Header Ads

MAHAKAMA YAZIDI KUMCHELEWESHA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania, Amatus Liyumba, umedai kuwa mahakama nchini inawatenda vibaya.


Malalamiko hayo yalitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu mkazi, Aloyce Katemana, na kiongozi jopo la mawakili wa mshitakiwa, Majura Magafu aliyekuwa akisaidiwa na Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke.

Mawakili hao walilalamika mara baada ya hakimu kusema kuwa, kesi hiyo haitoweza kusikilizwa kama ilivyopangwa kwa sababu, uongozi wa mahakama haujapanga jopo la mahakimu wa kuisikiliza.

Wakati hakimu huyo akisema hayo, wakili kiongozi wa serikali, Justus Mulokozi aliambia mahakama kuwa, wapo tayari kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa.

Wakili upande wa utetezi, Magafu aliomba mahakama hiyo itoe maelezo kadhaa yakiwemo ya kesi hiyo kuchelewesha kinyume na kifungu namba 225 (4,5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002, kuweka bayana kwamba, ndani ya siku 60, upelelezi wa kesi uwe umekamilika na kuanza kusikilizwa.

Kwa mujibu wa Magafu, endapo siku hizo zitakuwa zimepita, kesi hiyo inatakiwa ufutwe.

“Upande wa mashtaka umefanya kazi yao na ukakamilisha upelelezi wao na mahakama hii Juni 28, mwaka huu, iliipanga leo (jana) kwamba kesi hii inakuja kwa ajili ya mshitakiwa kusomewa maelezo ya awali….sasa tunashindwa kuelewa kwanini mahakama inashindwa kusikiliza kesi hii?” alihoji Magafu kwa sauti ya ukali.

Aliendelea kudai katika kesi hiyo hivi sasa mahakama ndiyo inavunja sheria kwa kushindwa kupanga jopo la kuisikiliza kesi hiyo ambayo siku 60 zimepita na haijaanza kusikilizwa.

Aliongeza kuwa, hali hiyo imekuwa aibu kwa mahakama kwani kipindi cha nyuma, upande wa mashitaka ndiyo uliokuwa ukilalamikiwa kwa kuchelewa kukamilisha upelelezi lakini hivi sasa mahakama imeanza kuwa kikwazo cha kupanga majopo ya kusikilizwa kwa kesi.

“Sasa sisi upande wa utetezi tunasema mahakama inatutenda vibaya na tunaomba ifikapo Ijumaa wiki hii, jopo liwe limeshaandaliwa kwani mahakimu wapo wengi na siyo lazima mahakimu watakaopangwa kuendesha kesi hizi watoke ng’ambo,” alidai Magafu.

Baada ya Magafu kumaliza kutoa madai hayo, Hakimu Katemana aliahirisha kesi hiyo hadi mchana ambapo alivyorudi, alitoa uamuzi wake na kusema Magafu amejichanganya wakati akiwasilisha hoja zake kwani kifungu alichokitumia hakihusu mahakama bali kinahusu upande wa mashitaka.

Katemana alisema, uongozi wa mahakama unaendelea kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kuakikisha jopo la mahakimu wa kusikiliza kesi hiyo wanapatikana hivyo akaairisha kesi hiyo hadi Agosti 25, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya Liyumba kusomewa maelezo ya awali.

Julai 28, mwaka huu, wakili kiongozi wa serikali, Mulukozi aliambia mahakama hiyo kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na mahakama hiyo ilipanga jana kesi hiyo isiskilizwe.

“Sisi upande wa utetezi ni rai yetu kwamba matakwa ya kifungu hicho hayajatimizwa na upande wa mashitaka kwa kuwa kesi hii ilifunguliwa Mei 28, mwaka huu, hadi leo (jana) siku 60 ziliisha juzi na hakuna hati ya kuomba kuongezewa muda…hivyo tulitarajia leo wenzetu wangemsomea mteja wetu maelezo ya awali lakini wameshindwa kufanya hivyo,” alidai Magafu.

“Sisi upande wa utetezi ni rai yetu kwamba matakwa ya kifungu hicho hayajatimizwa na upande wa mashitaka kwakuwa kesi hii ilifunguliwa Mei 28 mwaka huu, hadi leo(jana) siku 60 ziliisha juzi na hakuna hati ya kuomba kuongezewa muda…hivyo tulitarajia leo wenzetu wangemsomea mteja wetu maelezo ya awali lakini wameshindwa kufanya hivyo.

“Mheshimiwa hakimu sheria za nchi zimetungwa kwaajili ya watu wote wapate haki na taratibu zilizoainishwa kwenye sheria hizo zifuatwe sasa zisipofuatwa ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi pia kwani katiba inasema kila mtu ana haki ya kusilizwa…hivyo mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni mjeta wetu yupo mahabusu kwasababu ambazo serikali inazijua na sisi upande wa utetezi tunazijua, basi tunaomba mahakama imwachie.” alidai Magafu.

Mei 28, mwaka huu, Mulokozi alidai mahakamani hapo kuwa Liyumba anakabiliwa na makosa mawili ya jinai katika kesi hiyo Na.105/2009 kwa matumizi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa, kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu (BOT).

Aidha, anadaiwa kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha kosa linaloangukia kwenye shitaka la kwanza.

Liyumba alisomewa mashitaka mapya Mei 28 mwaka huu, baada ya Mei 27 mwaka huu, Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba yake 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina dosari za kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 12,2009

No comments:

Powered by Blogger.