VIGOGO WA DECI JELA MIAKA MITATU
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewahukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya jumla ya Sh.milioni 21 vigogo wanne wa iliyokuwa kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) baada ya kuwakuta na hatia ya kutenda makosa kuendesha shughuli za kupokea amana za umma bila leseni.
Hukumu hiyo imetoelewa na hakimu mkazi Stewart Sanga na ikasomwa na Hakimu Mkazi Alocye Katemana ambaye alisema kesi hiyo ilikuwa na jumla ya washitakiwa wa tano, ambao ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye, Samwel Sifael Mtares, Arbogast Francis Kipilimba ambao walikuwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke.
Hakimu Katemana alisema washitakiwa hao ambao ni wachungaji wa makanisa ya Pentekosti ni mshitakiwa wa kwanza, wa pili,watatu, wanne ila mshitakiwa wa tano Kipilimba ameachiliwa huru baada ya mahakama kumuona hana hatia katika makosa hayo mawili ambayo wenzake wamekutwa nayo na hatia.
“Mahakama imeridhika kuwa upande wa jamhuri uliokuwa unawakilishwa na wakili wa serikali Prosper Mwangamila na Justus Mulokozi umeweza kuthibitisha kesi yao na kwa maana hiyo mahakama inawatia hatiani washitakiwa hao wannne na kumwachiria huru mshitakiwa mmoja kwasababu mashitaka dhidi yake mshitakiwa wa tano jamhuri imeshindwa kuthibitisha”alisema Hakimu Katemana.
Alisema katika kosa la kwanza kila mshitakiwa atapaswa alipe faini ya Sh.milioni tatu au kwenda jela miaka mitatu, na katika kosa la pili kila mshitakiwa atatakiwa alipe faini ya Sh.milioni 18 au kwenda jela miaka mitatu na kwamba mshitakiwa atakayeweza kulipa faini ataachiriwa huru.
Aidha hakimu Katemana alisema pamoja na adhabu hiyo pia mahakama hii imeagiza Serikali ifanye mchanganuo wa mali za DECI ambazo zinashikiliwa na serikali kwani kuna mali zilishikilia na serikali sio mali za DECI ni mali za watu wengine hivyo na fedha za wateja wa DECi walizopandwa zirejeshwe kwa wateja wenyewe ambao wateja hao wataonyesha uthibitisho wa kuonyesha kweli walipanda fedha zao katika DECI.
Kabla ya Hakimu Katemana kuwapatia adhabu hiyo ,aliwapatia nafasi mawakili wa pande zote mbili kuzungumza chochote, ambapo wakili wa serikali Mwangamila, alieleza kuwa washitakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, na kwamba makosa waliyoyatenda ya madhara katika chumi wa nchi hivyo akaomba washitakiwa wapewe adhabu kali iliwe fundisho kwa watu wengine ambao wanatamani kutenda makosa hayo na kwamba wafungwa wanaopatikana hatia ya makosa ya jinai hawapaswi kufaidika na makosa hayo na hivyo akaiomba mahakama mali zao zikamatwe na zipelekwe serikalini. .
Aidha kwa upande wa wakili washitakiwa Ndusyepo alidai kuwa washitakiwa ni mara yao ya kwanza kutenda makosa na makosa hayo waliyatenda wakati wakiwa kwenye harakati za kuwakwamua waumini wao katika lindi la umaskini na kwamba anaomba mahakama isiwapatie adhabu kali kwani wateja wake hawana huwezo wa kulipa fidia kwani wengine ni wastaafu na hawana huwezo wa kifedha.
Hadi jana saa saba ni Domick na Mtares ndiyo waliweza kulipa faini ya kila mmoja alilipa fedha taslimu sh.milioni 21 na hivyo kuachiliwa huru na hivyo washitakiwa wawili hadi jana saa tisa alasiri walishindwa kulipa faini hiyo na hivyo kupelekwa gerezani .
Juni 12 mwaka 2009 washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza baada ya vuta nikuvute kati ya viongozi na wanachama DECI. Wakili Mwangamila alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.
Alidai kuwa, kati ya mwaka 2007 na Machi 2009, katika makao makuu ya DECI, yaliyopo Mabibo Mwisho, jijini Dar es Salaam, washitakiwa waliendesha na kusimamia mradi wa upatu katika sehemu tofauti nchini kwa ahadi ya kuwapa wanachama wake fedha zaidi ambazo katika mazingira ya kibiashara ni kubwa kuliko mradi waliokuwa wakiufanya.
Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila kuwa na leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha Na.5 ya mwaka 2006 na kwamba, washitakiwa wote katika kipindi hicho, wakiwa kwenye ofisi zao za DECI, walipokea amana kutoka kwa umma bila leseni.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 20 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment