Header Ads

ZOMBE ASHINDA KESI

*Jaji Massati awaachia washitakiwa wengine
*Asema serikali imeshindwa kuthibitisha kesi
*Aagiza polisi kuwasaka waliofanya mauaji hayo
*Wananchi washangaa, wadai haki haijatendeka

Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilitoa hukumu ya kushtusha baada ya kumwaachilia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.


Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa sita, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, amebaini kuwa serikali imeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo.

“Katika kesi hii upande wa mashitaka licha ya kuleta mashahidi 37 na vielelezo 23, umeshindwa kuithibitishia mahakama kuwa ni kweli washitakiwa wote ndio waliowaua marehemu na kwa sababu hiyo nawaachia huru washitakiwa wote.

“Na kwa kuwa mahakama hii imewaona washitakiwa si wauaji, hivyo kuanzia sasa naliagiza Jeshi la Polisi liende kuwasaka wauaji wa marehemu wale, na Zombe na wenzake waachiliwe huru,” alisema Jaji Massati na kuuacha umati wa watu ukiwa umeshangaa.

Jaji Massati, alisema kamwe mahakama haiwezi kumhukumu mshitakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo, kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria.

“Mahakama haipo kwa ajili ya kuonea mtu kwa kumhukumu kwa ushahidi wa kusikia, ambao haukubaliki kisheria,” alisema Jaji Massati huku akionekana kujiamini.

Baada ya Jaji Massati kutamka kuwaachia huru washtakiwa hao, Zombe na Christopher Bageni (aliyekuwa mshitakiwa wa pili) walikumbatiana kizimbani kwa furaha na wananchi waliokuwa wamefurika katika ukumbi namba moja mahakamani hapo wakionekana kushangilia na wengine kuhuzunika.

Baada ya Jaji Massati kutoka mahakamani hapo, Zombe na wenzake walitolewa kwa mlango wa nyuma huku wakiongozwa na wanausalama.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinaeleza kuwa baada ya Zombe na wenzake kutolewa mahakamani hapo, walipelekwa Kituo cha Polisi Kati na baada ya muda kila mmoja aliondoka.

Habari hizo zinaeleza kuwa kuanzia leo, Zombe na wenzake wanaweza kwenda gereza la Keko kuchukua vifaa vyao.

Awali, akiuchambua ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, Jaji Massati, alisema ushahidi wa upande wa mashtaka ni dhahifu na ulijikita katika ushahidi wa kusikia.
Alisema kati ya mashahidi waliofika mahakamani hapo, hakuna hata mmoja aliyeiambia mahakama kwamba alikuwa eneo la Msitu wa Pande na kushuhudia washitakiwa hao wakiwaua marehemu hao.

Jaji Massati alisema hoja ya upande wa mashitaka kwamba hatua ya Zombe kwenda Kituo cha Polisi Urafiki Januari 14, 2006 ilidhiirisha kwamba alikuwa akijua nini kilikuwa kikiendelea kuhusu mauaji hayo, haina nguvu kwani kwa mujibu wa Police General Order (PGO), inampa mamlaka Mkuu wa Upelelezi (RCO) kufika eneo lolote pindi litokeapo tukio la uhalifu, hivyo akasema mshitakiwa huyo alikwenda kituoni hapo kwa mujibu wa sheria za Jeshi la Polisi.

Akipangua hoja kwamba Zombe alitoa mkono wa pongezi kwa baadhi ya washitakiwa wenzake, Jaji huyo alisema kwa mujibu wa PGO pia inamruhumu kiongozi wa Jeshi la Polisi kutoa zawadi au mkono wa pongezi kwa askari wake wa chini pindi apatapo taarifa kuwa wamefanya vizuri.

Hata hivyo, alisema licha ya baadhi ya washitakiwa kudai kuwa walipongezwa na Zombe, upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kama ni kweli alitoa mkono wa pongezi.

Akimzungumzia mshitakiwa wa 12, Rajabu Bakari, alisema pamoja na kwamba katika utetezi wake alikiri kwenda Msitu wa Pande na kueleza kuwa alimshuhudia mshitakiwa wa 14, Saad (hajakamatwa hadi sasa) kuwa ndiye aliyewaua marehemu hao kwa risasi, Jaji Massati alisema utetezi huo hauna msingi wowote kwa kuwa mshitakiwa huyo hajakamatwa.

“Ushahidi wa Bakari hauna msingi wowote kwa sababu alimtaja Saad ambaye hayupo mbele ya mahakama hii, na mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa mtu ambaye bado hajafikishwa mahakamani,” alisema Jaji Massati.

Pamoja na hayo, Jaji Massati alisema hakubaliani na hoja za upande wa mashitaka iliyowahi kutolewa na wakili Mgaya Mtaki, kwamba mahakama hiyo imwone Zombe na Festus Gwasabi kuwa wana hatia ya mauaji, na endapo mahakama haitawaona na hatia katika mashitaka hayo, basi iwatie hatiani na kosa la kujua tukio hilo.

Alisema kimsingi washitakiwa hao walishitakiwa kwa kesi ya mauaji, hivyo si kazi ya mahakama kubadilisha hati ya mashitaka na kuwashitaki kwa kosa jipya.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, maelfu ya wananchi walianza kumiminika katika viwanja ya mahakama hiyo kuanzia saa 12 asubuhi, ili kushuhudia Zombe na wenzake watakapofika mahakamani hapo.

Zombe na wenzake waliwasili mahakamani hapo, majira ya saa 2:30 asubuhi wakiwa kwenye basi la mahabusu na kusindikizwa na magari madogo aina ya Land Cruiser STK 4479 na STK 4478, yaliyokuwa na askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza waliokuwa na silaha nzito.

Ndani ya Mahakama Kuu

Kutokana na umati mkubwa wa wananchi waliomiminika kusikiliza kesi hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Lameck Mlacha, alitaka watu wasijae mahakamani hapo kwani vitafungwa vipaza sauti ukumbini hapo na kwenye varanda za mahakama hiyo.
Hata kabla ya kuanza kusomwa kwa hukumu hiyo, watu walionekana kuchoka kutokana na kufika mahakamani hapo muda mrefu.

Kijana akamatwa mlangoni kwa Jaji

Katika tukio lisilo la kawaida majira ya saa 5:20 asubuhi, kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Fabric Msami (20), alikamatwa na Jeshi la Polisi, akiwa amejiegesha kwenye uchochoro mdogo ambao Jaji anapitia kuingia na kutoka mahakamani.

Kijana huyo, aliyekuwa na kitambulisho cha Shule ya Sekondari Jitegemee ya jijini Dar es Salaam, ambacho kilimalizika muda wake mwaka 2007, aliwaeleza polisi katika mahojiano kuwa alikuwa ametumwa na askari polisi ambaye hakumtaja kwa jina.

Bila kueleza alikotokea, alipozidi kuulizwa hakuweza kueleza lengo la kujibanza katika mlango huo ambao hauruhusiwi kuingilia mtu yeyote au kusimama, na sababu za kuwepo mahali hapo zaidi ya kueleza kuwa alikuwa ametumwa na askari.

Askari polisi walimkabidhi kijana huyo mahabusu ndogo ya mahakama, ambapo baadaye haikujulikana alikopelekwa baada ya kuchukuliwa maelezo.

Ulinzi waimarishwa kila kona

Askari polisi, askari kanzu, na wale wa usalama wa taifa zaidi ya 200, walifurika mahakamani hapo kwa lengo la kuimarisha ulinzi wakati hukumu ya kesi ikisomwa.
Askari hao, waliokuwa wamechanganyika na maofisa wa majeshi hayo hususani wale wenye vyeo vya warakibu na wakaguzi wasaidizi, walionekana wakizunguka kila kona ya jengo la mahakama wakiwa na redio za mawasiliano.

Mbali na askari hao wa vyeo vya juu kufurika katika mahakama hiyo, askari wengine wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), waliokuwa kwenye magari sita aina ya Land Rover, wenye silaha nzito na mabomu ya machozi, mbwa na gari la maji ya kuwasha, walionekana wakiwa umbali wa mita 30, kutoka jengo la mahakama.

Mbali na polisi, askari wa Jeshi la Magereza, nao jana walionekana wamevalia kininja, wakiwa wametanda ndani ya uzio wa mahakama hiyo wakiwa na silaha.

Taarifa ambazo zilipatikana kutoka kwa vyanzo vya kuaminika ndani ya Jeshi la Polisi, zilieleza kuwa amri ya kuwepo kwa askari polisi wengi mahakamani hapo ilitoka makao makuu ya jeshi hilo tangu asubuhi, kwamba uongozi wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, udhibiti wananchi kusogelea lango la Mahakama Kuu.

Hukumu inatolewa

Mara baada ya Jaji Massati kumaliza kusoma hukumu, nyuso za watu wengi waliokuwapo eneo la mahakama zilibadilika na baadahi yao kuanza kukimbia huko na huko. Wengine wakishuka ngazi kwa kuhofia vurugu, wengine wakipiga makelele kuwa hakuna haki iliyotendeka.

“Hawana kosa! Hawana kosa! Wameachiwa wote!’’ ni sauti za mikato zilizokuwa zikisikika kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwapo mahakamani hapo huku wakielekea kutoka nje ya mahakama hiyo.

