Header Ads

ZOMBE KUFA,KUPONA LEO

*Jaji Massati kusoma hukumu hiyo
*Wazee wa baraza walimtoa hatiani
*Wadai hakukuwa na ushahidi wa kuhusika
* Jaji alionya maoni yasiangalie magazeti
*Washitakiwa wengine wanane roho juu

Na Happiness Katabazi

MACHO na masikio ya Watanzania wengi leo yataelekezwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambayo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelezi Mkoa wa Dar es Salaam, ASP Abdallah Zombe (55) na wenzake wanane.


Zombe na wenzake wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

Kesi hiyo ambayo imedumu kwa takriban miaka mitatu, imekuwa gumzo jijini Dar es Saalam kutokana na idadi kubwa ya watu wanaojitokeza pindi inaposikilizwa.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, ambaye amekuwa akiisikiliza kesi hiyo tangu ilipofunguliwa mahakamani hapo mwaka 2007, ndiye anayetarajiwa kutoa hukumu inayongojewa kwa hamu kubwa.

Juni 9, 2006, Zombe alikamatwa na kuunganishwa na washitakiwa wenzake katika kesi hiyo ya mauaji ambayo awali ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kisha kuhamishiwa katika mahakama hiyo ya juu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Washitakiwa wenzake sita, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu kwa mara ya kwanza Februari 20, mwaka 2006, ikiwa ni siku chache tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza kusoma ripoti ya Tume ya Jaji Mussa Kipenka ambayo katika uchunguzi wake ilibaini waliouawa hawakuwa majambazi.

Jaji Kipenka ambaye alikuwa Mwenyekiti wa tume hiyo wakati Katibu wake alikuwa Mwanasheria wa Serikali, Eliezer Feleshi ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), tume yao iliweza kufanya kazi yake na kuwahoji wananchi mbalimbali.

Baada ya Rais Kikwete kuagiza washitakiwa ambao ni maofisa wa polisi wakamatwe, Jeshi la Polisi liliunda tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Mauaji dhidi ya Binadamu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Sidyen Mkumbi, ambayo nayo ilihoji baadhi ya wananchi walihojiwa katika Tume ya Kipenka na baada ya kumaliza uchunguzi wake jamhuri ilifungua kesi.

Septemba mwaka jana, upande wa mashitaka ulifunga ushahidi wao ambapo jumla ya mashahidi 37 walitoa ushahidi na kutoa vielelezo 23.

Februari 9, mwaka huu, Jaji Salum Massati, aliwaachilia huru washtakiwa watatu katika kesi hiyo ambao ni F.5912 PC Noel Leonard, D.6440 Koplo Nyangelera Moris na E.6712 Koplo Felix Cedrick kwa kuwaona hawana kesi ya kujibu kutokana ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kutowagusa.

Aidha, Jaji Massati, alimuona Zombe na washtakiwa wanane wana kesi ya kujibu kutokana na kuguswa kwa namna moja au nyingine na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Februari 10, mwaka huu, Zombe alianza rasmi kujitetea na katika hali isiyotarajiwa aliangua kilio mara kadhaa kizimbani wakati akijitetea.

Licha ya Zombe kumwaga chozi mara nne akiwa kizimbani, wakati akitoa utetezi wake, alionyesha kujiamini na kunukuu baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi (PGO), Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 1985 na Sheria ya Ushahidi.

Februari 11, mwaka huu, Zombe alimaliza kuhojiwa na mawakili wa serikali na utetezi, na aliibua mapya kwa kudai kuwa barua za washtakiwa wanne katika kesi hiyo walizomwandikia aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Geofrey Shaidi ni mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa na DPP.

Februari 19, mwaka huu, Mahakama Kuu ililazimika kusitisha usikilizaji wa kesi hiyo kutokana na mshtakiwa Lema, kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi wake, kwa sababu ya afya yake kuwa mbaya.

Aprili 3, mwaka huu, aliyekuwa mshitakiwa wa 11 katika kesi hiyo, Koplo Rashid Lema, alifariki dunia katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road alikolazwa kwa zaidi ya wiki tatu.

Mei 5, mwaka huu, Jaji Salum Massati ilitupilia mbali ombi alilowasilisha Zombe la kutaka aruhusiwe kujitetea kwa mara ya pili.

“Kama Zombe akiruhusiwa kujitetea kwa mara ya pili basi washtakiwa wengine watakuwa na haki ya kuomba nao waruhusiwe kujitetea kwa mara ya pili na endapo hilo litatokea, ni wazi kabisa hali hiyo itasababisha kuvurugika kwa mwenendo mzima wa kesi hii na kwa sababu hiyo natupilia mbali ombi lake,” alisema Jaji Massati.
Mei 6, mwaka huu, Mahakama Kuu ilifunga ushahidi wa utetezi.

Mei 7, mwaka huu, mawakili wa utetezi kwa nyakati tofauti waliwasilisha majumuisho yao na kuiomba mahakama hiyo kuwaachia huru wateja wao kwa kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ulijaa mkanganyiko mkubwa na pia ni wa kuunga unga.

Mawakili hao walidai kuwa, mashahidi katika kesi hiyo wameshindwa kuthibitisha kuwa washitakiwa hao walihusika kufanya tukio hilo la mauaji, Januari 14, mwaka 2006.

Juni 25, mwaka huu, upande wa serikali katika kesi hiyo, ulijigamba kuwa umethibitisha kesi hiyo pasipo shaka, hivyo kuiomba mahakama kuwatia hatiani washitakiwa hao kwa makosa waliyoshitakiwa.

Majumuisho hayo ya serikali yaliwasilishwa na wakili, Mugaya Mtaki, ambaye alidai katika kuthibitisha kesi hiyo, walileta mashahidi 37 na kutoa vielelezo 23.

Jaji Massati baada ya kusikiliza majumuisho hayo, aliwaasa wazee wa baraza, kutoa maoni yao kuhusu kesi hiyo kwa kuzingatia ushahidi ulio bora, uliowasilishwa mahakamani hapo na kutozingatia yale yaliyoripotiwa na vyombo vya habari, kwani yameandikwa mengi kuhusu kesi hiyo.

Juni 26, mwaka huu, wazee wa baraza; Magreth Mossi na Nicolus Kimolo, waliiomba mahakama imwachie huru Zombe kwa kuwa hawakumuona na hatia.

Mbali na kuomba Zombe kuachiwa huru, wazee hao pia wameiomba mahakama kumwachia huru mshitakiwa wa 13 katika kesi hiyo, Festus Gwasabi, kwa maelezo kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo dhidi ya washitakiwa hao haukuweza kuthibitisha kuhusika na mauaji hayo.

Wazee hao wa baraza walitoa maoni yao kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na pande zote mbili.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D1406 Koplo Emmanuel Mabula, D8289DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari, D.1317D/XP Festus Gwabusabi.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwaua wafanyabishara hao na dereva teksi katika msitu wa Pande uliopo huko Mbezi Louis, nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu,Agosti 17,2009

No comments:

Powered by Blogger.