Header Ads

KESI YA DECI:MAHAKAMA YAMSHAURI DPP KUONDOA KIAPO

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilimshauri Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP)Eliezer Feleshi, kuangalia upya sababu ailizozianisha katika kiapo chake chake cha kuzuia dhamana katika kesi inayowakabili vigogo wa Taasisi ya Entrepreneurship for Community Initiative (DECI).

Ushauri wa bure ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema wakati akitoa uamuzi kuhusu malumbano ya hoja yaliyowasilishwa hivi karibuni na pande mbili ambapo wakili wa utetezi Hudson Ndusuepo aliomba hati hiyo iondolewe mahakamani kwasababu hali ya usalama imetengamaa wakati wakili Kiongozi wa Serikali Justus Mulokozi alisisitiza kiapo hicho kiendelee kuwepo kwakuwa iliwasilishwa na DPP na kwamba anayepaswa kuindoa ni DPP mwenyewe.

Lema akisoma uamuzi wake alisema yeye hataki kupingana na uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa Juni 17 mwaka huu, na Hakimu Mkuu Mfawidhi mstaafu, Addy Lyamuya ambaye sipo hiyo aliipokea kiapo cha DPP na akasema kuwa kufuatia kuwasilisha kwa hati hiyo mahakama yake imefungwa mikono hivyo haiwezi kutoa dhamana kwa washitakiwa hao.Sababu za kuzuiwa kwa dhamana ni kwaajili ya usalama wa washitakiwa na maslahi ya Jamhuri.

“Ieleweke wazi kwamba mahakama hii haipo kwaajili ya kuhoji kiapo hicho na inaamini DPP atatumia kiapo hicho kwa matakwa ya sheria na si utashi wake hivyo mahakama hii inaiachia ofisi ya DPP iangalie zile sababu zilizoainishwa kwenye kiapo kama bado zipo hadi sasa, vinginevyo washitakiwa wanahaki ya kupata dhamana na ninaairisha kesi hii hadi Agosti 12 mwaka huu.”alisema Lema huku akionyesha kujiamini.

Hata hivyo Kiongozi wa Serikali Justus Mulokozi aliambia mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Jackson Mtares Dominic Kisendi, Timotheo ole Loitgimnye, Samwel Mtares, Arbogast Kipilimba na Samwel Mtalis ambao wote wanaendelea kusota rumande.

Juni 12 mwaka huu, Wakili Kiongozi wa Serikali Justus Mlokozi alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na mashitaka mawili, shitaka la kwanza ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1)(3)cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu , na shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha Na.5 ya 2006.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,Julai 29,2009

No comments:

Powered by Blogger.