Katika ngazi za jengo la Mahakama Kuu, kutoka ghorofa ya kwanza, ambako hukumu ilikuwa ikisomwa, ndugu wa Zombe waliokuwa wamekaa katika viti vya mapokezi, walipopata taarifa, walianguka chini na kuzimia, huku baadhi ya watoto ambao hawakufahamika wametoka wapi walionekana wakilia na wengine wakiruka ruka kushangilia.

Wakati huo, wananchi wengi walioonekana wenye hasira, walianza kupiga kelele na kuziba lengo la mahakama wakitaka Zombe atolewe nje, ili wamshambulie kwa mawe, kitendo kilichofanya askari kanzu kuzingira lango hilo na kudai kuwa hatatolewa hadi wananchi wote watakapoondoka eneo hilo.

Huku magari ya askari kanzu yasiyo na namba za polisi yakiwa yamezingira lango la mahakama, ghafla saa 9:47 adhuhuri, Zombe na wenzake walipakizwa katika gari ndogo aina ya RV4 ya rangi ya fedha, kwa mlango wa nyuma huku wakisindikizwa na askari zaidi ya 20, wenye silaha waliokuwa kwenye magari maalumu yaliyokuwa yakipiga ving’ora vya tahadhari.

Wakati Zombe na wenzake wakiondolewa kwa kasi katika eneo hilo, wananchi wengi walikuwa wakipiga kelele na kuyafukuza magari hayo kwa nyuma, wakitukana na kutoa maneno hovyo wakidai kuwa hakuna haki.

Wakili wa Zombe anena

Wakili wa kujitegemea, aliyekuwa upande wa utetezi, Gaudiosus Ishengoma, alisema ushahidi wa kosa la jinai ni tofauti na watu wanavyotarajia, kwani hakukuwepo na ushahidi wa moja kwa moja, kati ya ule wa mahakama na polisi, kwani hawakuweza kuwasilisha ushahidi wa mauaji.

“Polisi haikuweza kuleta ushahidi wa moja kwa moja juu ya mauaji, haikutoa vielelezo ni nani aliyeua, sasa sheria imeshachukua mkondo wake, afadhali kuachia watu 100, kuliko kumtia hatihani mtu mmoja asiye na hatia,” alisema Ishengoma
Alisema serikali inalo jukumu la kufikiri kama inakata rufaa, ifanye hivyo ndani ya muda iliyopewa ambao kisheria ni siku 14, baada ya hukumu kutolewa.

Akizungumzia suala la Zombe na wenzake kudai fidia kwa kushitakiwa kwa ma
kosa ambayo si ya kwao, Ishengoma, alisema wanayo haki ya kufanya hivyo wakitaka, na kama wataona kama wanahitaji kulipwa fidia kutokana na kupotezewa muda na kuchafuliwa majina yao.

Mwanasheria huyo, alibainisha anayetakiwa kulipa fidia kama Zombe na wenzake watakwenda mahakamani ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani ndiye aliyeunda tume ya kuchunguza tukio hilo na kuwafikisha mahakamani na si familia ya marehemu waliouawa.

“Mtu anayeachiwa na mahakama kwa kutokuwa na kosa, hasa kwa kesi kama hii, anamshitaki aliyempeleka polisi na kusababisha kupandishwa mahakamani. Hapa ni rais ambaye aliunda tume ya kuwachunguza na baadaye kuwapelekea polisi taarifa ambapo waliwakamata watuhumiwa hao,” aliongeza.

Wakili wa Serikali, Kaishozi, alisema katika kesi hiyo Jaji ndiye aliyekuwa na maamuzi ya mwisho, ila wataenda kukaa na kuangalia kama watarudi mahakamani kukata rufaa au la.

Wananchi walalamika

Umati wa wananchi uliokuwa umefurika nje ya mahakama, ulianza kutoa maoni yao, wengi wao wakionekana kuilaumu mahakama kwa kutoa hukumu hiyo.
“Wazee wa baraza walishasema kuwa anayo hatia, leo mahakama inasema hawajaua, sisi raia tunajiuliza haki ipo wapi? Tunaiomba serikali kukata rufaa la sivyo serikali imeshindwa kazi, na hatuitaki tena,” alisema Ramadhan Abdallah, huku akishangiliwa na mamia ya wananchi wenzake.

Pia baadhi ya wananchi walionekana kukerwa na kitendo cha washitakiwa hao kuachiwa huru na kupewa ulinzi wa polisi wa kuwatoa mahakamani na ving’ora wakati mwananchi masikini hapewi ulinzi wala msaada hata wa kumpeleka hospitali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 18,2009

No comments:

Powered by Blogger.