Header Ads

SPIKA SAMEUL SITTA NI FISADI PIA?

Na Happiness Katabazi

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, ni askari wa mwavuli aliyejeruhiwa. Aliamini kwamba atakapodondoshwa na mwavuli wake atakuta maadui zake wamelala ama hawapo.


Lakini, mtu anayejua historia ya serikali ya Awamu ya Nne, atajua ni serikali ya makundi; kundi la mtandao ambalo Sitta ni mshiriki wa jikoni. Limesambaratika. Sasa, juhudi zinafanyika kuliunganisha tena.

Kiini cha kusambaratika kwa kundi la mtandao ni Sitta, pale aliposhindwa kumlinda jemedari wa mtandao aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kwa kuwa Sitta ni mwanamtandao, anawajua maadui zake.

Sitta, asijaribu kuvamia matale wakati wa kuzama majini. Gazeti la Tanzania Daima na vyombo vya habari vingine, viliandika kuhusu tuhuma za spika huyo ambazo ni matete, hayahusiki kabisa na gharika lililojaza mto unaomzamisha Sitta.

Kwa kifupi, tunasema kila kitu kina mwanzo na mwisho wake. Mtandao ulianza kama kikundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kikundi hicho kilijenga maadui ndani ya chama hicho tawala katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Wale walioshindwa katika mchakato wa uchaguzi ule ndani CCM, bado wanaishi na bado wamo kwenye siasa ndani ya chama alichomo Spika Sitta. Ndiyo maana nasema, iweje sasa Spika anavamia kila mtu na kumfanya adui yake?

Kwani kule ndani ya CCM ambako wako maadui zake na wiki iliyopita alikiri bungeni kwamba, anataka aongezewe ulinzi, sasa Tanzania Daima tuna mamlaka gani nao? Je, hao ndio anaodai wametuhonga ili tumpige vita?

Tangu lini gazeti hili limekuwa chombo cha makundi ya CCM? Au Sitta atuambie hiyo ndiyo mbinu chafu inayotumiwa na wanamtandao wenzake kuwahonga baadhi ya wanahabari? Maana isingekuwa hivyo, Spika asingekuwa na ubavu wa kulizungumzia hilo bungeni.

Basi ni vema Spika Sitta, atuambie katika hao maadui zake anaowajua wamemhonga nani ambaye ni mfanyakazi wa gazeti hili? Kama huna ushahidi wa hili, basi kiongozi wa heshima na hadhi yako, hatazamiwi kuzungumza lugha ya maandazi. Acha, itakuondolea heshima yako.

Lakini, najadili suala zima la jinsi kundi la mtandao linavyofanya kazi baada ya kutwaa madaraka mwaka 2005 hadi sasa. Inasemekana, Sitta alitazamia kuwa Waziri Mkuu lakini aliyeteuliwa ni Lowassa.

Sitta, akaambulia uspika. Hicho kikawa chanzo cha uadui ndani ya mtandao uliomsaidia Rais Jakaya Kikwete, kabla na wakati wa kampeni kuhakikisha anaingia Ikulu. Nani asiyelijua hilo? Sasa vita ya makundi haya mawili, kati ya Spika na Lowassa, mara kusinzia, kuibuka na kuwa kali sana.

Sasa ni vema spika asituchanganye Tanzania Daima na wenzake katika mapambano yao kwani walipojitenga kama wanamtandao na wakagawana vyeo, hatukuwepo.

Ikiwa wanamtandao wanamwona Sitta hawafai, ni nani wa kumsaidia vita hiyo? Ninachojua tunayo Serikali ya Awamu ya Nne ambayo ni serikali ya 'kishikaji’, rais aliteua baadhi ya marafiki zake kushika nafasi mbalimbali ndani ya serikali.

Nakushauri Spika Sitta, usimtafute mchawi. Ukihisi wadhifa huo mkubwa ndani ya Bunge unakushinda, nenda kalie kwenye kundi lako kupitia vikao viwe halali au haramu.

Najua kwamba wanamtandao hawajaweza kutudhihirishia na kututhibitishia kuwa ni waadilifu kwani wengi wao wanaandamwa na kashfa ya matumuzi mabaya ya ofisi za umma na madaraka, wizi wa rasilimali za nchi, uuzaji dawa za kulevya, uzembe na kusaini mikataba dhalimu ambayo sasa inaligharimu taifa.

Tuhuma zilizo mitaani zinazomhusu Spika hazinishtui na wala sioni jambo la ajabu kwani ndege wenye manyoya yanayofanana huruka pamoja.

Sitta, unalalamika kwa sababu gani wakati wewe pia ni mwanamtandao? Kama wanamtandao wengine ni wala rushwa, wabadhirifu au wazembe, kwa nini nawe usiwe?

Ingekuwa vema Spika utumie muda wako kupinga tuhuma zinazoelekezwa kwako kwa hoja na vielelezo badala ya kuvisingizia vyombo vya habari vinavyoandika tuhuma kwa kusema eti vimehongwa na maadui zake.

Sisi Tanzania Daima hatuwajui maadui zake Sitta, hawajatuhonga ila ni kweli wiki iliyopita tuliandika habari kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake kwa nia njema; naye tulimpa fursa ya kujibu tuhuma hizo.

Kwa kuwa kashfa zinazowaandama wanamtandao ni sawa na kundi la wachawi wanaotuhumiwa kushiriki kula nyama ya maiti, Sitta kama mshiriki wa kundi hilo ni msafi kiasi gani?

Naomba kutoa hoja.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774 494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 5,2009

No comments:

Powered by Blogger.