Header Ads

WASHTAKIWA PEMBE ZA NDOVU WAKWAMA KISUTU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema haina mamlaka ya kisheria ya kutoa dhamana kwa washtakiwa sita wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha nje ya nchi kilo 11,061 za pembe za ndovu zenye thamani ya sh 791,514,020kinyume cha sheria.


Uamuzi huo ulitolewa jana na mahakimu Anisetha Wambura na Mohamed Mchengelwa wanaosikiliza kesi hizo.

Akitoa uamuzi wake, Hakimu Wambura alisema mashtaka yanayowakabili washitakiwa hao kisheria yana dhamana na kwamba Mahakama ya Wilaya na Mkoa zinaruhusiwa kutoa dhamana pale thamani ya mali inapokuwa chini ya sh milioni 10.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Wambura aliushauri upande wa utetezi kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi hiyo iliyopo mbele ya Wambura washtakiwa ni Eladius Colonerio (39) ambaye ni Mkurugenzi wa Team Freight (T) Ltd, Gabriel Balua (33), Meneja Usafirishaji wa nje na ndani ya nchi wa kampuni hiyo, na Shaban Yabulula (44) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kigoma M. N Enterprises (T) Ltd, wanaokabiliwa na mashtaka 11 na nyara hizo za serikali zina thamani ya 684,827,000 mali ya serikali.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mchengelwa, alisema anakubaliana na upande wa mashtaka kwamba baadhi ya makosa yanayowakabili washtakiwa ni ya uhujumu uchumi na hivyo kusema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana isipokuwa Mahakama Kuu.

Washtakiwa katika kesi iliyopo mbele ya Hakimu Mchengelwa ni Nebart Kiwale (45) ambaye ni Mkurugenzi wa Uplands Freight Forwarders (T) Ltd, Gabrile Balua (33) wa Team Freight, Issa Lweno (40) wa Uplands Freight Forwarders, Eladius Colonerio (39), Mkurugenzi wa Team Freight (T) Ltd na Abubakar Hassan (38).

Washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha pembe za ndovu kiasi cha kilo 1,483, zenye thamani ya sh 106,687,020 kwenda Manila, Phillippines kinyume cha sheria. Kesi hizo zitatajwa Agost 17.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 4,2009

No comments:

Powered by Blogger.