SIRI ZAANIKWA KESI YA JENGO LINALOKARIBIA IKULU
Na Happiness Katabazi
SHAHIDI wa tatu katika kesi ya matumizi mabaya ya
madaraka katika ujenzi wa jengo la ghorofa 18, lililo karibu na Ikulu, Saimon
Maembe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Manispaa ya Ilala
iliwanyima kibali washtakiwa katika kesi hiyo cha kuongeza idadi ya ghorofa
kwenye juu.
Kesi hiyo inawakabili vigogo wawili wa
Wakala wa Majengo (TBA) ambao ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA,
Makumba Togolai Kimweri na Msanifu Mkuu wa TBA, Richard John Maliyaga.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia
madaraka yao vibaya kwa kutoa kibali cha kupanua jengo hilo kwa kuongeza
ghorofa tatu zaidi kutoka 15 hadi 18, bila idhini ya mamlaka husika na bila
kufuata Sheria za mipango miji.
Jengo hilo linalomilikiwa kwa ubia kati
ya kampuni ya Royalle Orchard Inn na TBA, liko katikati ya Jiji la Dar es
Salaam, katika mtaaa wa Chimara, kitalu namba 45 na 46, karibu na Taasisi
ya Saratani Ocean Road, katika Manispaa ya Ilala.
Akitoa ushahidi wake jana Mchunguzi wa kesi hiyo toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), alidai wakati anafanya uchunguzi wake aligundua kuwa Manispaa ya Ilala ilikataa maombi ya
washtakiwa hao kujenga ghorofa 15.
Maembe alidai licha
ya kuwa Wizara ya Ujenzi kutoa waraka kwa TBA ikielekeza kuwa ni lazima
ishirikishwe katika mchakato wa uendelezaji wa viwanja vinavyomilikiwa na TBA
kwa niaba ya Serikali, hata hivyo washtakiwa hao hawakuishirikisha wizara hiyo
katika mradi huo.
Maembe aliyekuwa akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai, kutoa
ushahidi wake alieleza kuwa alianza kufanya uchunguzi wa ujenzi wa jengo hilo baada
ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa maelekezo
kwa Takukuru, na kwamba alikabidhiwa jukumu
hilo na Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru.
Alidai
wakati akifanya uchunguzi wake alikwenda
TBA ambako alipata nyaraka mbalimbali za mradi huo kama vile tangazo la zabuni
ya ubia wa ujenzi wa jengo hilo, maombi ya wazabuni na taarifa ya tathmini ya
zabuni hiyo.
Alizitaja nyaraka nyingine kuwa ni
mihtasari ya vikao na uamuzi wa Bodi ya Zabuni ya TBA, mkataba wa ujenzi wa
jengo hilo na vibali vya ujenzi, na kwamba kampuni ya Royalle Orchard Inn ndio
ilishinda zabuni hiyo na kwamba nilibaini kuwa vibali vya ujenzi vilitolewa na
TBA, jambo ambalo lilimshangaza nikuona kuwa vibali vya ujenzi vilitolewa na TBA
wenyewe, kwa sababu haikuwa kawaida kwani kuna mamlaka zinazohusika na vibali
vya ujenzi.
Maembe alidai kuwa katika makubaliano ya ubia kati ya TBA na kampuni
hiyo, walikuabaliana kujenga jengo kwa ajili ya makazi na biashara na kwamba
jengo litakuwa ni la ghorofa 15.
Alidai kuwa kibali cha kwanza kilikuwa
ni cha ujenzi wa ghorofa 15 na cha pili kikiwa ni cha upanuzi wa mradi kutoka
ghorofa 15 hadi 18 na kwamba vyote vilitolewa na kusainiwa na mshtakiwa wa
pili, Maliyaga.
Shahidi huyo alidai kuwa baadaye
alikwenda Manispaa ya Ilala ambayo kwa mujibu wa Sheria namba 8 ya
Mipango Miji ya mwaka 2007 ndio yenye mamlaka ya kutoa vibali, ili kuona kama
walihusika kutoa vibali vya ujenzi huo.
“Kiongozi wa Idara ya Mipango Miji
alieleza kuwa waliwahi (washtakiwa) kupeleka maombi ya kibali cha kujenga
ghorofa 15 lakini wakayakataa, kwa sababu hayakuendena na ramani ya mchoro wa
eneo husika.”
Maembe alidai baadaye alikwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi ambayo ndio yenye uamuzi wa mwisho ya matumizi ya ardhi, na
kwamba katika Idara ya Mipango Miji alipata ramani ya eneo husika ya mwaka
2000.
“Maelekezo ya ramani yalikuwa wazi,
kwanza ni kuwa matumizi ya ardhi katika eneo husika ni makazi tu na mbili
majengo katika eneo hilo ni ya ghorofa tatu hadi sita. Kwa hiyo niligundua kuwa
kilichofanyika katika ujenzi huo kilikuwa kinyume cha sheria.”, alidai shahidi
huyo.
Hata hivyo alidai kuwa alipowauliza
wizara kama waliwahi kutoa mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika eneo husika,
walikataa kuwa hawajawahi kupata mnaombi kama hayo.
Katika ushahidi wake shahidi huyo
alidai kuwa wakati akichambua nyaraka alizozikusanya, alipata waraka kutoka
Wizara ya Ujenzi, ambako TBA iko chini yake, ukiielekeza TBA kuishirikisha
katika mchakato wa uendelezaji wa miradi ya viwanja inavyovimiliki.
Hata hivyo shahidi huyo alidai kuwa
alipokwenda Wizara ya Ujenzi kuona jinsi walivyoshirikishwa, Katibu Mkuu wa
wizara hiyo alisema TBA haikuwahi kuwashirikisha katika mradi huo.
Pia shahidi huyo alidai kuwa kwa mujibu
wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, taasisi yoyote ya umma inapotaka kuingia katika
ubia na sekta binafsi katia mradi, lazima ifanye upembuzi yakinifu, ili kubaini
changamoto, gharama, faida, wadau na namna ya kutatua changamoto za mradi na
kwamba hata hivyo TBA haikufanya upembuzi yakinifu katika mradi huo na kwamba.
Alisisitiza licha ya ukiukwaji huo wa
sheria katika ujenzi huo, washatakiwa walikuwa na ufahamu wa taratibu
zilizopaswa kufuatwa kwani kulikuwa na dokezo kutoka mshatakiwa wa pili kwenda
kwa mshtakiwa wa kwanza.
Katika dokezo hilo lililosomwa
mahakamani hapo mshtakiwa wa pili alikuwa akieleza kuwa amefanya mawasiliano na
Manispaa ya Ilala, lakini imesisitiza kuwa eneo hilo ni la makazi na
linahitajika ghorofa tatu hadi sita tu.
Alidai kuwa baada ya uchunguzi huo
aliwahoji washtakiwa kutokana na tuhuma hizo ambapo walikiri, katika maelezo
yao ya onyo, ambayo aliomba mahakama iyapokee kama kielelezo cha ushahidi.
Hata hivyo upande wa utetezi ukiongozwa
na Wakili Majura Magafu, ulipinga kupokewa kwa maelezo hayo na Hakimu Sundi
Fimbo aliamuru kesi hiyo ya msingi isimame ili kuendesha kesi ndogo (Trial
within a trial) kuona uhalali wa maelezo hayo ya onyo ya washtakiwa na hakimu
huyo akaiarisha kesi hiyo hiyo hadi Septemba 5 mwaka huu, itakapokuja kwaajili
ya mahakama kuanza kuisikiliza kesi hiyo ndogo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 29 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment