Header Ads

9 KORTINI KWA UNYANG'ANYI WA KUTUMIA SILAHA

Na Happiness Katabazi

WATU tisa akiwamo mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 75826 Koplo Julius Kwayu (32), jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Washitakiwa hao walifikishwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi wa kikosi cha kupambana na ujambazi kutoka polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, huku askari hao wakiwa wamebeba silaha. Washitakiwa hao walisomewa mashitaka kwa mahakimu tofauti.

Mbele ya Hakimu Michael Mteite, Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, alidai mbali na askari huyo wa JWTZ ambaye ni mfanyakazi wa jeshi hilo Mkoa wa Arusha, wengine ni Novati Meria maarufu kwa jina la Moshiro (29) na Shaban Rashid (35) ambao ni wafanyabiashara.

Alidai Julai 22 mwaka huu, saa saba usiku huko Ubungo Msewe, washitakiwa waliiba vocha za muda wa maongezi za sh 1,000,000, fedha taslimu 700,000, simu moja ya mkononi aina ya Nokia yenye thamani ya sh 1,000,000, vyote vikiwa na thamani ya sh 3,200,000, mali ya Frank Lema na kwamba kabla ya kupora vitu hivyo walifyatua risasi mbili hewani.

Aidha, mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga, wakili wa serikali, Leonard Chalo, aliwataja washitakiwa sita ambao ni Peter Juma, Julias Mwita, Julias Michael, Julias Chacha, Ester Samson na Catherine Juma wanaokabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Chalo alidai Julai 20 mwaka huu, saa saba usiku katika eneo la Kibamba Shule, washitakiwa waliiba simu mbalimbali zenye thamani ya sh milioni nne, maboksi mawili ya sigara aina Sportsman za sh milioni 1.4 na fedha taslimu sh 500,000, vyote vikiwa na thamani ya sh 5,910,000, mali ya Gradius George na kuwa kabla ya unyang’anyi huo walifyatua risasi tatu hewani.

Washitakiwa walikana tuhuma hizo na kurudishwa rumande kwa kuwa kesi hizo hazina dhamana. Kesi itatajwa Agosti 11.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Agosti 6,2009

No comments:

Powered by Blogger.