Header Ads

KESI YA MAHALU YAKWAMA TENA KISUTU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilikubaliana na hoja za upande wa utetezi katika kesi kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 2,inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Italia, Profesa Costa Mahalu na Meneja Utawala na Fedha Fedha,Grace Martin, kwamba hawawezi kuanza kujitetea kwasababu wameishawasilisha hati ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.


Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji wa Mahakama Kuu, Sivangilwa Mwangesi alisema anakubaliana na hoja ya wakili wautetezi Alex Mgongolwa kwamba washitakiwa hawapo tayari kuanza kujitetea kwakuwa wameishawasilisha hati ya nia ya kukataa rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

“Hivyo ni busara ya kisheria mahakama hii ikasubiri hadi rufaa ya washitakiwa itakapotolewa uamuzi hivyo naairisha kesi hii hadi Septemba 8 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Awali Wakili wa TAKUKURU,Ponsian Lukosi na Tabu Mzee waliambia mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya washitakiwa kuanza kujitetea na kwamba wao wapo tayari kwaajili ya shauri hilo kuendelea.

Lakini Wakili Mgongolwa aliambia mahakama hiyo kuwa hawapo tayari kuanza kujitetea kwakuwa wamewasilisha hati ya nia ya kukata rufaa katika mahakama kuu, kupinga uamuzi Jaji Juxon Mlayi alioutoa Juni 8 mwaka huu, ambao ulitupilia mbali ombi la washitakiwa lilokuwa likitaka waachiliwe huru kwa sababu mwenendo mzima wa kesi yao ya msingi ,una dosari za kisheria.

Mgongolwa alidai kuwa licha ya kuwasilisha hati ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu, Juni 22 mwaka huu, hadi sasa bado hawajapatiwa rekodi ya uamuzi wa Jaji Mlayi ili wawe kutumia kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa nchini.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 13,2009

No comments:

Powered by Blogger.