Header Ads

SHAHIDI:FEDHA ZA EPA SI MALI YA SERIKALI

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa tatu katika kesi ya wizi wa zaidi ya shilingi bilioni tatu, Meneja wa Mabenki ya Kimataifa katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Laison Mwakapenda (65), jana alidai kuwa fedha za Akaunti ya Madeni ya Akaunti ya Medeni ya Nje (EPA) si mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Sambamba na hilo, pia jopo la mahakimu wakazi wanaosikiliza kesi hiyo, linaloongozwa na Samwel Kalua na Winfrida Mutungi, walitoa onyo kali kwa washitakiwa, kwa kuwataka waache tabia ya kukonyeza wananchi wanaoudhuria kesi hiyo na kuchekacheka pindi wawapo kizimbani, na endapo watarudia tena vitendo hivyo mahakama itawafutia dhamana.

“Tangu kesi hii imeanza, nyie washitakiwa mmekuwa mkikonyezana na kuchekacheka ovyo na wananchi waliofika kuudhuria kesi hii, wakati nyie mpo hapo kizimbani wakati kesi hii inaendelea, sasa nasema hii iwe mwanzo na mwisho wenu, mkirudia tena mahakama hii itawafutia dhamana,” alisema Hakimu Mkazi Kalua.

Akitoa ushahidi wake, Mwakapenda alidai kuwa fedha za EPA zilikuwa ni mali ya wafanyabiashara wa Tanzania waliokuwa wakiweka fedha zao NBC, ili benki hiyo iweze kuzibadilisha na kuwa fedha za kigeni kisha kuwalipa wafanyabiashara wa nje ya nchi.
Sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa utetezi, Mabere Marando na shahidi huyo ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Unaposema EPA iliwekewa Data base kwa rahisi unamaanisha nini?
Shahidi: Ni kumbukumbu zote za EPA zilizohifadhiwa NBC na kisha zikahamishiwa Benki Kuu.
Wakili: Hizi fedha za EPA ni za Watanzania walionunua bidhaa kwa wafanyabiashara wa nje ya nchi waka-deposite fedha za malipo NBC ili NBC iweze kuwalipa wafanyabiashara wa nje kwa dola, kwa hiyo utakubaliana fedha za EPA si mali ya BOT wala NBC?
Shahidi: Ni kweli.
Wakili: Nitakuwa sahihi nikisema BoT walikuwa ni ‘custodian’ tu wa hizo fedha?
Shahidi: Ni kweli BoT walikuwa ni walinzi tu wa zile fedha.
Wakili: Shahidi umekuja na register yoyote au ushahidi wowote kuonyesha wafanyabiashara wa nje (supplies of goods) wanaodai fedha hizo?
Shahidi: Sina.
Wakili: Unaweza kuithibitishia mahakama kuwa wafanyabiashara wa nje waliokuwa wanadai fedha hizo kama kweli wanadai?
Shahidi: Sina.
Wakili: Una ushahidi wowote unaoonyesha waliokuwa wakidai fedha za EPA kama walilipwa au la?
Shahidi: Sina.
Washitakiwa katika kesi hiyo wanaotetewa na Mabere Marando, Majura Magafu na Gabriel Mnyere wakati mawakili wa serikali ni Fredrick Manyanda na Vitalis Timon, ni Farijala Hussein, Rajabu Maranda na Ajay Somani, wote ni wafanyabiashara na Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Lalika, ambao ni maofisa wa Benki Kuu.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita ya kula njama, kughushi na kujipatia ingizo toka Benki Kuu, huku wakionyesha Kampuni ya Mibale Farm ilipewa idhini ya kukusanya deni la Kampuni ya Lakshmi Textile Mills Co. Ltd ya India.
Kesi imeahirishwa hadi Septemba 21, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Agosti 22,2009

No comments:

Powered by Blogger.