Header Ads

HUYU NDIYE PAPII KATALOGI WA FM ACADEMIA


*Sasa atoka kivyake
*Nyota yake yaanza kung’ara

Na Happiness Katabazi

“HEBU nikiss mpenzi ni mekumiss tii, ebu nikiss mpenzi nimekumiss!”
Ghani hii imetungwa na kuimbwa na rapa mahiri wa bendi ya Fm Academia ‘Wazee wa Ngasuma’, Bahogwerhe Polepole Papy maarufu ‘Papi Katalogi’(29) na kwa wale wapenzi na mashabiki wanaohudhuria maonyesho ya bendi hiyo wamekuwa wakikipata vizuri kionjo hicho.


Hivi karibuni Tanzania Daima ilifanya mahojiano na Papi Katalogi ambaye ni miongoni mwa marapa wanaoanza kupata umaarufu katika medani ya muziki wa dansi nchini.

Mahojiano haya yalifanyika nyumbani kwetu Sinza C na kufanikiwa kumhoji mambo mbalimbali yahusuyo maisha yake na changamoto zinazowakabili wanamuziki wa hapa nchini.

Katalogi ambaye ni mzaliwa wa Bukavu ya Mashariki katika kijiji cha Bagira, nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), anasema anazikubali kazi za wanamuziki wa Tanzania kwamba ni nzuri na hasa wanamuziki wa hip hop.

Anasema tatizo linakuja kwa wasambazaji wa kazi za wanamuziki hao. Katalogi anasema hapa nchini bado kuna tatizo la uhaba mkubwa wa wasambazaji kazi za wanamuziki jambo linalosababisha kushindwa kuuza na kuzitambulisha kikamilifu kazi hizo ndani na nje ya nchi.

“Nashauri apatikane mtu au kampuni ya kusambaza kazi za wanamuziki ipasavyo ili zisikike ndani na nje ya nchi ili mwisho wa siku mauzo ya kazi zao yapande na wanamuziki waweze kupata mikataba ya kufanyakazi nje ya nchi.”

Anasema, “Ujue kwa nini wanamuziki wa nchi ya Uganda wanaendelea kupata mikataba ya kufanya kazi nje ya nchi hiyo ni kwa sababu wana wasambazaji wa uhakika wanaoweza kusambaza kazi zao kikamilifu na ndiyo maana hata zinapigwa mara kwa mara kwenye televisheni nyingi duniani. Ni bora pia kusambaza katika kituo kikubwa barani Afrika cha MTV.

Licha ya siku hizi baadhi za nyimbo za mwanamuziki wa hapa nyumbani, Ambwene Yesayah ‘AY’, kupigwa katika televisheni hiyo, tunasema bado,” anasema Katalogi.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili wanamuziki mbalimbali nchini, anasema changamoto mojawapo ni kufanya kazi katika mazingira magumu kwani nyimbo zilizobeba ujumbe muhimu zinakuwa hazipewi vipaumbele kwenye vituo vya utangazaji na badala yake baadhi ya nyimbo ambazo maudhui yake hayatoi funzo lolote kwa jamii ndizo zinazopigwa kila wakati kwenye vituo hivyo na kuongeza kuwa yote hiyo ni kwa sababu nyimbo hizo zisizo na maudhui mazito walioziimba wanasaidiwa na watu wenye fedha.

Licha ya rapa huyu kuwa mwajiriwa wa bendi ya Fm Academia, katika harakati zake za kujiongezea kipata yupo mbioni kuzindua albamu yake yenye nyimbo saba itakayotambulika kwa jina la ‘Tetemeko’ ambapo baadhi ya nyimbo zilizo katika albamu hiyo, zinaendelea kutamba katika vituo mbalimbali vya utangazaji hapa nchini.

Katika albamu hiyo Katalogi ambaye ni mtoto wa mwanajeshi mstaafu wa jeshi la DRC, anasema ameshirikisha wanamuziki mbalimbali akiwemo Maunda Zorro,Toskani Biavanga wa Fm Academia, Cantona ‘mgogo wa mazizini’ toka bendi ya Daimond Musica na wengine wengi.

Akizungumzia historia ya maisha yake anasema yeye alizaliwa Septemba 20 , 1980; alianza muziki akiwa na umri wa miaka 14 huko Bukavu. Akiwa na umri huo alijiunga na watoto wenzake waliokuwa wakicheza wote mitaani na walianza kuimba nyimbo mbalimbali na wasanii wakubwa , na mara baadaye walipoonekana wana vipaji waliweza kupata mialiko ya kuimba jukwaani katika maonyesho mbalimbali nchini DRC.

Mwaka 1996 Katalogi alianza kuimba kwenye bendi iitwayo Haliga Tar Musica, walikuwa wanapiga muziki wa dansi na kudumu na bendi hiyo kwa miaka miwili; baada ya hapo alihamia katika bendi iliyokuwa ina jina kubwa ya Quartier Desas.

“Nilipokuwa kwenye bendi hiyo sikuweza kutunga nyimbo na baada ya miaka mitatu baadaye, mwaka 2001, nikahamia bendi iliyoanzishwa na vijana iliyokwenda kwa jina la Influence Baboul ambapo nilidumu nayo kwa miaka mitano,” anasema.

Anasema akiwa hapo alitunga wimbo mmoja ulioitwa Balcania na ulikubalika sana ambapo wimbo huo sasa ameuboresha kwa kuweka maneno ya lugha ya Kiswahili ambao umebeba ujumbe wa kuhamasisha amani duniani unaitwa ‘Tetemeko la ardhi’.

Alisema licha ya kutunga kibao hicho pia alitunga kibao kingine kwa lugha ya Kilingala kiitwacho ‘Umeniacha Mpweke’.

Mwaka 2006 alisafiri kwenda Kigali nchini Rwanda alikojiunga na bendi ya Armeee Rouge’ Jeshi jekundu’ na kudumu nayo kwa mwaka mmoja kisha akarudi Kongo kwenye kikundi chao cha vijana na kuendelea kufanya maonyesho kwenye kumbi mbalimbali za starehe.

Anasema ilipofika mwaka 2007 akiwa Kongo, alikutana na mwanamuziki wa FM Academia, Roger Muzungu, ambaye alimweleza kuwa alikuwa amekwenda huko kumtafuta na kwamba alikuwa ametumwa na uongozi wa bendi ya Fm kumchukua na kumleta nchini ili aweze kujiunga na bendi hiyo.

“Nilipoingia Fm nilikuta wameisharekodi albamu ya ‘Dunia Kgeugeu’ ila katika albamu ijayo ya bendi hiyo nimetunga rapu mpya kama zifuatazo ‘Mgongo Tingisha’, ‘Weka mikono kichwani’ , ‘Niko sawa nikurukie’ na ‘Hebu ni kiss mpenzi nimekumiss’,” anasema Katalogi ambaye ni baba wa mtoto mmoja aitwaye Frorence Pole Pole (9).

Katika albamu ijayo hajatunga wimbo na kuongeza kuwa katika kipindi hicho kifupi ameweza kupata mafanikio kidogo na kuweza kurekodi nyimbo na kwamba mashabiki wa FM wanamkubali.

Katalogi alisoma shule ya Bukavu inayofahamika kwa jina la SeniBasheka na ilipofika mwaka 2003-2004 alijiunga na chuo cha sheria Institute Superier du Pedagogie(ISP), ambapo alikatisha kozi hiyo baada ya kupata matatizo ya kifamilia.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 28,2009

No comments:

Powered by Blogger.