Header Ads

KESI YA MEREY BALHBAHOU YAKWAMA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya wizi wa dola za Marekani milioni 1.08 (sawa na sh bilioni 2.4), kwa njia ya mtandao wa kompyuta, mali ya Benki ya Barclays, inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Dar es Salaam, Cement Muslim na mfanyabiashara maarufu wa mafuta nchini, Merey Ally Saleh (41), maarufu kwa jina la Merey Balhbahou na wafanyakazi saba wa benki hiyo, umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.


Mwendesha Mashitaka, Inspekta Francis Mboya, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Euphemia Mingi, aliiambia mahakama kuwa upelelezi haujakamilika kwa sababu wanasubiri vielelezo kutoka Barclays pia kuna vielelezo walivipeleka katika kitengo cha utambuzi wa maandishi kilichopo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, ambavyo havijarejea.

Hakimu Mingi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 15 mwaka huu. Mbali na Balhbahou, washitakiwa wengine ni Meneja Mwendeshaji wa Kigamboni Oil Co. Ltd, Abdallah Said Abdallah (48), Winford Mwang’onda, Shubira Mutungi, Naima Saria, Upendo Mushi, Magreth Longway, Emmanuel Mukoni na Ramadhani Khamis.

Wakati huo huo, mfanyabiashara mwingine maarufu wa madini, Justice Rugaibura (36), mkazi wa Msasani Beach jijini, anayekabiliwa na kesi ya wizi wa kiasi hicho cha fedha katika benki hiyo ya Barclays, kwa njia ya mtandao, jana tena alishindwa kutokea mahakamani, kwa kile kilichodaiwa na mdhamini wake kuwa ni mgonjwa.

Mwendesha Mashitaka, Francis Mboya, mbele ya Hakimu Mingi alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini mdhamini wa mshitakiwa huyo, amewasilisha cheti kinachoonyesha kimetolewa na Hospitali ya Aga Khan, kinachosema mshitakiwa huyo ni mgonjwa.

Hata hivyo, Inspekta Mboya aliomba mahakama impe nafasi ya kuchunguza cheti hicho kama kweli kimetolewa na hospitali hiyo na baadaye Mingi alikubaliana na ombi la mwendesha mashitaka huyo na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho.

Mapema Machi mwaka huu, Mwendesha Mashitaka, Inspekta Emma Mkonyi, alidai kuwa, mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka ya kula njama kwa nia ya kudanganya.
Ilidaiwa kuwa Oktoba 29-30 mwaka jana, katika eneo lisilofahamika jijini Dar es Salaam, kwa kutumia ujanja, mtuhumiwa alifanya udanganyifu na kuibia benki hiyo dola za Marekani 1,081,263.00.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Agosti 11,2009

No comments:

Powered by Blogger.