Header Ads

UENDESHAJI KESI ZA EPA WALALAMIKIWA

Na Happiness Katabazi

UTARATIBU wa uendeshaji kesi za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, umeanza kulalamikiwa na wadau katika kesi hizo.


Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau wa kesi hizo ambao ni mawakili wa serikali, mawakili wa kujitegemea, mashahidi walisema licha ya nia njema ya Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, kuamua kesi hizo ziendeshwe kwa mtindi wa jopo, lakini uamuzi huo hivi sasa umeonekana kuwa kikwazo kutokana na tabia ya baadhi ya wana jopo kushindwa kuhudhuria kesi.

Walisema kimsingi kesi zinazosikilizwa na jopo haziwezi kuendelea kusikilizwa wala kutolewa maamuzi endapo koramu ya jopo hilo halijatimia, hali inayosababisha ucheleweshaji wa kesi hizo.

“Jaji Mkuu alianzisha utaratibu wa jopo kwa nia njema lakini tunaona sasa utaratibu huu umeanza kuwa kero hata kwetu sisi mawakili, upelelezi umekamilika muda mrefu, mashahidi wanaletwa mahakamani lakini unakuta wanashindwa kutoa ushahidi kwa sababu idadi ya jopo haijakamilika.

‘Sisi tunasema kama mwanajopo amepangiwa kusikiliza kesi hizi tarehe ya kesi asipewe kazi nyingine; aje kuhudhuria kesi aliyopangiwa. Lakini utakuta jopo hilo hilo linatuambua tarehe fulani tulete mashahidi; tunawaleta wakija jopo linasema mwanajopo mmoja hayupo yupo safari ya kikazi ….kwa kweli huu ni usumbufu,” alisema mmoja wa wadau hao.

Kwa upande wao, mawakili wa kujitegemea walisema uamuzi wa kuendesha kesi hizo za jopo ni mzuri ila kuna baadhi ya wanajopo katika baadhi ya kesi wamekuwa ni mabingwa wa kutoa udhuru hali inayosababisha kesi hizo kushindwa kuendelea.

Tanzania Daima ilipozungumza na baadhi ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania juu ya uamuzi wa kesi hizo kusikilizwa kwa utaratibu wa jopo, viongozi hao kwa masharti ya kutotajwa majina yao walisema lengo la utaratibu huo ni kudhibiti rushwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 11, 2009

No comments:

Powered by Blogger.