Header Ads

MFANYABIASHARA WA MAGARI ATUHUMIWA KUIBA GARI

Na Happiness Katabazi
MFANYABIASHARA wa magari jijini Dar es Salaam, Masoud Seif (32), jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na kesi ya wizi wa gari aina ya Rav 4, lenye thamani ya sh milioni 12.


Mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema , wakili wa serikali Beatrice Mpangala, alidai kuwa mshitakiwa huyo ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa, kuwa yeye na wenzake ambao hawapo mahakamani tarehe na muda usiofahamika walikula njama na kutenda kosa la wizi wa gari.

Mpangala alidai kuwa mshitakiwa huyo na wenzake ambao hawapo mahakamani katika tarehe na muda usiyofahamika walikula njama na kutenda kosa.Wakili huyo wa serikali alidai shitaka la pili ni kwamba Januari 19 mwaka huu, katika Ikombolera Lodge iliyopo Kibamba waliiba gari lenye namba za usajili T982 AQP, cheses Na.SXA110022812 aina ya Rav 4 yenye thamani ya milioni 12, mali ya Sauda Maro.

Mshitakiwa alikana shitaka na wakili wake Mgongolwa aliomba mahakama mpatie dhamana kwa sababu kesi inayomkabili ina dhamana ambapo hakimu Lema alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye nusu ya kiasi cha thamani, hata hivyo mshitakiwa alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo ikaairishwa hadi Septemba mosi mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wakati huo huo Mfanyakazi wa mapokezi wa kampuni ya Tanzania Security, Maria Wilson( 27) mkazi Kinondoni ,alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na kosa la kula njama na kujipatia sh milioni 800.

Mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga ,Wakili wa Serikali Mukabatunzi Dereck alidai kuwa kati ya Januria hadi Mei mwaka huu, katika eneo lisilojulikana alikula njama na kujipatia sh milioni 800,000,000.

Dereck alidai shitaka la pili ni mshitakiwa huyo pamoja na wenzake ambao hawapo mahakamani kati ya miezi hiyo katika ofisi za Tanzania Security-IPS Building alikula njama na kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Mussa John, baada ya kujifanya yeye ni msambazaji wa vocha za muda wa maongezi kwa riba ya milioni 360, huku akijua si kweli.

Mshitakiwa huyo alikana shitaka na hakimu Sanga alisema ili mshitakiwa huyo apate dhamana ni lazima atoe hati au fedha taslimu zenye nusu ya thamani ya kiasi hicho cha fedha anachotuhumiwa kuiba, wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya sh milioni 100, na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani lakini hata hivyo mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti, hakimu akaahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 5,2009

No comments:

Powered by Blogger.