Header Ads

MDOGO WA ROSTAM AZIZ KIZIMBANI KWA DAWA ZA KULEVYA

Na Happiness Katabazi


ASSAD Aziz Abdulasul ambaye ni mdogo wa mwanasiasa maarufu nchini, Rostam Aziz, anayetuhumiwa kusafirisha kilo 92.2 za dawa ya kulevya aina ya heroine yenye thamani ya sh bilioni 2, jana alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga na kusomewa maelezo ya awali.


Mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Kipenka Mussa, wakili mwandamizi wa serikali Biswalo Mganga aliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ya jinai Na.1/2011 ilikuja mahakamani hapo kwa mara ya kwanza jana ikitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Tanga kwa ajili ya maandalizi ya kuhamishiwa katika mahakama hiyo ya juu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na jana upande wa jamhuri uliwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

Wakili wa mganga aliwataja washtakiwa hao mbali na Assad kuwa ni Kileo Bakari Kileo, Yahya Makame, Mwamadali Podadi ambaye ni raia wa Iran, Salum Mparakesi, Saidi Ibrahim Hamis na Bakari Kileo ‘Mambo’ ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na Edward Chuwa.

Akiwasomea maelezo hayo ya awali, Wakili Mganga alieleza kuwa washtakiwa wote kwa pamoja kati ya Januari mwaka 2009 hadi Machi 8 mwaka 2010 walikula njama na kusafirisha kiasi hicho cha dawa za kulevya na kuziingiza nchini.

Aidha wakili Mganga alidai kuwa kosa la pili linalowakabili washtakiwa hao ni kusafirisha dawa hizo za kulevya na kukamatwa na askari wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, mkoani Tanga, Machi 8, 2010.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo hayo ya awali, walikana mashtaka hayo yanayowakabili na badala yake walikubali majina tu kuwa ndiyo yao.

Kwa upande wake Jaji Kipenka aliahirisha kesi hiyo hadi kikao kingine cha Mahakama Kuu na akaamuru washtakiwa wote kurudi mahabusu kwa sababu kisheria, makosa yanayowakabili washtakiwa hao hayana dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Novemba 12 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.