DAVID MATTAKA KIZIMBANI
Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATLC), David Emmanuel Mattaka jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa matatu likiwemo kosa la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na Sheria na kifungu 31 Na.11 ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007.
Mbali na Mattaka anayetetewa na wakili wa kujitegemea Peter Swai, washtakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha Elisaph Mathew Ikomba na Mkazi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji anayetetewa na wakili Alex Mgongolwa walifikishwa mahakamani hapo jana saa nne asubuhi na makachero wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa(TAKUKURU), chini ya ulinzi mkali wa makachero hao.
Wakili wa Takukuru, Ben Lincoln aliyekuwa akisaidiwa na wakili wa serikali Oswald Tibabyekomya mbele ya Hakimu Mkazi Ritha Tarimo aliyasoma mashtaka hayo
Kuwa ni kosa la kwanza ambalo linawahusu washtakiwa wote ni kwamba washtakiwa wote kwa pamoja walishindwa kutunza kumbukumbu za mawasiliano ya manunuzi waliyokuwa wakifanya na mtoa huduma kinyume na kifungu cha 55(3),87(1)(f) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma Na. 21 ya mwaka 2004 na kanuni ya 17(1) ya Sheria ya Manunuzi (Goods,Works,Non-Consultant Services and Disposal of Public Asets by Tender) Regulation,G.N. No.97 of 2005.
Wakili Lincoln alidai shtaka la pili ambalo pia linawakabili washtakiwa wote ni la kushindwa kutimiza matakwa ya vifungu vya Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni zake kinyume na kifungu cha 87(1)(f) cha Sheria ya Manunuzi ya umma ya mwaka 2004.
Na shtaka la tatu lina mkabili Mattaka peke yake ni matumuzi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa ya mwaka 2007.
Lincoln alidai kuwa maelezo ya shtaka la kwanza kuwa Juni 2007 na JUlai 2007 ndani ya jiji la Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja kupitia nafasi zao wote kwa pamoja walishindwa kutunza rekodi ya tangazo la tenda idadi ya magari 26 waliyoyanunua ambapo magari hayo yalinunuliwa na shirika hilo yakiwa tayari yamekwishatumika(magari mitumba) kutoka kwa kampuni ya Bin Dalmouk Motors Co.Ltd yenye ofisi zake nchini Dubai katika Falme za Kiarabu, kampuni ambayo ilipewa tenda shirika hilo kuleta magari hayo 26 ambayo ni mitumba.
Wakili Lincoln alidai kuhusu shtaka la pili ambalo ni la kushindwa kutimiza masharti ya sheria hiyo ya Manunuzi ya mwaka 2004 kuwa kati ya Julai 2-Agosti 23 mwaka 2007 wote kwa walishindwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 87(1)(f) cha Sheria ya manunuzi ya umma na Kanuni ya 58(3) sheria hiyo kwa kutumia kampuni ya umma ya ATLC walinunua magari ya mitumba 26 toka kwa kampuni ya Bin Dalmouk Motors Co.Ltd ya Dubai kinyume na kifungu hicho ambacho kinakataza ofisi yoyote ya serikali kununua bidhaa ambazo zilizokwishatumia.
Wakili Lincoln alidai shtaka la tatu la matumizi mabaya ya madaraka linalomkabili Mattaka peke yake ambaye amestaafu hivi karibuni utumishi wa umma, alitumia madaraka yake vibaya kwa makusudi na kuagiza magari hayo ya mitumba 26 huku akijua kufanya hivyo ni kwenda kinyume na vifungu hivyo vya sheria ya manunuzi.
Hata hivyo washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na wakili wa serikali Tibabyekomya alidai kuwa upelelezi bado unaendelea na kwamba makosa yanayowakabili washtakiwa yanadhaminika na hivyo akaiomba mahakama iwapatie dhamana washtakiwa kwa kutumia kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002,ambayo yanamtaka mshtakiwa atoe mahakamani nusu ya fedha taslimu au hati ya mali isiyoamishika yenye thamani ya nusu ya kiwango anachotuhumiwa kuiba, kuharibu au kusababisha hasara.
Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa vikali na mawakili wa utetezi Peter Swai na Alex Mgongolwa ambao walidai kimsingi mashtaka yanayowakabili wateja hao si ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, kusababisha hasara wala wizi hivyo kamwe dhamana ya washtakiwa hao haiwezi kuangukia chini ya kifungu hicho na kuiomba mahakama ikatae hoja hiyo ya mawakili wa jamhuri.
Akitoa uamuzi wake Hakimu Tarimo alisema anakubaliana na hoja ya mawakili wa utetezi kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hayo hayahusiani na fedha, kusababisha hasara, wizi wala uharibu wa mali ya umma.
“Hivyo masharti yangu ya dhamana ni haya hapa kuwa ili kila mshtakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambapo kila mdhamini atapaswa asaini bondi ya milioni 10 kila mmoja na kwa anaiarisha kesi hiyo hadi Desemba 5 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa”alisema Hakimu Tarimo.
Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana ambapo Mattaka alitolewa ndani ya chumba hicho cha mahakama kwa kasi huku akisindikizwa na ndugu zake na maaskari na kisha kuondoka ndani ya eneo hilo la mahakama.
Hivi karibuni Mattaka alistaafu kwa mujibu wa sheria utumishi wa umma akiwa na cheo cha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la ndege nchini.
Rais Jakaya Kikwete alipochaguliwa kuwa rais wa Tanzania Desemba 21 mwaka 2005 muda mchache baadaye alimteua Mattaka kuwa mkurugenzi wa shirika hilo la ATCL na kisha baadaye kumteua Mattaka kuwa Mjumbe wa Tume ya Rais ya Kikosi Kazi cha Kurekebisha Shirika la Bima la Taifa.
Wakati Rais Kikwete akimteua Mattaka kushika nyadhifa hizo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne, wananchi mbalimbali walilaani uteuzi huo bila mafanikio.
Na kabla ya Rais Kikwete kumteua Mattaka kushika nyadhifa hizo,Rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alikuwa amemstaafisha Mattaka kwa manufaa ya umma.Na wakati Mkapa anamstaafisha mshtakiwa huyo kwa manufa ya umma alikuwa akishikilia cheo cha Ukurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pesheni wa Mashirika ya Umma(PPF).
Chanzo:Gazeti la Tanzania Jumatano, Novemba 23 mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment