi uliotolewa na
mashahidi watano wa upande wa jamhuri,mahakama yake imefikia uamuzi wa kuona
upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake na hivyo kwa kauli moja
mahakama yake inamuona Ntagazwa na washitakiwa wengine akiwemo mtoto wake wana
kesi ya kujibu na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi Agosti 2 na 5 mwaka huu, itakapokuja
kwaajili washitakiwa hao kuanza kujitetea.
Kwa upande wake Ntagazwa ambaye ni pia ni Mwanasheria kitaaluma alieleza
kuwa anakusudia kuleta mashahidi wawili wakati atakapoanza kujitetea.
Mbali na Ntagazwa washtakiwa wengine ni Senetor Mirelya (60)
na Webhale Ntagazwa ambaye ni mtoto wa Ntagazwa ambao wanatetewa na wakili wa
kujitegemea Alex Mgongolwa.
Aprili 23
mwaka jana, ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Ladslaus Komanya
mbele ya Hakimu Mkazi Liad Shamshama alidai kuwa Oktoba 22 mwaka 2009 huko
Msasani Mikoroshini washtakiwa hao kwania ovu walijipatia fulana 5000 na kofia
5000 zenye jumla ya thamani ya Shilingi milioni 74.9 toka kwa Noel Sevele kwa
makubaliano kuwa wangemlipa Sevele kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha
mwezi mmoja tangu walipochukua vifaa hivyo lakini hata hivyo walishindwa
kumlipa na washtakiwa walikana shtaka na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika.
Ntagazwa
ambaye kwa sasa ni Kada wa Chadema , kabla ya kujiunga na chama hicho miaka
minne iliyopita, akitokea chama cha Mapinduzi (CCM).Akiwa mwanachama wa CCM,
aliwahi kuteuliwa na rais wa Serikali ya awamu ya pili na ya tatu, Ally Hassan
Mwinyi na Benjamin Mkapa kushika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali
hadi ilipofika mwanzoni mwa mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete alipounda baraza
lake jipya la mawaziri na kuamuacha nje ya baraza hilo.
Ntagazwa
ambaye aliwahi kuwa mbunge wa muda mrefu wa Jimbo la Mhambwe kwa tiketi ya CCM,
hadi sasa nakumbukwa kwa msemo wake mmoja maarufu aliowahi kuutoa bungeni akiwa
Waziri Nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira alisema ‘Ipo
siku wajukuu zetu watafukua makaburi yetu wachunguze ubongo wetu kama tulikuwa
na akili timamu’. Ntagazwa alitoa msemo huo kutokana na kutoridhishwa na baadhi
ya maamuzi yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji waliopewa dhamana.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 31 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment