Header Ads

JOPO LA MAHAKIMU LAPANGWA KESI YA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Jopo la Mahakimu Wakazi watatu likiongozwa na Hakimu Edson Mkasimwongo anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwinga, limepangwa kwa ajili ya kusikiliza kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania, Amatus Liyumba.

Katika kesi hiyo, Liyumba anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Licha ya kuwepo kwa jopo hilo, upande wa Jamhuri ulishindwa kuanza kusikiliza kesi hiyo jana kwa madai kwamba waendesha mashitaka wa serikali walikuja kwa ajili ya kuangalia kama jopo la Mahakimu wa kusikiliza kesi hiyo lipo.


Awali Wakili Kiongozi wa Serikali, Justus Mulukozi, aliiambia Mahakama kuwa, upande wa serikali katika kesi hiyo upo tayari kuendelea na kesi hiyo na kuomba iahirishwe.

Kwa upande wake wakili kiongozi wa utetezi Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Onesmo Kyauke na Kate ambao nao ulisema hauna pingamizi na ombi la upande wa serikali lililotaka kesi hiyo iahirishwe.

Aidha, Hakimu Mkazi Mkasimwongo, baada ya kusikiliza hoja hizo alisema kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama za Agosti 11 mwaka huu, zinaonyesha kesi hiyo ilikwenda kwa ajili ya mshitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

“Ila kwa kuwa pande zote mbili katika shauri hili zimekubalina shauri liairishwe, jopo halina pingamizi tunaiairisha kesi hii hadi Septemba 7 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya upande wa serikali kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa,” alisema Mkasimwongo.

Mei 28 mwaka huu, Mulokozi alidai mahakamani hapo kuwa Liyumba anakabiliwa na makosa mawili ya jinai katika kesi hiyo Na.105/2009 kwa matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006 akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Aidha, anadaiwa kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha kosa linaloangukia kwenye shitaka la kwanza.

Liyumba alisomewa mashitaka mapya baada Mei 27 mwaka huu, Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba yake 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina dosari za kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 26,2009

No comments:

Powered by Blogger.