Header Ads

HIVI DK.MAHANGA NI MZIMA?

Na Happiness Katabazi

‘MNAFKI akisema anasema uongo, akiahidi hatimizi na ukimwamini anakufanyia hiyana’. Maneno hayo yanapatikana kwenye kwenye ‘Surat Munafiquun’ katika kitabu cha Hadithi za Mtume Mohamad.


Kwa wale wanaofuatulia matamshi ya wanasiasa wetu, watakubaliana nami kwamba maneno hayo yamekuwa yakitumiwa mara kwa mara na mwanasiasa machachari wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini, na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, wanapohutubia kwenye mikutano yao ya kisiasa majukwani.

Nimelazimika kutumia nukuu hiyo ya maneno kutoka kwenye kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislamu katika makala hii, kwa sababu mada nitakayoizungumzia leo inanipa fursa ya kuitumia nukuu hiyo.

Katika makala hii nitachambua hoja zilizotolewa na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk. Milton Makongoro Mahanga, iliyotaka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaopinga ufisadi hadharani watoswe kwa madai kwamba wanakivuruga chama hicho tawala.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa baadhi ya vyombo vya habari, Dk. Mahanga alisema wabunge na wana-CCM wengine wanaotoa tuhuma zisizo na ushahidi kwamba ndani ya chama hicho kuna mafisadi, wanahatarisha uhai na ushindi wa chama katika chaguzi zijazo.

Kwa mujibu wa Dk. Mahanga: “Hivi hata kama leo nchi hii ikiamua kwamba hawa wanasiasa wachache mafisadi wa kufikirika watoswe baharini au wafungwe maisha, je, CCM sasa itapona au ndiyo itakuwa mwisho wa vitendo vya rushwa na ubadhirifu nchini mwetu? Mimi nasema hapana.

Kinachotakiwa ushindi wa CCM si hao mafisadi wa kufikirika au wa kubuni ndani ya CCM kama wapambanaji, ndizo zitakazokiharibia chama kwani wananchi wasioelewa malengo yao halisi, wanaweza kuamini kwamba kweli chama hiki kimejaa mafisadi na kukinyima kura”.

Kama kweli kauli hiyo imetolewa na msomi Makongoro Mahanga, basi nashawishika kuamini kuwa kiongozi huyu ana matatizo ambayo kwa hakika yatampa matatizo siku za usoni katika medani ya siasa.

Kwanza kabisa kimsingi tukubaliane kwamba lengo la chama chochote cha siasa kokote duniani, ni kukamata dola. Lakini lengo hilo lazima lishabihiane na uadilifu ndani ya chama hicho na wanachama wake na si vinginevyo, sasa kauli hiyo ya Dk. Mahanga imedhihirisha wazi kwamba tuhuma za ufisadi zinazowakabili baadhi ya wanachama wa CCM zifunikwe, zisijadiliwe, na vyombo vyenye mamlaka ya kuchunguza tuhuma hizo ziache kufanya kazi ya kuchunguza tuhuma eti kwa sababu ni hofu ya CCM kunyimwa kura. Hii ni ajabu na kichekesho.

Hebu tumuulize Dk. Makongoro, kauli yake hiyo ilikuwa na lengo la kukinusuru kweli chama chake kisinyimwe kura au yeye ameanza maandalizi ya kutetea kiti chake cha ubunge Jimbo la Ukonga?

Ninachokiona hivi sasa ndani ya CCM ni kuwa kila mtu amegeuka kuwa ‘msemaji’, kwani kila kukicha kila mbunge, waziri au makada wakongwe hutoa msimamo unaohusu chama hicho. Kibaya zaidi kauli zinazotolewa hupingana kiasi cha kuwafanya wananchi wasijue wachukue la nani na waliache la nani.

Leo ndani ya chama hicho kikongwe, kuna tuhuma nyingi zinazowakabili wanachama wake, kiasi cha kukipaka matope na baadhi ya wanachama wakitaka wenzao wanaokichafua wawajibishwe, lakini kuna viongozi wengine wanasema chama hakina mafisadi na wala hakijawatuma wanachama wake wafanye ufisadi, viongozi hao wanakwenda mbali zaidi kwa kudai hizo ni tuhuma na si vizuri kuwahukumu watu kwa kuzifuata.

Ukiona chama au taasisi yoyote imefikia hatua hii ya kila mtu anageuka kuwa ni msemaji, ujue wazi hali si shwari ndani ya chama hicho na hata aliyepewa dhamana ya kuwa msemaji wa chama hicho ni dhahiri haaminiki au hafanyi kazi yake ipasavyo.

Ndiyo maana kila mwanachama anaamua kubwabwaja anavyoweza na hatimaye wanaishia kuwekeana chuki na kukishusha hadhi chama hicho.

Mapema wiki hii Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, amekaririwa kuwa wabunge wanaoandamwa na tuhuma za ufisadi kuwa watakuwa na wakati mgumu, kwani chama hicho kimeweka taratibu za kuwabana, lakini Dk. Mahanga anaueleza umma kuwa ndani ya CCM kuna mafisadi wa kufikirika - kwa tafsiri nyepesi hawapo - lakini akajichang’anya aliposema wapo lakini hawazidi wanne.

Alipotakiwa awataje akashindwa lakini tukumbuke kuwa katiba ya chama hicho inamtaka mwanachama kusema ukweli daima na fitina mwiko. Tukumbuke kiongozi huyo aliahidi kuitumikia katiba hiyo!

Lakini cha ajabu amekuwa mwoga, hataki kusema ukweli, amekuwa mnafiki kwa kukataa kuwa kuna mafisadi wa kufikirika CCM wakati yeye na nafsi yake anatambua wazi pamoja na mazuri iliyokifanya chama hicho na kuwapo kwa viongozi waadilifu na wachapakazi, bado kina viongozi wasio na uadilifu na walio legelege.

Dk. Mahanga ameshindwa kutimiza ahadi ya kusema kweli daima fitina kwake mwiko ambayo hiyo ni ahadi ya mwana-CCM, ambaye Watanzania walimuamini wakampa uongozi amewatendea hiyana.

Tumewashuhudia viongozi wa aina ya kina Mahanga wanaosema uongo mweupe kwa kuwa hivi sasa wana madaraka, lakini wanapokosa madaraka hayo huwa ni mahiri wa kutafuta vyombo vya habari na kuanza kueleza tuhuma nyingi zilizopo ndani ya chama hicho.

Wakati mwingine tuhuma anazozitoa wakati hayupo madarakani zilitendeka wakati yeye akiwa na nyadhifa, ila alishindwa kutimiza ‘ahadi ya chama chake inayomtaka ya kusema ukweli daima fitina kwake mwiko,’ kwa kuwa alikuwa akilinda kitumbua chake kisiingie mchanga.

Ni rai yangu kwa wananchi wenzangu waliomo kwenye ulingo wa siasa au kwenye taasisi za umma, waanze kujenga utamaduni wa kusema ukweli hata kama utawagharimu ili tuweze kujenga nchini yetu, kwani utatetea maovu lakini kumbuka utetezi huo wa maovu utasababisha taifa ambalo lina ndugu zenu kuangamia au kuishi maisha ya tabu kwa ajili ya kukumbatia ufisadi.

Mungu ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Agosti 16,2009

No comments:

Powered by Blogger.