Header Ads

VIGOGO DECI WAPATA DHAMANA

Na Happiness Katabazi

BAADA ya kusota rumande kwa muda wa miezi miwili gerezani, hatimaye washitakiwa katika kesi inayowakabili vigogo wa Taasisi ya Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), wamepata dhamana.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Waliarwande Lema baada ya Wakili Kiongozi wa Serikali, Justus Mulokozi na Prosper Mwangamila kuiambia mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka amewasilisha hati ya kutengua kiapo chake cha awali kilichokuwa kimewanyima dhamana washitakiwa hao.

Hakimu Lema alisema kutokana na atatoa dhamana kwa yenye masharti ya kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya sh milioni 10, na mmoja k ya wadhamini awe anaishi Dar es Salaam, kusalimisha hati za kusafiria mahakamani pamoja na washitakiwa kutofanya mikutano ya hadhara.

Hata hivyo, washitakiwa watatu ndio walioweza kutimiza masharti ya dhamana baada ya kudhaminiwa na walimu wanne wa shule za msingi na sekondali na wachungaji wawili wa kanisa la Pentekosi.

Washitakiwa waliopata dhamana ni Jackson Mtares Dominic Kisendi, Timotheo ole Loitgimnye na Samwel Mtares.

Wakati mshitakiwa ambao hawajapata dhamana baada ya kushindwa kutimiza masharti ni Arbogast Kipilimba na Samwel Mtalis ambapo wataletwa leo mahakamani kwa ajili ya kukamilisha masharti ya dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Agosti 26 mwaka huu, itakapotajwa.

Aidha baadhi ya wafuasi wa DECI,ndugu jamaa wa washitakiwa hao waliokuwa wamepaki magari katika viwanja vya mahakama hiyo, waliwalaki ndugu zao na kuwaingiza kwenye gari lenye namba za usajili T186 AY aina ya Mark Two.

Juni 17 mwaka huu, DPP-Feleshi aliwasilisha kiapo chake katika mahakama hiyo cha kuzuia dhamana ya washitakiwa kwaajili ya usalama wa washitakiwa na maslahi ya Jamhuri.

Juni 12 mwaka huu, Wakili Kiongozi wa Serikali Justus Mlokozi alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na mashitaka mawili, shitaka la kwanza ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1)(3)cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu , na shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha Na.5 ya 2006.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Agosti 13,2009

No comments:

Powered by Blogger.